Pwani. Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesisitiza mambo matano kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHWs), pindi wanawapopokea wagonjwa, ikiwamo kuwapima kiwango cha shinikizo la damu.
Mambo mengine ni kuwapima kiwango cha mafuta mwilini, upana wa kiuno, akizingatia ukubwa unaoshauriwa sentimita 35 kwa mwanamke na 40 kwa mwanaume, kupima urefu na ugonjwa wa sukari.
Amesema hayo leo Ijumaa Desemba 20, 2024 kwenye ziara ya kujionea utoaji huduma, iliyohusisha mkutano na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs) uliofanyika Chuo cha Afya Kibaha.
Akizungumza na wahudumu hao wanaopatiwa mafunzo na Chuo cha Afya Excellent, Profesa Janabi amesema mambo hayo matano ni muhimu kuzingatiwa wanapotoa elimu ya afya kwa wananchi.
Profesa Janabi ambaye pia ni mshauri wa Rais wa masuala ya afya, ametaja mambo hayo akisisitiza kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanayomshambulia binadamu yanachangiwa na mfumo wa maisha na asilimia 25 yanatokana na kurithi.
Amesema watoa huduma wa afya ngazi ya jamii ni kiungo muhimu kati ya wananchi na vituo vya kutolea huduma na endapo magonjwa yatadhibitiwa kuanzia ngazi ya jamii, wananchi watajitika zaidi kwenye maendeleo badala ya kutumia muda mwingi hospitali.
“Elimu ya afya ikitolewa kuanzia ngazi ya jamii watu wengi hawatafika hospitali na tutapunguza vifo vya akina mama na tutafanikisha kukinga kuliko kutibu,” amesema.
Akizungumzia bima ya afya kwa wote, Profesa Janabi amesema mpango wa Serikali kutumia watoa huduma wa afya ngazi ya jamii, utawezesha wananchi kupata elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Samwel Lema amesema baada ya Serikali kuvichagua vyuo vya kutoa mafunzo kwa watoa huduma wa afya ngazi ya jamii, mkoa huo unawapatia mafunzo CHWs 207 watakaotumika kwenye mkoa huo.
Naye Mratibu Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Dk Norman Jonas amesema lengo la uwepo wa watoa huduma hao ni kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii.
Amesema mikoa 12 nchini ndio imefikiwa na watoa huduma wa afya ngazi ya jamii na kufikia mwaka 2028 mikoa yote itakuwa na watoa huduma wawili kila mtaa.
Akizungumzia Mradi wa Afya Tek, Ofisa Mradi wa programu hiyo, Fatma Mahmoud amesema matumizi ya Tehama kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii kumewezesha upatikanaji wa takwimu wa vifo vya mama na mtoto.
Akizungumzia mafunzo waliyopata kuhudumia jamii, Batuli Maero mtoa huduma Mkoa wa Pwani amesema mafunzo waliyopatiwa yanawawezesha kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi.
Jukum,u jinginw ni kufuatilia wagonjwa kwa karibu na kurekodi maradhi yao na kuwapangia vituo vya afya vya rufaa wanazopaswa kwenda kupata huduma za afya.