Kibaha. Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini limeanzisha utaratibu wa kusajili wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi, lengo likiwa kuwafahamu na kuwawezesha kutoa huduma bora kwa jamii.
Kabla ya mchakato huo, wataalamu hao walikuwa wanatoa huduma bila kusajiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 19, 2024 Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini, Agnes Mtawa, amesema hatua hiyo inatokana na wataalamu hao kwa miaka mingi wamekuwa wakitoa huduma pasipo kusajiliwa.
“Kwa muda mrefu dawa za usingizi walikuwa wanatoa madaktari, kuanzia sasa kutakuwa na wataalamu maalumu waliosomea taaluma hiyo vyuoni na kufanya mtihani ili kupata leseni,” amesema.
Amesema kwa mara ya kwanza wataalamu hao wanatarajiwa kujumuishwa kwenye mtihani wa leseni kwa wauguzi 5,147 utakaofanyika kesho Desemba 20, 2024.
Mtihani huo utafanyika mikoa mbalimbali nchini ukilenga kutathmini ufanisi na weledi wa wauguzi na wataalamu wa dawa za usingizi.
“Baada ya kumaliza masomo, wauguzi wanapaswa kufanya mtihani wa kupata leseni ili waweze kutoa huduma, hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa wataalamu wa dawa za usingizi pia,” amesema.
Utaratubu wa kusajili wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama na ufanisi wa huduma za afya nchini.
Baraza linatarajia utekelezaji wa utaratibu huu utaleta mabadiliko chanya kwa mfumo wa afya, huku jamii ikifaidi na huduma bora.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Taaluma ya Uuguzi nchini, Happy Masenga amesema baraza halitavumilia udanganyifu katika mtihani.
“Tunawatahadharisha watahiniwa wote kuwa makini. Ikibainika udanganyifu, hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kumfuta mtahiniwa,” amesema.
Baadhi ya wananchi wametaka baraza lisiishie tu na usajili na mitihani, bali lihakikishe linasimamia utendaji wa wauguzi kazini ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii.
Joseph Kaduma, mkazi wa Kibaha mkoani Pwani amesema katika baadhi ya hospitali za umma kuna wauguzi wamesikika wakitoa kauli zinazokatisha tamaa kwa wagonjwa jambo linalopaswa kutatuliwa ili kuboresha huduma za afya.