Njombe. Serikali ya Mkoa wa Njombe imesema haitafumbia macho matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia yanayofanyika mkoani humo ambapo pamoja na hatua za kisheria, majina ya wahusika wa matukio hayo yatatangazwa hadharani ili jamii iwafahamu.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 20, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka kwenye mkutano maalumu wa kujadili maadili, ukatili wa kijinsia na matukio yanayofedhehesha mkoa huo.
Kauli hiyo ya Mtaka imekuja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga kueleza kuwa tangu mwaka 2020 hadi 2024, jumla ya matukio 367 ya mauaji yametokea mkoani humo, ya unyang’anyi wa kutumia silaha 16 na unyang’anyi wa kutumia nguvu 48.
Amesema matukio mengine yaliyoripotiwa katika kipindi hicho ni ya ubakaji ambayo ni 829 na ulawiti ni 91. Ameongeza kuwa uchunguzi wao umebaini kuwa matukio mengi yanafanywa na ndugu au majirani wa karibu.
“Kwa upande wa makosa ya mauaji, mwaka 2020 tulikuwa na matukio 88, mwaka 2021 yalikuwa 69, mwaka 2022 yalikuwa 73, mwaka 2023 yalikuwa 77 na mwaka 2024 hadi Novemba, kuna matukio 60 likiwemo lililotokea hivi karibuni la unyang’anyi wa kutumia silaha lililosababisha mauaji ya mfanyabiasha,” amesema Banga.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Njombe, Elice Simonile amesema sababu ya kuwepo kwa ukatili ni jamii ya watu wa mkoa huo kuwa na usiri mkubwa ambao unapelekea watu katika familia kushindwa kutoa taatifa ya matukio ya ukatili mara yanapotokea.
“Lakini kuna Ramli chonganishi zinazofanywa na waganga wa kienyeji lakini pia kutokuwa na hofu ya Mungu miongoni mwa wanajamii wa Njombe, kiasi cha kushika imani ya asili na ile ya Mungu,” amesema Simonile.
Akizungumzia matukio hayo, Mtaka amesema mkoa huo hauwezi kukaa kujadili masuala ya maendeleo kwa wananchi na kufanikiwa kama matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia yataendelea na wahusika hawachukuliwi hatua.
Amesema lazima kuwepo na kampeni mahsusi ya kimkoa kujadili namna bora ya kukomesha matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia na ikiwezekana wahusika wa ubakaji wawekwe hadharani ili jamii iwatambue.
Ameeleza sababu kubwa ya kutokea kwa matukio hayo ni kumomonyoka kwa maadili ya jamii ya kuanzia ngazi ya familia kuelekea mitaani mpaka kwenye nyumba za ibada ambapo huko kote elimu inapaswa kutolewa.
“Sisi kama Serikali ya Mkoa tumesikitishwa na kufedheheshwa kwa matukio yanayohusiana na ukatili wa kijinsia, madawati yetu ya polisi ya jinsia, maofisa wetu wa ustawi wa jamii, idara yetu ya afya na maofisa wote wa Serikali ambao mambo haya yanawafikia, walete taarifa zifanyiwe kazi na ionekane kwamba kazi imefanyika,” amesema Mtaka.
Mtaka amesema wataandika waraka na kupeleka kwenye nyumba zote za ibada kwa ajili ya kukemea matukio maovu na mabaya ya ukatili wa kijinsia na mauaji yanayofedhehesha na kutweza utu wa mwanadamu kwenye Mkoa wa Njombe.
Amewaomba viongozi wa dini na wale wa kimila kuwa mstari wa mbele katika kukemea matendo ya aina hiyo ikiwemo kuwakumbushwa waumini wao suala la maadili ili kupunguza uhalifu huo mkoani Njombe.
Amemwagiza Kamanda Banga kufanya kazi ipasavyo ili kuhakikisha wanaofanya matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia wanakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Pia, amewataka wananchi mkoani Njombe kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa matukio ya aina hiyo kwa kuwa wapo kwenye jamii inayowazunguka na wengine ni ndugu wa familia.
Ofisa Uangalizi Mfawidhi Mkoa wa Njombe kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Monica Mlawa ameshauri kwamba ili kupunguza matukio hayo vyombo vya kutoa haki vinapaswa kutenda haki kwa uadilifu na kuepukana na vitendo vya rushwa.
“Mfano mhalifu ametenda kosa, wananchi wanatarajia aadhibiwe kulingana na kosa alilotenda, sasa asipoadhibiwa akaachiwa huru, lazima watajichukulia sheria mkononi,” amesema Mlawa.
Sheikh Ibrahim Chang’a wa Makambako ameunga mkono hoja ya Mtaka akisema watu wanaolawiti watoto wadogo au watu wazima na wanaobaka ni takataka kwa kuwa wanaenda kinyume na maadili na maadiko ya dini.
“Watu hawa kwanza hawatangazwi, nilidhani wawe wanatangazwa katika jamii, kwamba huyu mtu kamlawiti mtoto wa fulani mahala fulani na wapelekwe kwenye mkutano wa hadhara chini ya polisi kwa huyu ndiyo tabia yake ili tumjue” amesema Chang’a.