Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekamilisha chaguzi za Kanda za Kaskazini na Kati na kupata viongozi wapya watakaoongoza kanda hizo kwa miaka mitano ijayo.
Katika uchaguzi uliofanyika Sanawari, Arusha, Desemba 19, 2024, Samwel Welwel alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, akipata kura 51 dhidi ya Michael Kilawila aliyepata kura 48. Awali, uchaguzi huo ulilazimika kurudiwa baada ya mshindi kutopata zaidi ya asilimia 50 ya kura, kama inavyotakiwa na Katiba ya Chadema.
Welwel anachukua nafasi ya Godbless Lema, ambaye alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo. Kupitia akaunti yake ya X, Lema amempongeza Welwel na kuahidi kushirikiana naye katika kuimarisha kanda hiyo.
Awali Kilawila alipata kura 46 akifuatiwa Samwel Welwel 42, huku Anthony Mallya akiambuliwa kura 12, ndipo ulirudiwa kwa kuwashindanisha Kilawila na Welwel aliyeibuika mshindi.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Patrick Ole Sosopi alimtangaza Welwel kushinda nafasi baada ya kupata asilimia 51 huku mpinzani wake, Kilawila akipata asilimia 48.
Kupitia akaunti yake ya X, Lema ambaye ni Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini ameandika, “hongera sana mheshimiwa mwenyekiti wangu wa kanda wewe na timu yako, nakutakia wajibu mwema katika kanda yetu ya Kaskazini.
“Nitafanya kazi na wewe kwa kadri utakavyoelekeza na kuongoza. Nimefurahi sana, nimekuwa na siku nzuri kabisa leo, Mungu akubariki bosi wangu,” ameandika Lema.
Katika uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia Ijumaa, Desemba 20, 2024, Devotha Minja alichaguliwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kati, akipata kura 55 sawa na asilimia 56.5, akifuatiwa na Ezekiel Chisinjila aliyepata kura 33.
Wengine ni David Jumbe aliyepata kura saba, Idd Kizota aliyepata sifuri sawa Shujaa Evarist aliyepata sifuri.
Shughuli pevu ilikuwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti ambapo kulikuwa na mchuano mkali kati ya Imelda Malley na Jingu Jackson katika awamu ya pili Jackson alishinda kwa kura 55 sawa asilimia 59 dhidi ya Malley 37 sawa asilimia 40.
Vilevile upande wa mhazini wa kanda kulikuwa na mchuano kati ya Kapalatu Singamagazi na Modestus Chitemi. Hata hivyo, baada ya uchaguzi kurudiwa Chitemi alipata kura 53 sawa asilimia 57 huku Singamazi akipata kura 38 sawa asilimia 41.3.
Minja, ambaye ni mbunge wa zamani wa viti maalumu na mwanahabari kitaaluma, anachukua nafasi iliyokuwa wazi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa kanda hiyo, Lazaro Nyalandu kurejea CCM.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano huo, Jumbe alizungumza kwa ufupi akisema, mara zote anapenda kujifunza na kuhusu mchakato huo amejifunza pia. Uchaguzi huo uliomalizika saa 8 usiku wa kuamia Ijumaa ulikwenda vizuri.
Hadi sasa, Chadema imeshafanya chaguzi katika kanda tisa kati ya 10, ikisalia na Kanda ya Unguja. Kanda zilizofanya uchaguzi ni pamoja na Pwani, Kusini, Magharibi, Kati, Kaskazini, Pemba, Victoria, Nyasa na Serengeti.
Viongozi wapya wa kanda hizo ni pamoja na Boniface Jacob maarufu ‘Boni Yai’ (Pwani), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Nyasa), Dickson Matata (Magharibi), Devotha Minja (Kati), Samwel Welwel (Kaskazini), Aden Mayala (Kusini), na Omary Othman Nassoro (Pemba).
Karibu wote hao ni sura mpya katika Kamati Kuu ya Chadema itakayohudumu kwa miaka mitano ijayo, isipokuwa Sugu na Boni Yai ambao waliowahi kuwa kwenye Kamati Kuu ya mwaka 2015/2020.