Wahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kulawiti watoto wa miaka minne

Tanga. Watu wanne wamehukumiwa kifungo cha maisha na wengine watatu wakihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kukutwa na makosa ya kubaka watoto wenye umri wa miaka minne na tisa mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Desemba 19, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema kesi hizo zilifikishwa Mahakamani kwa kipindi cha mwezi Novemba hadi Desemba, 2024 na watuhumiwa nne wamehukumiwa vifungo vya maisha na wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Amewataja waliohukumiwa adhabu hiyo kuwa ni Mwamini Ezekiel Mgeja (32), mkulima na mkazi wa Kilindi Asilia amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka 9 huku Jonas Alphan (38), mkulima na mkazi wa Gombero Kilindi amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 4. Mwingine ni Rajabu Juma (25), mkulima na mkazi wa Mafuleta Kilindi amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 17, Salimu Riziki na Athumani Salumu Jumaa wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na miaka 20 Jela kwa kosa la kumiliki silaha kinyume na sheria.

Aidha Richard Kiyango Shelukindo(45), Mkulima na mkazi wa Kwaludege Handeni amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kulawiti mtoto wa miaka 5 na Mansuri Omari, (19), Mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kwakibuyu Pangani amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 16.

Amesema katika tukio lingine wamefanikiwa kuwakamata watu watano kwa makosa ya wizi kwa njia ya mtandao ambao ni Said Amiri (21), Mkazi wa Kimara Dar es Salaam, Athumani Amiri (24), mkazi wa Mbezi mwisho Dar es Salaam, Brayan Matina Mayunga (26), Mkazi wa Mombasa Ukonga Dar es Salaam, Wakala, James John Nathaniel, (24), mkazi wa Kitunda Dar es Salaam na Peter Michael Babuya (20), Mkazi wa Arusha, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jijini Dar es Salaam na Masasi Mkoani Mtwara baada ya kujifanya mawakala wa kujitegemea (freelancers) wa kampuni za Tigo, Vodacom na Airtel na kuiba fedha kiasi cha Sh20,390,000 milioni kwa njia ya mtandao mali ya Abdul Hemed Shedafa Mfanyabiashara na Mkazi wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

Kamanda Mchunguzi amesema baada ya uchunguzi wa kitaalamu kufanyika imebainika kuwa walitumia mbinu za ulaghai, ikiwemo kutumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina mengine ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Aidha Desemba 10, 2024 katika msako uliofanyika huko katika kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni, Tarafa ya Mombo Wilaya ya Korogwe walikamatwa watuhumiwa wawili ambao ni Hashimu Juma Mohammed (46), Dereva, Mkazi wa Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam na Ramadhan Ismail Mbaruku (28), Kondakta, Mkazi wa Tegeta Dar es Salaam wakiwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.

Amesema kuwa watu hao walikuwa wakitumia gari yenye namba za usajili T. 689 EJJ aina ya Coaster Hino rangi mchanganyiko (Mult Colour) wakitokea mkoani Kilimanjaro kuelekea jijini Dar es Salaam.

Pia katika upekuzi wa gari hilo walikutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi bunda 962 sawa na kilo 411.05 dawa hizi zilikuwa zikisafirishwa kwa lengo la kuingizwa sokoni hivyo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

 Pia amesema, kwa kipindi cha kuanzia Novemba, 2024 hadi Desemba 18,2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga katika operesheni ya kuimarisha doria na misako limefanikiwa kukamata watuhumiwa 95 wakiwa na makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya uvunjaji, kujeruhi, wahamiaji haramu na kupatikana na dawa za kulevya.

Amesema katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba 2024 wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya mirungi Kg 529.49, bangi ni Kg 563, pombe moshi lita 179.5.

Hata hivyo wamefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 3 kutoka nchini Ethiopia, mali mbalimbali za wizi ikiwa ni pamoja na; televisheni kumi za aina mbalimbali, Pikipiki nane za aina mbalimbali, visimbuzi 11 vya kampuni ya Azam, laptop saba za aina mbalimbali.

Vitu vingine ni friji mbili aina ya Rock rangi nyeupe, simu 30 za smart phone na simu ndogo saba na madumu ya mafuta ya kula lita 864 yaliyoingizwa kwa njia ya magendo, pamoja na kuwakamata watuhumiwa wa matukio hayo.

Lakini kwa upande wa makosa ya usalama barabarani madereva 56 wameondolewa madaraja pamoja na kufungiwa leseni zao za udereva kwa muda kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani na wengine wamelipa faini mahakamani kwa makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Related Posts