YANGA iliuhama Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Azam FC na Tabora United na leo itacheza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa KMC Complex, ikiikaribisha Mashujaa kutoka Kigoma.
Yanga ilianza kutibuliwa rekodi ya kucheza mechi nane mfululizo ikishinda bila kuruhusu bao lolote kwa kuchapwa na Azam 1-0, kisha ikacharazwa 3-1 na Tabora united na siku chache ikatangaza kuuhama Uwanja wa Azam iliyokuwa ikitumia kwa michezo za nyumbani na kutua KMC unaotumia pia na wenyeji KMC na Simba.
Kuanzia saa 10:00 jioni itakuwa wenyeji wa Mashujaa ambayo itakuwa na kazi kubwa ya kufanya kudhihirisha ushujaa walionao kama inataka kuendeleza kilichofanywa na Azam na Tabora kwa mechi za nyumbani za vigogo hao wa Bara.
Huo ni mchezo wa 12 kwa Yanga katika ligi hiyo msimu huu na inapambana kutetea taji lake kwani hivi sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 27.
Mashujaa iliyopo nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 19, mchezo wa leo inahitaji kushinda ili kuweka hesabu sawa za mzunguko wa kwanza kwani ndiyo wa mwisho kwao kabla ya kuingia mzunguko wa pili ambao nao utakuwa na mechi 15.
Yanga na Mashujaa huu utakuwa ni mchezo wa tatu katika ligi kukutana huku mechi mbili za msimu uliopita Yanga ikishinda zote. Ikianza na ushindi wa 2-1 nyumbani kupitia mabao ya Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya huku Emmanuel Mtumbuka akiifungia Mashujaa, kisha ugenini Yanga ikashinda 1-0 kwa bao la Joseph Guede ambaye kwa sasa hayupo kikosini hapo.
Mbali na rekodi hiyo nzuri kwa Yanga, lakini timu hiyo haikupata ushindi mechi mbili kati ya tano za mwisho katika ligi ikifungwa 3-1 dhidi ya Tabora United na 1-0 dhidi ya Azam, huku ikizifunga Namungo 2-0, Singida Black Stars (1-0) na Coastal Union (1-0).
Yanga iliyotoka kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika, inarejea kwenye ligi ikiwa bila ya huduma za wachezaji wake kadhaa ambao ni majeruhi akiwemo Djigui Diarra, Clatous Chama, Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda.
Kukosekana kwa wachezaji hao ambao wamekuwa muhimu zaidi kikosi cha kwanza, kutaifanya Yanga kuwa na mabadiliko makubwa na kutoa fursa kwa wengine kuchukua nafasi zao.
Hata hivyo, Kocha wa kikosi hicho, Sead Ramovic amesema atawatumia nyota waliopo tayari kwa ajili ya kufanya vizuri.
Katika kikosi cha Yanga kilichofunga mabao 16 na kuruhusu manne kwenye ligi msimu huu, nguvu yao kubwa ya mashambulizi inaonekana kubebwa na viungo kwani ndio wamefunga mabao mengi kikosini hapo hadi sasa.
Viungo hao wamefunga mabao saba kupitia Maxi Nzengeli (3), Pacome Zouzoua (3), Clatous Chama (1) na Aziz Ki (1) huku pia wakitoa asisti nyingi (11).
Kwa upande wa Mashujaa, ni timu ambayo haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo za mwisho ikiambulia sare zote huku mbili kati ya hizo ikishindwa kufunga bao lolote.
Uwepo wa David Ulomi na Ismail Mgunda, kunaifanya Mashujaa kuwa si timu ya kuibeza katika kucheka na nyavu kwani nyota hao ndiyo wanawabeba zaidi, hadi sasa kila mmoja amefunga mabao mawili huku Mgunda akiwa pia na asisti tatu ikimfanya jumla kuhusika kwenye mabao manne peke yake.
Ukiachana na nyota hao wa safu ya ushambuliaji, kwenye ulinzi wapo imara kupitia kipa wao, Patrick Munthary ambaye amekusanya clean sheet nane katika mechi 14 kitu ambacho kinaonyesha wazi wachezaji wa Yanga wanapaswa kufanya kazi ya ziada kumfunga kwani si kipa mwepesi kufungika.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema: “Tumeshamaliza mechi tatu za Ligi ya Mabingwa na sasa akili yetu inaelekea kwenye Ligi Kuu. Tunataka kupambana kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, nimezungumza na wachezaji umuhimu wa pointi tatu za mchezo wa kesho (leo) na wako tayari kwa hilo.
“Tunapewa nafasi ya kufanya vizuri lakini hilo halitufanyi tuwadharau wapinzani wetu, tunajiandaa vizuri kuhakikisha wachezaji wanakwenda kufanyia kazi tunayowaelekeza mazoezini. Tunaamini utakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani.”
Mohamed Abdallah ‘Bares’ ambaye ni Kocha wa Mashujaa, alisema: “Tuna wachezaji kama wawili majeruhi lakini wanaendelea vizuri, waliopo wapo tayari kwa mchezo huu na tumeshawapa majukumu ya kufanya katika mchezo wa kesho (leo) kilichobaki ni kwao kwenda kutekeleza tulichowafundisha.
“Tumecheza mechi nne tumesare tatu, ni matokeo ambayo sio rafiki na sio mabaya sana, tutaingia kwa kuwaheshimu lakini tutatumia nafasi tutakazozipata kwa sababu timu kubwa kama hizi unapocheza nazo ukipata nafasi inabidi uzitumie.
“Yanga bado wana kikosi bora, tunatakiwa tufanye kazi ya ziada kuhakikisha tunadhibiti maeneo ambayo kwao ni bora zaidi.”