Kagera Sugar yavizia watatu Simba, Yanga

UONGOZI wa Kagera Sugar umeziandikia barua Simba na Yanga kuwaomba wachezaji wao Ladack Chasambi, Salehe Karabaka na Denis Nkane kwa mkopo.

Chasambi na Karabaka wote wanacheza Simba huku Nkane akikipiga Yanga na hana namba ya kudumi kikosi cha kwanza.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kagera Sugar kimeliambia Mwanaspoti kuwa tayari wamefanya taratibu za kuziandikia barua timu hizo, kwaajili ya maombi ya wachezaji hao.

“Kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu zao haina maana kwamba hawana uwezo wa kucheza vizuri na kuja kutusaidia kuinusuru Kagera Sugar ambayo haijawa na matokeo mazuri mzunguko wa kwanza,”

“Licha ya kutokuwa na nafasi tunaimani kubwa na vipaji vyao ni wachezaji ambao wana uwezo mzuri kwenye nafasi wanazocheza, watakuja kuongeza kitu ndani ya timu hasa mzunguko wa pili ambao tunatarajia ushindani mkubwa.”

Mtoa taarifa huyo aliongeza kuwa hawatakuwa na cha kupoteza mzunguko wa pili kutokana na kupoteza mechi za mzunguko wa kwanza.

Kalabaka ni miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa na Simba kutolewa kwa mkopo dirisha hili la usajili ili kutafuta changamoto nyingine nje ya Simba, na tayari KMC pia wamemuomba kwa mkopo.

Kagera Sugar ambayo inanolewa na Melis Medo ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 14 imeshinda mbili, sare tano na vipifo saba ikikusanya pointi 11.

Related Posts