JESHI la Polisi limetoa ufafanuzi baada ya aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Bernard Morrison, kulituhumu jeshi hilo kituo cha Mbweni kuwa linachukua rushwa, likimtaka staa huyo kufikia kituo hapo.
Juzi Morrison raia wa Ghana, alisambaza taarifa katika mitandao ya kijamii akikituhumu kituo cha Polisi Mbweni kuwa polisi wake wanachukua rushwa na wanafanya kazi kwa maslahi yao binafsi.
“Kuna watu wanafanya kazi kwenye kituo cha Mbweni hawasaidii watu wenye shida na wana maslahi yao binafsi, wanajichukulia sheria mkononi na kufanya wanavyotaka, ikiwa mimi ninayejua vizuri ninaweza kutapeliwa na kutoheshimiwa unafikiri wananchi wa kawaida wanaweza kufanyaje,” ilisema taarifa ya Morrison.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia taarifa iliyotolewa leo kupitia na Msemaji wake David Misime imesema kuwa Morrison anatakiwa kusema ukweli.
“Taarifa hiyo inasema kuwa, Bernard Morrison, Machi, 2024 alifungua kesi ya Wizi wa Kuaminiwa katika Kituo cha Polisi Mbweni, akiwa Ghana alimtumia Abdul Rakeeb Mgaya kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000) ili amkabidhi mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Boat anayeishi hapa nchini akitafuta timu itakayomsajili lakini hakufanya hivyo.
“Baada ya malalamiko hayo, aliyetuhumiwa alitafutwa na alipohojiwa alieleza ni kweli kuwa alitumiwa hizo fedha ili zisaidie kwenye gharama za kumsajili huyo mdogo wake lakini ilishindikana kwasababu hakuwa na kiwango cha kusajiliwa na timu aliyokuwa anahitaji,” iliendelea kusema taarifa hiyo.
“Hata hivyo, alimtaka Bernard Morrison ampe muda atamrejeshea fedha zake. Pia alielezwa kulingana na ushahidi hakuna kesi ya jinai. Hivyo walielewana na kwa vile wote ni raia wa Ghana walikubaliana kulipana.
“Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa, Juni 3,2024 iliripotiwa kesi ya kuharibu mali ambapo Morrison akiwa na mdogo wake na mtu mwingine walifika katika nyumba anayoishi Abdul Rakeeb na kuvunja geti kisha kuchukuwa kwa nguvu gari aina ya IST namba T239 DFM.
“Jeshi hilo liliendelea kumtafuta Morrison bila mafanikio lakini Abdul Rakeeb alifanikiwa kuliona gari hilo likiwa limeegeshwa sehemu na kulichukua na kulipeleka Kituo cha Polisi Mbweni.
“Hivyo Morrison anachotakiwa kufanya ni kuacha kujificha, kusema ukweli na kufika kituo cha Polisi kuonana na uongozi ili sheria ichukue mkondo wake,” ilimalizia taarifa hiyo.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga na Simba aliwahi kucheza soka la kulipwa pia Afrika Kusini, DR Congo kwa muda mrefu alikuwa nchini baada ya kuondoka FAR Rabat Morocco iliyokuwa ikinolewa na kocha Nasreddine Nabi kabla ya kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kuja kujiuguzia hapa Tanzania.