DC Lijualikali ahusishwa na vurugu za uchaguzi Nkasi, mwenyewe akana

Rukwa. Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali amesema taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa amehusika kwenye vurugu zilizotokana na marudio ya uchaguzi wa serikali za mitaa si za kweli, akiwataka wanaozisambaza kuwasilisha ushahidi.

Taarifa hizo zimedai kuwa baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika Kijiji cha Ntalamila wilayani humo mkoani Rukwa kushindwa kufanyika Novemba 27 ulisogezwa hadi Novemba 30, lakini nako washindi halali hawakutangazwa.

Inaelezwa kuwa baada ya uchaguzi huo, katika vitongoji 10 Chadema ilipata vitano na CCM vitano, huku upande wa mwenyekiti Chadema ilipata kura 966 na mgombea wa CCM alipata 634.

Hata hivyo, taarifa hiyo imedai kuwa hakuna aliyetangazwa mshindi kwa nafasi zote, badala yake DC Lijualikali aliagiza wasimamizi kubeba maboksi ya kura kwenda Namanyere yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa jana Desemba 19, Mkuu huyo wa Wilaya akiambatana na polisi, alifika kijijini hapo kumtangaza mshindi, lakini wananchi hawakukubali na mkutano ukavunjika.

Baadaye, inaeleza polisi walivamia makazi ya wakazi ya wafuasi wa Chadema kwa kuvunja nyumba usiku wa manane kuwakamata.

Inaelezwa kuwa katika operesheni hiyo, watu takribani 50 wamekamatwa wakiwamo wanawake 16, huku ikiwa haruhusiwi mtu yeyote kujua hali zao.

Lakini akizungumza na Mwananchi leo Desemba 20, Lijualikali amekanusha kuhusika katika vurugu hizo, akieleza kuwa hajashiriki uchaguzi wala kuelekeza kukamatwa kwa mtu yeyote.

Amesema awali wafuasi wa Chadema waligomea uchaguzi kutofanyika shule ya Ntalamila, wakishinikiza kupigia kura katika maeneo ya vitongojini walipojiandikishia, licha ya ushauri aliotoa kutokana na hali ya hewa iliyokuwapo ya mvua.

“Wakasababisha uchaguzi kutofanyika Novemba 27 badala yake ikawa Novemba 30. Baada ya muda kuisha, mwenyekiti wa CCM aliyeshinda wanampa vitisho ama vya kumuua, kumpiga au kuhamasisha wananchi kutompa ushirikiano na kuharibu mali za ofisi.

“Baada ya vurugu hizo nilikwenda kwenye mkutano jana kuwasikiliza, nilichoambulia ni kupigwa mawe na kushambuliwa hadi video na picha ninazo, vyombo vinavyohusika na ulinzi vikatimiza majukumu yake, lakini sijatoa maelekezo yoyote kwamba mtu akamatwe au apigwe.

Amesema baadhi ya wafuasi wa Chadema walimshambulia na kuvamia nyumba za watu wa CCM, kuvunja na kuharibu mali na kuhatarisha amani.

“Kwa maana hiyo ieleweke kwamba sikushiriki kutangaza matokeo, hayo ni maneno ya mtu ameamua kujiandikia na kama wana ushahidi waulete,” amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Kuhusu watu walioshikiliwa, Lijualikali amesema bado hajapewa taarifa na vyombo vinavyohusika na vinaedelea na kazi yake na baada ya kukamilisha watampa ripoti.

“Wito wangu, hatutaruhusu wala kukubali kwa namna yoyote mtu kuharibu, kutishia au kuhatarisha amani katika wilaya hii, atakayebainika atachukuliwa hatua, nazipongeza juhudi za Jeshi la Polisi kwa kazi waliyoifanya,” amesema.

Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Rukwa, Alfred Sotoka amesema msimamo wao ni mamlaka zinazohusika na uchaguzi kikanuni, zijitokeze kumtangaza mshindi aliyeshinda kihalali.

“Huyu mgombea wetu, Charles Kailya ndiye alikuwa mwenyekiti pekee nchi nzima katika uchunguzi wa 2019, mwaka huu alitetea na ameshinda tena, sasa mkuu wa wilaya ndiye analeta vurugu, vinginevyo hatutamtambua aliyemtangaza na huu ni msimamo wa wananchi na Chadema,” amesema Sotoka.

Mwenyekiti wa Baraza za Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani humo, Benjamin Mizengo, amesema baada ya uchunguzi walioufanya walibaini kuwa mgombea wao alishinda, lakini hakutangazwa.

“Tangu uchaguzi uliofanyika Novemba 30, watu walikaa bila kujua mshindi ni nani, ndiyo jana Desemba 19, Lijualikali akaenda kumtangaza mgombea wa CCM na vurugu zikaanza.

“Kutokana na fujo hizo kuwa kubwa, polisi walitoka Sumbawanga kuongeza nguvu, hivyo kazi ikawa ni kuvamia nyumba za watu kubeba raia ambao ni 22. Wanawake saba ambao wameachiwa muda huu (leo, Desemba 20, jioni) na wanaume 15 tunapambana waachiwe hapa Polisi Sumbawanga,” amesema Mizengo.

Related Posts