Majaliwa kukabidhi nyumba 109 za kisasa kwa waathirika wa tope Hanang’

Hanang’. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kukabidhi nyumba 109 za kisasa kwa waathirika wa maporomoko ya matope, zilizojengwa kwenye Kitongoji cha Waret, Gidagamowd mkoani Manyara.

Nyumba hizo zimejengwa kutokana na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan alipofika mji mdogo wa Katesh kutoa pole kutokana na maporomoko ya matope yaliyosababisha maafa kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amethibitisha Waziri Mkuu Majaliwa atakabidhi nyumba hizo leo Desemba 20, 2024.

Amesema pia Waziri Mkuu wakati wa kukabidhi nyumba hizo atazungumza na watu watakaokabidhiwa nyumba hizo na kupanda miti kwenye eneo hilo.

“Watu wote wanakaribishwa kuja kwa wingi kumpokea mgeni wetu Waziri Mkuu Majaliwa ambaye atakuwepo mkoani kwetu kwa tukio hilo maridhawa,” amesema Sendiga.

Mmoja kati ya waliothirika na tukio hilo anayetarajiwa kupatiwa nyumba, Peter Konki ameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya kutoa nyumba kwao.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan alipofika Katesh kutupa pole aliahidi kutupatia nyumba na leo ametimiza ahadi hiyo, tunasema asante sana,” amesema Konki.

Katika tukio hilo lililotokea Desemba 3, mwaka jana watu 89 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa huku wakipoteza mali zao ikiwemo mifugo, mazao na nyumba kubomoka.

Related Posts