Serikali kuwapima afya ya akili waajiriwa wapya

Dodoma. Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma itafanya upekuzi wa afya ya akili (psychonomic test) kwa waajiriwa wapya, lengo likiwa ni kuhakikisha wanaoingia katika ajira mpya wanakuwa na utimamu wa akili.

Mbali na hilo, Serikali imekemea utovu wa nidhamu, vitendo vya rushwa, vitisho na ubabe kwa waajiri na watumishi wa umma.

Akifunga kikao kazi cha wakuu wa idara za raslimaliwatu na utawala leo Desemba 19, 2024, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema mwajiriwa mpya anaweza kuwa amekidhi vigezo vya kitaaluma na kielimu lakini kisaikolojia anakuwa na shida.

Amesema hilo linaweka umuhimu wa kuangalia afya ya akili kwa watumishi wapya wanaoajiriwa.

“Sekretarieti ya ajira wamekuja na utaratibu wa kuwafanyia upekuzi waajiriwa wapya wa ‘psychonomic test’ ili kujua mtu tunayempeleka huko kama kuna shida fulani, tufanyie marekebisho ili akiingia aweze kutusaidia kazi vizuri,”amesema. Ametoa mfano wa kijana mmoja ambaye ni mwajiriwa wa halmashauri ana miaka minne kazini, lakini hataki kupangiwa kazi yeyote bali muda wote ni kuwatisha waajiri na kuwa bosi wake wanayefanya naye kazi wanavutana mashati na wanakesi hadi polisi.

“Yaani ajira mpya halafu mbabe nikawaambia mnawezaje kuishi? Tumewapa mamlaka hamtaki kutumia nikasema sasa nitawasaidia namna ya kufanya kazi kwenye utumishi wa umma,” amesema.

Sangu amesema vijana wanaoingia kwenye utumishi wa umma wanadhani wanaenda kufanya utovu wa nidhamu na kujiingiza kwenye mikopo ambayo inachangia washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema vitendo hivyo vinawafanya kukosa utulivu wa kufanya kazi na kuwa lazima wawape elimu ya fedha kwa sababu wanaweza kuingia kazini na wakadhani wanafanya kazi bure kumbe mshahara wao wameutumia vibaya kwenye mikopo huko ya kausha damu.

 Aidha, Sangu amewaagiza maofisa utumishi kuwaangalia vijana ili kuwaepusha kuingia katika katika vitendo vinavyokiuka maadili.

“Kuna vijana wanaingia kwenye taasisi nyeti zinazohusika na maduhuli ya Serikali, anapokewa anaambiwa umefika hapa mwaka mmoja usipojenga utakuwa wa ajabu, kumbe anamkaribisha kuwa huku uliko kuna kula rushwa kweli, kumbe anakutana na mikono mibaya,” amesema.

Pia, amewataka maofisa utumishi hao wakafanye mipango kwenye bajeti zao kwa kuhakikisha wanatenga fedha za uhamisho.

Ametoa mfano katika halmashauri moja (bila kuitaja) yupo mtumishi anadai zaidi ya miaka 10 na deni lake ni zaidi ya Sh60 milioni na kisingizio kinachofanyika kuwa utumishi ndio wanachelewesha jambo ambalo si kweli.

Amewataka maofisa utumishi hao kuongeza umakini kwenye suala la uhamisho ambapo sasa kumeshamiri vitendo vya kugushi barua.

Katika hatua nyingine, Sangu amekemea tabia ya maofisa utumishi kuwafukuza kazi watumishi kwa kuwaonea na kuwa mwaka huu wa fedha mashauri zaidi ya 300 yamerudishwa yakaanze upya na yanaisababishia Serikali hasara.

Kuhusu rushwa ya ngono katika utumishi wa umma, Sangu amesema wapo waajiri wanachukua rushwa ndio watoe huduma kwa watumishi.

Bila kuitaja, amesema ipo halmashauri amepokea karatasi za madada zaidi ya 30 wanamtuhumu mtu mmoja kwa rushwa ya ngono na tayari ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ifanye uchunguzi.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Juma Mkomi amesema miezi minne iliyopita kuna mtumishi aliandika barua ofisini kwao akimtuhumu bosi wake kwa sababu ya uhamisho.

Amesema mtumishi huyo hakuwa amefukuzwa kazi, hajapoteza cheo na hajafanyiwa lolote baya, jambo ambalo linawafanya kujiuliza mtumishi huyo kama akili yake ipo timamu.

“Analiyoyafanya huku nyuma hayakubainika wakati anaajiriwa? Tumesisitiza na lazima mtumishi yeyote anayeajiriwa lazima vipimo vifanyike,” amesema.

Related Posts