Pamba yamng’oa straika Mkenya | Mwanaspoti

PAMBA Jiji imepania hasa katika dirisha dogo la usajili, ikielezwa imemalizana na klabu ya Naspa Stars ya Zambia, Rally Bwalya, huku ikiwa hatua ya mwisho ya kumsajili mshambuliaji wa Shabana inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kenya, Tegisi Mathew.

Tuanze na Bwalya, imefikia makubaliano na Napsa Stars iliyopo Ligi Kuu Zambia, ili kupata huduma ya kiungo mshambuliaji Larry Bwalya kwa mkopo wa miezi sita.

Mkataba huo umejumuisha kipengele cha kumsajili jumla, ikiwa watavutiwa na nyota huyo ambaye aliwahi kuwika Ligi Kuu Bara akiwa na wekundu wa Msimbazi, Simba kabla ya kutimkia Afrika Kusini.

Awali, Pamba Jiji ilionyesha nia ya kumleta Bwalya kwa usajili wa moja kwa moja katika dirisha hili la usajili, lakini walishindwa kufikia makubaliano na klabu yake ambayo bado ana mkataba nayo wa mwaka mmoja.

Hata hivyo, baada ya majadiliano ya kina kwa pande zote mbili, klabu hizo zimefikia makubaliano ya mkopo, na sasa Bwalya atajiunga na kikosi cha Pamba kwa ajili ya kuimarisha safu ya kiungo cha timu hiyo.

Bwalya, ambaye ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Napsa Stars, anatarajiwa kutua Tanzania mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili wake na kusaini mkataba rasmi.

Kwa ishu ya Tegisi, inaelezwa viongozi wa Pamba imevunja mkataba wa mchezaji huyo kwa miaka miwili na kumnunua moja kwa moja ikielezwa ni chaguo la kocha Fred Felix Minziro.

Hata hivyo, Tegisi anatazamwa na Minziro kuja kuongeza ushindani kwenye eneo la ushambuliaji ikiongozwa na George Mpole mwenye mabao mawili.

Chanzo kililiambia Mwanaspoti, hadi sasa dili hilo limekamilika kwa asilimia 80 ikisubiriwa nyota huyo kuja Tanzania kuanza mazoezi na wenziwe.

“Ni kweli wamevunja mkataba na Shabana na kila kitu kimeenda sawa muda wowote kuanzia sasa vibali vyake vya kazi vitatoka kilichobaki ni kuja Tanzania na kuanza mazoezi na timu.” kilisema chanzo hiko

Hata hivyo, Tegisi mapema wiki hii ameaga rasmi klabuni hapo na mechi yake ya mwisho ilikuwa Desemba 15, Shabana hiyo ikishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya KCB.

“Umekuwa mwaka wa kipekee, uliosheheni ukuaji wa kibinafsi na taaluma, ninashukuru sana Shabana kwa kunipa nafasi, kwenda Pamba ni fursa kubwa kwangu kuchunguza ligi mpya na nchi mpya, naiona kama hatua muhimu kuelekea ndoto yangu ya kucheza katika ligi za juu nje ya nchi,” alisema

Mwanaspoti ilipomtafuta Ofisa Habari wa Pamba, Moses William juu ya uhamisho huo alisema “Kama tulivyosema mambo yakiwa sawa mtaambiwa kwa sasa dili hilo haliko.”

Msimu huu mshambuliaji huyo amefunga mabao matano kwenye mechi 11 akiwa nafasi ya pili kwenye vinara wa upachikaji mabao juu ya Brian Michira mwenye nayo saba.

Related Posts