Dar es Salaam. Ajali za barabarani zimeendelea kuwa chanzo cha vifo vya Watanzania, hali inayozua maswali iwapo hatua zinazochukuliwa na mamlaka mbalimbali nchini kama zinakidhi katika kukabiliana na changamoto hii.
Katika ajali hizi, mwendo kasi umebainika kuwa moja ya sababu, zingine zikitajwa kuwa ni matumizi ya vilevi, miundombinu zikiwamo barabara zenye mashimo, zisizo na alama za barabarani.
Chanzo kingine ni kutozingatiwa sheria za usalama barabarani, matatizo ya kiufundi na uzembe wa madereva.
Kiwango kidogo cha adhabu ya kosa la kuvunja sheria ya usalama barabarani na madereva kukosa mapumziko, ni baadhi ya sababu zingine zinazotajwa na wadau wa usalama barabarani kama kichocheo cha ajali.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2024 jumla ya watu 453 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani.
Idadi hiyo ya vifo imepungua kutoka 477 vilivyotokea katika kipindi kama hicho mwaka 2023, huku waliojeruhiwa wakiwa 835, ikilinganishwa na majeruhi 782 wa mwaka 2023.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi anasema hatua mbalimbali zinafanyika kudhibiti ajali hasa kwenye maeneo korofi, akieleza kwa sehemu kubwa ajali hutokea mchana.
Miongoni mwa ajali zilizopoteza nguvu kazi ya Taifa ni iliyotokea Machi, 2024 mkoani Dodoma ikihusisha basi lililogongana na lori. Katika ajali hiyo watu 17 walipoteza maisha na wengine 30 walijeruhiwa.
Ajali hiyo ilifuatiwa na nyingine Mei, jijini Dar es Salaam iliyosababisha watu tisa kufariki dunia, huku 15 wakijeruhiwa.
Ajali hiyo ilihusisha daladala lililokuwa likielekea Mbagala lililogongana na lori katika Barabara ya Kilwa.
Juni, 2024 watu 12 walifariki dunia na wengine 20 wakijeruhiwa kutokana na ajali ya basi la abiria katika barabara ya Morogoro-Dar es Salaam.
Matatizo ya kiufundi kwenye gari ndiyo yalitajwa kuwa sababu ya ajali hiyo.
Agosti 2024, mkoani Singida ajali ya basi ilikatisha uhai wa watu 14 na kujeruhi wengine 18. Katika tukio hilo, inaelezwa dereva alikuwa akijaribu kulipita gari lingine hivyo kupoteza mwelekeo.
Novemba 7, 2024 watu 14 walifariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika tukio la ajali iliyohusisha gari ndogo ya abiria iliyogonga lori kwa nyuma wilayani Nzega, mkoani Tabora.
Watu 12 akiwemo mmoja wa wamiliki wa mabasi ya kampuni ya AN Coach, Amduni Nassor walifariki dunia katika ajali ya basi lililokuwa likiendeshwa na mmiliki huyo.
Ajali hiyo ilitokea Septemba 6, alfajiri mkoani Mbeya, sababu ikitajwa ni mwendokasi. Watu 36 walijeruhiwa.
Septemba 4, 2024 katika Kata ya Chimala mkoani Mbeya, watu tisa walifariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali ya basi la kampuni ya Shari Line.
Tukio lingine la ajali ni la Desemba 6, 2024 lililojeruhi wabunge 16, baada ya basi la kampuni ya Shabiby walilokuwa wamepanda kugongana na lori, Kongwa mkoani Dodoma.
Septemba 16, 2024 watu 12 walifariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa katika ajali ya Fuso walilopanda kwenda sokoni, mkoani Mbeya.
Chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa propela kulikosababisha gari lipoteze mwelekeo.
Desemba 3, watu saba walifariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu, wilayani Karagwe mkoani Kagera. Ajali hiyo ilitokana na magari hayo kugongana.
Desemba 18, 2024 watu 15 walipoteza maisha na wengine saba kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Mikese mkoani Morogoro. Katika ajali hiyo, gari aina ya Toyota Coaster iligongana na lori.
Kiwango kidogo cha adhabu ya kosa la kuvunja sheria ya usalama barabarani na madereva kukosa mapumziko, ni baadhi ya mambo yanayotajwa kuchochea ajali, kama inavyoelezwa na Irene Msellem, mmoja wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA).
“Madereva wanavunja sheria, hata wakikamatwa faini ni Sh30,000 na bado wanapewa muda wa siku saba kuilipa, wakati matokeo ya kosa hayalingani na kiwango cha adhabu,” anasema.
Sababu nyingine kwa mujibu wa Irene ni kupungua kwa utaratibu wa udhibiti mwendokasi kwa kutumia tochi, badala yake imebaki njia ya kutumia mfumo wa VTS.
“Sina uhakika sana kwa mtandao wa barabara tulionao na tochi tulizonazo kama zinakidhi,” anasema.
Amependekeza kuongezwa maeneo ya kupimia vilevi kwa madereva ili kupunguza wale wanaoendesha wakiwa wamelewa, pia upimaji usiishie kwenye pombe pekee akisema wapo waraibu wa ugoro.
Anapendekeza wawepo madereva wawili kwenye mabasi yanayosafiri zaidi ya saa nane ili kupunguza ajali zinazotokana na uchovu wa dereva.
“Uwepo wa wakaguzi wa kutosha kukagua vyombo vya moto nalo linaweza kutusaidia kupunguza ajali. Kikubwa zaidi ni usimamizi wa sheria ya usalama barabarani, tuache mazoea kati ya askari na madereva, tusiwaonee aibu madereva wanaovunja sheria,” anasema.
Kwa mujibu wa Irene, askari wa usalama barabarani wanapaswa waachwe wafanye kazi kwa uhuru, kusiwepo utaratibu wa dereva anakamatwa anapiga simu kwa mkubwa kisha anaachiwa.
“Hii tabia dereva anakamatwa halafu anapiga simu kwa wakubwa huko juu halafu maelekezo yanatoka kwa askari kuwa amuachie inawavunja moyo hawa askari wanaosimamia usalama barabarani,” anasema.
Anaeleza juhudi za kudhibiti madereva zisiishie kwa wale wa mabasi pekee ni vema wanaoendesha malori pia wasimamiwe kwa sababu makosa yao yanaathiri usalama wa wengine.
“Ufike wakati tuwekeze nguvu na upande wa madereva wa malori. Kwa kuanzia, tugawanye madaraja ya leseni daraja E ili tupate madereva wenye weledi kulingana na aina ya gari analoendesha.
“Leo hii hakuna daraja la leseni linaloweza kumtofautisha dereva anayeendesha Canter na anayeendesha Semi Trailer. Tuvunjevunje leseni ya daraja E angalau tupate E, E1, E2 na E3 kama ilivyo kwenye daraja C,” anasema.
Ili kupunguza matukio ya ajali hasa yanayosababishwa na hali ya eneo husika, Mkuu wa Trafiki nchini, Ramadhan Ng’anzi anasema wameamua kuanzisha utaratibu wa kuwavusha watu kwa awamu.
Maeneo unakotumika utaratibu huo anaeleza ni Mlima Nyoka na kwenye mikoa ya Mbeya na Songwe.
“Malori na magari ya kawaida yanapita kwa zamu, tumeona imesaidia, nichukue nafasi hii kuwataka madereva wanaosafiri masafa marefu kuhakikisha magari yao madhubuti yanayoweza kuhimili milima na jiografia ya aina tofauti,” anasema.
Mbali ya vifo, madhara mengine yanayosababishwa na ajali anasema ni uharibifu wa miundombinu, zikiwemo kingo za madaraja na taa za barabarani.
Ingawa kuna matukio ya ajali, Ng’anzi anasema kumekuwa na mwenendo mzuri wa mabasi yanayofanya safari usiku kuhusu ajali.
“Ajali mlizozisikia zote zimetokea mchana, kwa mabasi ya usiku hakuna ajali yoyote iliyotokea na kuleta madhara kwa binadamu, lakini zile ndogo ndogo ikiwemo gari kupoteza njia au kupata break down. Kwa mabasi ya mchana yapo yanayopata ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva au kutaka kulipita gari jingine pasipo kuchukua tahadhari,” anasema.
Kwa sababu ajali zinasababisha vifo na majeruhi, madhara ya kiuchumi kutokana na gharama za matibabu, ukarabati wa magari na upotevu wa nguvu kazi, pia msongo wa mawazo kwa waathirika, ni muhimu kuchukuliwa hatua madhubuti kuzipunguza au kuzimaliza kabisa.
Kampeni za uhamasishaji kuhusu usalama barabarani zishirikishe taasisi zingine za umma, za kiraia na sekta binafsi ili kukomesha ajali.
Ni muhimu jitihada za pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo zichukuliwe kupunguza ajali. Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake.