Wadau waunga mkono masomo ya Kiswahili UDSM

Dar es Salaam.  Wakati wadau wa maendeleo wakiendelea kuunga mkono matumizi ya Kiswahili nchini, wanafunzi watatu wanaofanya Programu ya Shahada ya Uzamili ya Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamepewa ufadhili wa masomo hayo.

Hadi sasa, zaidi ya watu milioni 200 duniani wanazungumza Kiswahili ambacho kimataifa huadhimishwa Julai 7 ya kila mwaka baada ya siku hiyo kuanzishwa na Umoja wa Mataifa (Unesco).

Akikabidhi hundi kwa wanufaika hao jana Jumatano Desemba 18, 2024, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf, Hawa Bayumi amesema ufadhili huo, umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza Kiswahili ndani na nje ya nchi.

“Kiswahili ni moja ya tunu kubwa tuliyorithi kutoka kwa Muasisi wa Taifa letu la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo sisi kama wadau wa maendeleo, tumeona hatuna budi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuikuza lugha hii adhimu,” amesema.

Hawa amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na jukumu kubwa na muhimu katika kuandaa na kutekeleza Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika, ambazo Alaf inadhamini kwa kushirikiana na kampuni zake tanzu zilizopo nchini Kenya na Uganda kwa kuwaunganisha waandishi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

“Sisi kama moja wapo ya makampuni yaliyopata mafanikio makubwa tumeona umuhimu wa kukuza Kiswahili na ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuikuza lugha hii,” amesema.

Amewataja wanufaika wa ufadhili huo ni Asha Ally Mustapha, Asia Omary Saidi na Fredrick Venance ambao kila mmoja amepata Sh3,900,000.

Meneja huyo ametoa wito kwa wanufaika kutumia ufadhili walioupata kwa kuhakikisha wanafanya vyema kwenye masomo yao ili waweze kutoa mchango mkubwa katika kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili kupitia elimu watakayoipata.

Kwa upande wa Uongozi wa UDSM umeishukuru Alaf Limited kwa ufadhili huo, “kwa kawaida huwa kuna maombi mengi kutoka kwa wanafunzi kuhusiana na ufadhili huu lakini ni wanafunzi watatu pekee ndio wanaonufaika; kwa hili tunawashukuru sana ila tunaomba mfikirie jinsi ya kuongeza idadi ya wanufaika ili lugha ya Kiswahili iweze kukua zaidi,” amesema Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Profesa Rose Upor.

Related Posts