Dar es Salaam. Mwili wa John Tendwa aliyewahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini umeagwa leo, huku waombolezaji akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakieleza namna alivyoanzisha uhakiki wa vyama vya siasa.
Wameeleza uhakiki huo ulipoanzishwa baadhi ya vyama havikuukubali lakini leo ndiyo uhai wa vyama vyote.
Tendwa ambaye mwili wake utazikwa kesho Desemba 20, 2024 alifariki dunia Desemba 17 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kabla ya waombolezaji kuaga mwili wa Tendwa, kulifanyika ibada iliyoongozwa na Padri Patrick Msimba wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Viongozi wengine waliokuwepo kwenye viwanja vya Karimjee kulikofanyika shughuli ya kuaga mwili ni Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderianaga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika shughuli hiyo amesema msingi alioujenga Tendwa kwenye vyama vya siasa ndiyo unaendelezwa hadi sasa.
Majaliwa amesema Rais Samia ameshindwa kuungana na waombolezaji kutokana na kuwa na wageni kutoka nje ya nchi.
“Tuna jukumu la kuenzi mazuri aliyoyafanya katika utumishi wake, alijenga demokrasia kwenye vyama vya siasa wakati wa utendaji wake,”amesema Majaliwa.
Kwa upande wake Kikwete, amesema alipochaguliwa kuwa Rais mwishoni mwa mwaka 2005 alimkuta Tendwa akiwa msajili na alifanya naye kazi kwa miaka minane hadi alipostaafu.
“Alikuwa mkweli, hata chama chetu (CCM) pamoja na ukubwa, Tendwa alikuwa akiona mambo hayapo sawa ananiambia Rais nakwenda kuwaambia ukweli.
“Vivyo hivyo hata kwa wapinzani, alikuwa akiwambia ukweli, ndiyo sababu alipokwenda CUF (kuhakiki) walimfungia lakini yeye aliweka mkazo lazima uhakiki ufanyike,” amesema Kikwete.
Amesema katika miaka minane aliyofanya kazi na Tendwa aliwasaidia kujenga demokrasia.
“Alipougua, mwanawe alinipigia simu akasema baba anaumwa na kwa nyakati mbalimbali amekuwa anakutaja, hivyo tumeona tukupe taarifa.
“Nikauliza hali yake ikoje? akasema ni ngumu yupo ICU, sikuwa nchini niliporejea Jumamosi nilipanga kwenda kumuona lakini nikapata taarifa amefariki,” amesema Kikwete na kutoa pole kwa familia ya Tendwa.
Akitoa salamu za familia, Mchungaji David Tendwa amemshukuru Rais Samia, Waziri Mkuu na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kuwa nao bega kwa bega kipindi cha kuuguza hadi mauti ya mpendwa wao.
Tendwa ambaye ameacha mjane na watoto wanane alihudumu kwenye nafasi ya msajili wa vyama vya siasa kwa miaka 12 mfululizo akichukua mikoba ya hayati George Liundi.
Alianza kutumikia nafasi hiyo Mei 2001 hadi Agosti 2013 na kukabidhi kijiti kwa Jaji Francis Mutungi anayehudumu hadi sasa.
Hadi alipofariki dunia Tendwa alikuwa mshauri wa sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika masuala ya siasa na uchaguzi, pia alikuwa mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Amewahi kuwa mwalimu Daraja A, pia Wakili wa Serikali Mkuu katika Wizara ya Sheria na Katiba, naibu mwenyekiti katika Mahakama ya kazi na mkurugenzi wa utafiti na mafunzo wa wizara hiyo.
Aliacha ofisi na vyama 23
Akizungumza namna Tendwa alivyomuachia ofisi ya msajili mwaka 2013, Jaji Mutungi amesema aliiacha ofisi ya msajili ikiwa na vyama 23 vya siasa.
“Hivi sasa vipo vyama 19, vingine tumeving’oa kwa sababu havikidhi,” amesema.
Jaji Mutungi amesema Tendwa ndiye alimpokea ofisini na kuwa mwalimu na mshauri wake katika kazi anayoifanya sasa.
“Alikuwa kiongozi mwenye maono aliyehakikisha misingi ya vyama vingi inajengwa kwa demokrasia na uwazi.
“Katika kipindi chake, ndipo zoezi la uhakiki lilianza, CUF pamoja na kwamba walimfungia kwenye chumba wakilikataa zoezi hilo, lakini sasa ndiyo linaangalia uhai wa vyama,” amesema Jaji Mutungi.
Hayati Tendwa katika mahojiano aliwahi kueleza moja ya matukio aliyoyakumbuka ni kufungiwa ndani ya ofisi za CUF Zanzibar.
Alisimulia mwaka 2001, alifungiwa ndani ya ofisi hizo huku milango na madirisha yakiwa yamefungwa, isipokuwa sehemu ndogo tu ya madirisha ya juu. Wafuasi wa CUF walimtuhumu kuwa yeye ni mtu wa CCM.
“Wakanifungia ndani, wakaniambia nisiseme chochote. Kwa zaidi ya saa mbili na nusu walizungumza wao, sikutakiwa kujibu chochote. Baada ya kumaliza, walinipa nafasi ya kuzungumza na nikatumia saa moja na nusu kueleza msimamo wangu. Tukio hilo lilinijengea heshima kwa CUF na walitambua kuwa mimi si mtu wa CCM kama walivyokuwa wanadhani,” alieleza Tendwa katika mahojiano hayo.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema Tendwa akiwa msajili alisimamia demokrasia ndani na nje ya vyama vya siasa.
“Ili kumuenzi tunawajibu wa kuendelea kuvisimamia na kuvikuza vyama vyetu katika demokrasia,” amesema.
John Cheyo, Mwenyekiti wa UDP amesema katika miaka 30 aliyokaa kwenye siasa, Tendwa ana maua yake kwa chama hicho.
“Aliwahi kumuondoa kijana mmoja mvamizi kwenye chama chetu,” amesema Cheyo.
Juma Ally Khatibu, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa amesema wanamkumbuka Tendwa na namna alivyopunguza migogoro hasa ule uliowahi kutokea kati ya CCM na CUF akimtaja kujenga mshikamano katika nyakati ambazo taifa lilihitaji busara.