GARI limewaka. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Prince Dube kufunga hat trick katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa ni siku chache tangu aipate ‘code’ ya kutupia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakati akiipa Yanga sare ya bao 1-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Dube aliyesajiliwa msimu huu kutoka Azam, alikuwa hajafunga bao lolote kabla ya mechi hizo mbili, lakini leo alidhihirisha mambo yamemnyookea baada ya kufungua akaunti ya mabao katika ligi wakati Yanga ikiizamisha Mashujaa kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
Hiyo ilikuwa ni hat trick ya kwanza katika Ligi Kuu kwa msimu huu baada ya kupigwa mechi 111 hadi sasa, lakini ya pili kwa Mzimbabwe huyo tangu alipotua nchini akijiunga na Azam akitokea Highlanders ya Zimbabwe na kuitumikia klabu hiyo kwa misimu minne kabla ya kuhamia Yanga msimu huu.
Hat trick ya kwanza ya Dube aliifunga Juni 6, 2023 wakati Azam ikiizamisha Polisi Tanzania kwa mabao 5-0 na leo akiwa na moto mkali alitupia mabao mawili kipindi cha kwanza na kuongeza jingine cha pili na kumaliza ukame aliokuwa nao Ligi Kuu tangu msimu ulipoanza rasmi Agosti mwaka huu, akipiga mabao mawili ya vichwa na moja la mguu wa kulia.
Dube alianza kufunga bao la kwanza dakika nane akimalizia pasi ya Pacome Zouzoua aliyegongeana na straika huyo, kabla ya dakika ya 22 kuongeza chuma ya pili kwa kichwa akimalizia mpira wa Mzize aliyechachafyiana na mabeki wa Mashujaa.
Bao la tatu la kufungia hesabu alitupia tena kwa kichwa akimalizika krosi tamu kutoka kwa Kibwana Shomari aliyeanzishwa katika mchezo wa leo kama beki wa kushoto kabla ya kutolewa kipindi hicho kumpisha Chadrack Boka aliyeanzia benchi pamoja na Nickson Kibabage.
Abubakar Khomeiny aliyeanzishwa langoni kutokana na kipa namba moja, Diarra Djigui kuwa majeruhi, aliruhusu mabao mawili na kutibua rekodi yake ya kucheza mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao, zikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya CAF.
Aliyeanza kumtia doa Khomeiny ni David Ulomi aliyefumua shuti kali la mbali sekunde chache kabla ya mapumziko na kufanya mapumziko Yanga kuwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili dakika 10 tu tangu Yanga ifunge bao la tatu, mtokea benchi, Idriss Stambuli alimtungua tena Khomeiny kwa shuti jingine la mbali na kuwafanya mashabiki waliojaza Uwanja wa KMC kubakiwa wameduwaa, kwani waliamini angeudaka mpira huo, lakini ukamchurupuka na kuingia wavuni.
Tofauti na Yanga iliyocheza mechi nne zilizopita, zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa na moja ya Ligi Kuu dhidi ya Namungo ikiwa chini ya kocha Sead Ramovic, timu ikionekana kucheza kinyonge na kupoteza hovyo mipira, kwa leo timu hiyo ilionekana wachezaji wamechangamka na kugeana kiustadi mwanzo mwisho.
Licha ya kupoteza mechi hiyo, lakini Mashujaa katika vipindi vyote ilionekana kucheza kwa nidhamu na hasa kipindi cha pili walitumia nafasi chache walizotengeneza kulitingisha lango la Yanga ambalo liliwatia presha mashabiki kutokana na kushindwa kumuamini Khomeiny ambaye alicheza kama mwenye mchecheto vile.
Ulomi, Mapinduzi Balama, Ismail Mgunda na Shaaban Mgandila walipambana kuitafuta mabao timu hiyo katika kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata moja kabla ya kipindi cha pili kuongeza jingine na dakika 20 za mwisho za pambano hilo baada ya timu zote kufanya mabadiliko mchezo ulikuwa fifte fifte.
Matokeo hayo yameifanya Mashujaa kusalia nafasi ya saba na pointi 19 baada ya mechi 15 za duru la kwanza, ikipoteza jumla ya michezo minne, ikishinda minne na kutoka sare saba, huku ushindi huo ni 10 kwa Yanga katika mechi 12, ikiwa imepoteza mbili na haijatoka sare.
Pia huo ni ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu kwa Ramovic, baada ya awali kushinda ugenini dhidi ya Namungo iliyoifunga 2-0 wiki tatu zilizopita.