Mume ahukumiwa miaka 20 jela kwa kumbaka mkewe – DW – 19.12.2024

 

Tukio hilo lilizigusa nyoyo za watu wengi nchini Ufaransa na kuushanga ulimwengu, pale Bwana Dominique Pelicot mwenye umri wa miaka 72 aliposhtakiwa kwa makosa ya ubakaji dhidi ya mkewe Bi Gisele. Si hayo tu, inaaminika kwamba kwa zaidi ya muongo mmoja, Bwana Dominique alikuwa akimuwekea kilevi bi Gisele na kuwasaka mtandaoni wanaume wengine walioshirikiana kumbaka mkewe.

Kesi hiyo ilifuatiliwa kote nchini Ufaransa kutokana na uamuzi wa bi Gisele wa kuruhusu tangu mwanzo, kesi hiyo kuwa wazi kwa umma. Mumewe wa zamani Dominique Pelicot, alikiri makosa hayo na ndipo mahakama katika mji wa kusini mwa Ufaransa wa Avignon kumkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela. Wakili wake amesema haondoi uwezekano wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Soma pia: Mwanaume wa Kifaransa akiri “mimi ni mbakaji”

Hakimu Roger Arata amesema Dominique Pelicot hatoruhusiwa kuachiliwa hadi atakapokuwa ametumikia thuluthi mbili ya kifungo chake. Washtakiwa wengine wapatao 50 wamehukumiwa pia hadi miaka 15 jela, hukumu ambayo mashirika ya haki za wanawake pamoja na watoto watatu wa Bi Gisele Pelicot wanaiona kuwa haitoshi. Washtakiwa wengine sita waliondoka wakiwa huru baada ya Mahakama kutowakuta na hatia yoyote.

Gisele Pelicot. “Mwanamke shujaa”.

Gisele Pelicot
Gisele PelicotPicha: Imago/Jonathan Rebboah

Lakini katika maoni yake ya kwanza baada ya hukumu hiyo, Gisele Pelicot  amesema anaheshimu uamuzi wa mahakama hiyo. Kwa sasa mwanamke huyo anachukuliwa kama shujaa wa utetezi wa haki za wanawake ndani na nje ya Ufaransa kwa kukataa kufedheheshwa huku akikabiliana mbele ya vyombo vya sheria na wale waliomdhulumu haki yake ya faragha. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amepongeza ushujaa na ujasiri wa mwanamke huyo kwa kupigania haki yake.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Bi Gisele amesema wakati wote wa mkasa huu amekuwa akiwawaza watoto wake watatu, familia zote zilizohusishwa na wale ambao bado hawawezi kuyaweka hadharani yale wanayoyapitia majumbani mwao.

Ameongeza kuwa anatumai masaibu na matokeo yake yatabadilisha mtazamo wa jamii na akasema kuwa ana imani kwamba kila mtu, iwe wanawake na wanaume, wataweza kuishi kwa maelewano na heshima.

 

Related Posts