Dar es Salaam. Jeshi la Polisi la Tanzania limetajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora 10 ya Afrika kwa kwa kutumia weledi na kuheshimu haki za wananchi.
Katika kigezo hicho, nchi ya Burkina Faso imeongoza ikifuatiwa na Morocco, Niger, Benin, Mali, Senegal, Tanzania, Madagascar, Mauritania na Mauritius.
Mbali na kigenzo hicho, pia Tanzania imeongoza kwa wananchi kuwa na imani na polisi, ikishika nafasi ya pili kwa wananchi kutohofia usalama wao.
Kwa matokeo hayo, Tanzania imezipita baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zikiwamo Kenya na Uganda ambazo kwa ujumla zimefanya vibaya katika vigezo mbalimbali.
Hayo yamo kwenye ripoti inayoitwa “Watekelezaji Sheria au Wavunjaji Sheria?” iliyotolewa na taasisi ya Afrobarometer Januari 2024 iliyofanya uchambuzi kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.
Utafiti huo wa awamu ya tisa umefanywa kwa nchi nchi 39 za Afrika, ambapo Afrobarometer wamefanya mahojiano na watu 53,444 kwa lugha anayochagua mhojiwa na takwimu zimepimwa ili kuhakikisha sampuli zinawakilisha kitaifa.
Vigezo vilivyoangaliwa ni pamoja na uwepo wa polisi, utaalamu wa polisi: ufisadi na uhalifu wa polisi, ukatili wa polisi, uhusiano kati ya vipengele vya utendaji wa polisi, matokeo yanayohusiana na mwenendo wa Polisi.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa masuala ya haki za binadamu wamekuwa na maoni tofauti kwa utafiti huo, akiwamo Mkurugenzi wa Utetezi na Mageuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe akisema sio lazima vigezo hivyo viakisi hali halifi.
“Inawezekana wamefanya vizuri kutokana na vigezo na kutegemea ni wapi wametoa taarifa hizo, kwa sababu kumekuwa na matukio mengi ya uhalifu ambayo polisi wanatuhumiwa na mpaka wenyewe wamechukuliana hatua, kwa mfano lile tukio la mauaji ya mfanyabiashara wa madini kule Mtwara ambalo polisi wameshitakiwa,” amesema.
Ameendelea kusema kuwa kutokana na Tanzania kutosikika katika vyombo vya habari kimataifa, huenda hata sifa zake mbaya hazisikiki.
“Ni tofauti na Kenya ambayo inasikika zaidi kwenye vyombo vya kimataifa pengine ni kutokana na lugha ya Kiingereza,” amesema.
Hata hivyo, Massawe amelipongeza Jeshi la Polisi akishauri lifute rekodi mbaya zilizopo ili ziakisi sifa iliyotolewa na ripoti hiyo.
Maoni kama hayo yametolewa pia na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa aliyesema inawezekana vigezo vilivyopo visiakisi hali halisi ya wananchi.
“Inawezekana wanaangalia weledi katika taaluma, vifaa na kanuni, lakini kwa matukio yanayoendelea visiakisi hali ilivyo.
“Weledi a polisi unatakiwa uendane na changamoto zinazowakabili kwa mfano watu kukamatwa hovyo na wengine kufia vituo vya polisi,” amesema.
Amegusia pia suala la usimamizi wa demokrasia nchini akisema, “Tumesikia malalamiko ya usimamizi katika chaguzi hapo wanaonyeshaje weledi?”
Ameendelea kueleza: “Jeshi la polisi pia limehusishwa na matukio ya utekaji na watu kupotea, tungetarajia waonyeshe weledi katika matukio hayo ya watu waliopotea na mpaka sasa hawajapatikana.
“Kwenye ulinzi wa mali kweli, matukio ya uporaji yamepungua, lakini kwenye usalama wa raia bado wanapwaya.”
Maoni hayo yamekuja wakati hivi karibuni, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amelikosoa Jeshi la Polisi akisema limejiingiza katika siasa, alipokuwa akitoa tathmini ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam.
“Polisi ni chombo muhimu sana, ndicho kinacholinda wananchi na mali zao na kinatakiwa kifanye kazi na wananchi wote, katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi katika siasa za nchi, linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko, wananchi watagawanyika,” alionya Jaji Warioba.
Alipotafutwa kuzungumzia utafiti huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Mbali na kigezo cha weledi na kuheshimu haki za wananchi, Tanzania imeongoza katika kigenzo cha kuwa na imani na Jeshi la Polisi, ikiwa na asilimia 79, huku Uganda ikishika nafasi ya 27 na Kenya ya 30 na Nigeria ikiwa ya mwisho.
Katika kigezo cha kutohofia usalama au kutoogopa uhalifu, Seychelles imeongoza (asilimia 80) ikifuatiwa na Tanzania (asilimia 75), huku Burkina Faso ikishika nafasi ya mwisho.
Katika kigezo cha jinsi Serikali inavyopunguza uhalifu, Tanzania nafasi ya pili (asilimia 74) nyuma ya Benin (asilimia 77), huku Sudan ikiwa ya mwisho.
Hata hivyo, Tanzania haijafanya vizuri katika kipengele cha uwepo wa polisi mijini na vijijini, ikishika nafasi ya 39 ikiwa na asilimia 55 ya polisi mjini na asilimia 14 vijijini.
Nchi iliyoongoza katika kigezo hicho ni Morocco ikiwa na asilimia 94 ya polisi mijini na asilimia 31 vijijini.
Katika kigezo cha wananchi kuwasiliana na polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 34 ikiwa na asilimia 9 ya watu walioomba msaada na asilimia 24 ya watu waliowasiliana nao kwa namna nyingine.
Katika kigezo cha wepesi wa kupata msaada wa polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 11 ikiwa na asilimia 26 ya wepesi zaidi na asilimia 35 ya wepesi.
Katika kigezo cha ‘mara ngapi polisi husimamisha madereva bila sababu za msingi’, Tanzania imeshika nafasi ya 24 ikiwa na asilimia 37 ya mara kwa mara, asiliomia 22 ya mara kadhaa na asilimia 35 ya mara chache au hakuna.
Katika kigezo hicho, nchi ya Gabon imeongoza ikifuatiwa na Kenya.
Katika kigezo cha kutoa rushwa ili kupata msaada wa polisi au kujiepusha na matatizo, Tanzania iomeshika nafasi ya 26 ikiwa na asilimia 28 ya kutoa rushwa ili mtu asaidie na asilimia 28 ya kutoa rushwa ili mtu aachiliwe.
Katika kundi hilo, nchi ya Liberia inaongoza ikifuatiwa na Nigeria, Sierra Leone, Uganda na Congo- Brazzaville.
Katika taasisi zinazoongoza kwa utoaji wa rushwa, polisi imetajwa kuwa taasisi inayoongoza Afrika, ikifuatiwa na wabunge, maofisa wa kodi, watumishi wa umma, ofisi za marais, watendaji wa biashara, majaji na Mahakama, serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa jadi na viongozi wa dini.
Katika taasisi hizo, polisi wa Uganda wanaongoza wakifuatiwa na Nigeria, Sierra Leone, Gabon, Kenya, Liberia, Ghana, Afrika Kusini, Cameroon na Msumbiji, huku Tanzania ikishika nafasi ya 32.
Katika kigezo cha jinsi polisi wanavyohusishwa na uhalifu, Tanzania imeshika nafasi ya 38, ikiwa na asilimia 11 ya mara zote, asilimia 15 mara kadhaa, asilimia 13 walisema hawajui na asilimia 61 wakisema mara chache au hakuna kabisa.
Katika eneo hilo, Lesotho imeongoza, huku Kenya ikishika nafasi ya sita na Uganda nafasi ya 11.
Katika kigezo cha ukatili wa polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 32, ikiw ana asilimia 28 mara kadhaa, asilimia 26 mara kadhaa na asilimia 6 wakisema hawajui na asilimia 40 walisema mara chache au hakuna kabisa.
Katika eneo hilo, Gabon imeongoza, huku Kenya ikishika nafasio ya tatu na Uganda ya nne.
Katika kigezo cha matumizi ya nguvu kubaini wahalifu, Tanzania imeshika nafasi ya 22, ambapo asilimia 42 wamesema wakati wote, asilimia 24 wamesema mara kadhaa na asilimia tatu wamesema hawajui na asilimia 31 wamesema mara chache au hakuna kabisa.