Mwinyi azindua ujenzi ‘flyover’ ya kwanza Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezindua ujenzi wa daraja la juu (flyover) la kwanza visiwani hapa, akisema ni sehemu ya mipango ya Serikali kuijenga Zanzibar kila upande.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Desemba 20, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi wa daraja hilo eneo la Mwanakwerekwe ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi, akisema “Tumekamilisha kwa sasa tunatekeleza mambo makubwa zaidi.”

Summary: Daraja hilo ni miongoni mwa mawili yatakayojengwa, lingine likitarajiwa katika eneo la Amani, huku pia kukiwa na ujenzi wa barabara za urefu wa kilometa 100. 9 ulioanza Desemba mosi, 2023 ukitarajia kukamilika Machi 2025 kwa gharama ya zaidi ya Sh45 bilioni.

Huku akitoa kijembe cha kuwashangaa wanaobeza maendeleo yanayofanyika visiwani humo, Dk Mwinyi amesema: “Kama wanadhani tumemaliza hapa ndio tunaanza, kuna kitu kinaitwa ‘interchange’, haya madaraja ya juu ndio yanakuja.”

Amesema anashangaa mtu mzima anasimama hadharani anasema wanawajenga barabara kama vichochoro, “ndugu zangu, mambo mazuri yanakuja, tumeshatoka kwenye Hussein mabati na sasa tupo Hussein maflyover, kama hawakuona ardhini basi tazameni angani wasipoona basi hilo ni tatizo.”

Huku akielezea furaha yake, Dk Mwinyi amesema: “Leo tupo hapa, nafurahi kwa mara ya kwanza katika kisiwa chetu tunajega barabara ya juu, pale ninaposema tuwe na uongozi wa kuacha alama ndio haya, hii ni alama ya kudumu.”

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili maendeleo zaidi yazidi kupatikana.

Kadhalika, amewataka wananchi kutunza miundombinu hiyo na kuacha kujenga nyumba karibu na barabara, kwani hali hiyo inakwamisha baadhi ya miradi kufanyika kwa ufanisi.

Akitoa taarifa ya kitaalamu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Haji Machano amesema ujenzi wa madaraja hayo ni sehemu ya ujenzi wa barabara za mjini, zenye urefu wa kilometa 100.9 unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani 19 milioni (zaidi ya Sh45 bilioni).

Amesema ujenzi wake umefikia asilimia 80, jumla ya nguzo 48 zimejengwa na kila nguzo moja imeunganisha nguzo za chini nane katikati ya daraja na nguzo za chini 12 kwa maeneo ya upande wa mwanzo na mwisho katika kuunganisha daraja hilo.

Amesema kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi ndani ya mji wa Zanzibar na vyombo vya moto vimeongezeka, hivyo kukabiliwa na changamoto ya kuwapo foleni katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Machano, Serikali imetumia Sh2 bilioni kufidia wananchi waliopisha ujenzi wa daraja hilo.

“Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ujenzi wa foundation (msingi) na kuta za kuwekea chelezo na gari zitakazoanza kupanda kuelekea juu,” amesema.

Daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 72 na kina cha mita sita kwenda juu, upana mita 18, barabara za juu mbili zenye upana wa mita 8.35 kila moja na barabara za chini zenye upana wa mita nane.

Amesema ujenzi huo pia unajumuisha mitaro ya maji ya mvua na njia za watembea kwa miguu na itakuwa na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa kila upande kwenda na kurudi.

Kukamilika kutapunguza msongamamo wa foleni katika makutano ya barabara za Mwanakwerekwe na Amani.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Mohamed Salum amesema pia zinatengenezwa barabara zenye urefu wa kimeta 897.2 Unguja na Pemba kati ya mfumo rasmi wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,344.

“Leo unaweka legacy (alama) ni flyover ya kwanza Zanzibar, tayari tunajenga daraja Chwaka na Chakawe na Uzi Ngwamba lenye urefu wa kilometa mbili.

Related Posts