Maamuzi ya Fadlu yanashangaza Simba

KAMA kuna mchezaji ndani ya Simba anaamini ana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza basi pole yake, kwani kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu David amesema ataendelea kufanya mzunguko kwa wachezaji ili kutunza nishati ya mastaa kwa wingi wa mechi zilizopo mbele yao, huku akiwataka Awesu Awesu na Charles Jean Ahoua.

Fadlu ametoa msimamo huo juzi mara baada ya pambano la Ligi Kuu Bara walioshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya  KenGold na kusema ataendelea kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kutokana na idadi kubwa ya mechi zilizo na kubwa ni kutunza nishati ya wachezaji wake ili kukabiliana na changamoto ya michezo hiyo.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, kocha Fadlu alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi cha kwanza akiwamo kuwaweka nje wachezaji muhimu waliocheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien akiwamo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Jean Ahoua, Shomari Kapombe na Debora Mavambo, kisha kuwatumia Ladack Chasambi, Valentin Nouma, Kelvin Kijili, na Mzamiru Yassin.

Kikosi hicho chenye mseto kilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili yote yakifungwa na Leonel Ateba kabla ya kipindi cha pili kuwaingiza baadhi ya nyota waliocheza dhidi ya Sfaxien, huku Kapombe akikosekana hata benchi.

“Tumekuwa na mechi nyingi mfululizo, wachezaji nao ni binadamu hivyo ni muhimu kutunza nishati yao kwa kufanya mabadiliko kwa kutoa nafasi pia kwa wachezaji wengine. Hivyo wachezaji wajue hakuna mwenye uhakika wa namba, kila mmoja atatumika kutokana na umuhimu wa mchezo,” alisema Fadlu.

Kocha huyo alimtaja Awesu Awesu aliyemtumia katika kikosi cha kwanza katika mechi mbili zilizopita aliyesababisha penalti iliyozaa bao la kwanza kwa kusema; “Nimekuwa nikivutiwa na uwezo alionao. Ni mchezaji mzuri, lakini tunatakiwa kutambua kuwa kikosi kina wachezaji wengi na kila mmoja ana nafasi sawa ya kucheza. Hivyo, nitaendelea kumtumia kulingana na mpango wa mchezo husika.”

Licha ya kumtaja Awesu kama mchezaji mwenye uwezo, zipo taarifa Davids anahitaji huduma ya kiungo mchezeshaji mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo ya mechi atakayeshirikiana naye sambamba na Jean Ahoua.

Simba imekuwa ikiwategemea Awesu na Charles Jean Ahoua kwenye eneo la kiungo mchezeshaji, huku wakiwa na jukumu la kuunganisha mashambulizi na kumsaidia mshambuliaji wa mwisho.

Hata hivyo, Fadlu anatarajia kuongeza nguvu zaidi katika eneo hili ili timu iwe na chaguo zaidi la kiufundi.

Kwa upande mwingine, Simba tayari imeshacheza michezo miwili ya Desemba, ambapo waliibuka na ushindi dhidi ya CS Sfaxien kwa 2-1 na KenGold kwa 2-0. Katika mechi tatu zilizo mbele yao, Simba inahitaji pointi tisa katika michezo mitatu ya kufungia duru la kwanza ukiwamo wa kesho mjini Bukoba dhidi ya Kagera Sugar.

Mechi nyingine mbili za mwisho ni dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa jijini Dar es Salaam na ule wa Singida Black Stars utakaochezwa ugenini na hesabu za Faldu ni kuvuna alama zote bila kujali inacheza wapi kwani katika mechi 12 ilizocheza sasa imepoteza moja nyumbani mbele ya Yanga na kutoka droo na Coastal Union, huku ikishinda 10 na kujikusanyia pointi 31, ikiwa nyuma ya Azam yenye 33 ikimaliza mechi zote za duru la kwanza.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imethibitisha kuwa kila kitu kuhusu usajili wa Ellie Mpanzu ikisema imethibitisha rasmi sasa yupo tayari kuanza kuitumikia timu hiyo katika mchezo wa kesho dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema Mpanzu aliyejiunga na timu hiyo kutoka AS Vita ya DR Congo ana asilimia kubwa ya kucheza dhidi ya Kagera Sugar.

Ahmed alibainisha hayo akiweka wazi kwamba kila kitu kuhusu usajili wake kwa maana ya vibali kimekamilika, kilichobaki ni benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu David kuamua kumtumia kwani kiafya yupo vizuri.

“Ellie Mpanzu ana asilimia 99.99, Desemba 21 akawa sehemu ya kikosi, mambo yake yote yameshakamilika na sasa yupo tayari kuitumikia Simba,” alisema Ahmed na katika kuonyesha hawatanii katika msafara wa kikosi cha Simba kilichoondoka jana kwenda Kagera kwa mchezo huo, Mpanzu alikuwa sehemu ya wachezaji wa timu hiyo jambo linalotoa majibu ya moja kwa moja yupo kwenye mipango ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Related Posts