Hakuna kifo ajali ya basi la Kisire, dereva atiwa mbaroni

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia dereva wa basi la kampuni ya usafirishaji ya Kisire, Adam Charles (30) kwa tuhuma za kufanya uzembe uliosababisha ajali ya basi hilo na watu 44 waliokuwemo kunusurika, baadhi yao wakijeruhiwa.

Ajali hiyo ilitokea saa 7 mchana Desemba 19, 2024 katika Wilaya ya Magu wakati basi hilo likitoka Mwanza kwenda Musoma na Tarime, wakati dereva huyo akijaribu kulipita gari la kampuni ya George Town bila kuchukua tahadhari.

Akizungumzia ajali hiyo leo Desemba 20, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema dereva huyo yupo chini ya ulinzi kwa sasa na uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani.

“Dereva huyu ambaye ameumia kidogo kwenye kidole cha mkono wa kulia, kwa sasa yupo chini ya ulinzi kwa ajili ya mahojiano na pindi uchunguzi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yake kwa kitendo cha kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali iliyoleta majeraha kwa watu ambao hawana hatia,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akitoa taarifa ya kumshikiria dereva wa basi la Kampuni ya Kisire, Adam Charles (kushoto) leo Ijumaa Desemba 20, 2024. Picha na Anania Kajuni

Kamanda Mutafungwa amesema hali za majeruhi 44 waliopelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu wanaendelea vizuri, baadhi yao wakiendelea kuruhusiwa kurudi nyumbani lakini wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa uangalizi zaidi.

“Abiria walipata mshtuko na wengine kupata majeraha hasa kwenye mikono. Watu 44 wamefikishwa Hospitali ya Wilaya ya Magu na kutibiwa na tumepokea taarifa kwamba wengine wameanza kuruhusiwa,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Akisimulia namna ajali hiyo ilivyotokea, mmoja ya waathirika katika ajali hiyo, Monasi Kesi amesema baada ya gari kumshinda dereva huyo wakati akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake, ndipo ilipopata ajali wakati akijaribu kurudi upande wake.

“Nilikuwa nimekaa siti ya nyuma wakati ajali inatokea, tulikuwa tunapiga stori, mimi na wenzangu tukashangaa dereva ameingia upande wa kushoto gari likaanza kuyumba wakati anachukua hatua za kurudi barabarani wakati huo basi moja lipo mbele, ndipo likapita kwenye majani na kupata ajali,” amesema Kesi.

Naye Mkazi wa Bukombe aliyekuwa anaendaq Nyamongo kwa gari tofauti, Riguis Nyabwisho amesema baada ya ajali hiyo kutokea walisimama na kuanza kufanya uokozi.

“Mimi nilikuwa nasafiri na gari la George Town, sasa wakati tupo kwenye gari kuna gari lilijaribu kulipita gari letu nililokuwa nimepanda, bahati mbaya derava alishindwa kulidhibiti na kupata ajali. Baada ya hapo tulizima gari na kuanza kuokoa majeruhi, japokuwa siwezi kusema ni wangapi lakini watu wameumia,” amesema Nyabwisho.

Related Posts