Sababu mgonjwa kuwekewa betri ya moyo na asiyopaswa kuyafanya

Watanzania takriban 25 wanapandikizwa betri ya moyo kila mwezi, sawa na takriban watu 300 kwa mwaka. Hili ni ongezeko kutoka watu 150 waliopandikizwa betri hiyo mwaka 2015/16.

Kwa upande mwingine, takriban watu 400 hadi 500 hufika kliniki ya wagonjwa wa nje (OPD) katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kila siku.

Kitaalamu, betri ya moyo (Pacemaker) ni kifaa maalumu kinachosaidia kurekebisha mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.

Kifaa hiki hufanya kazi kama jenereta, kikirejesha mfumo wa umeme wa moyo ili kuhakikisha unafanya kazi kwa mpangilio sahihi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa katika tovuti mbalimbali za kiafya, ikiwamo ya American Heart Association, kuna watu zaidi ya milioni tatu wanaishi na betri hizo duniani, huku betri 600,000 zikipandikizwa kila mwaka.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Daktari Bingwa bobezi wa magonjwa na mishipa ya moyo JKCI, Dk Khuzeima Khanbhai anasema kinachofanya mtu awekewe betri ya moyo ni pale mapigo yanapokuwa chini na hayako kwenye mwelekeo unaohitajika.

“Kwa kawaida mapigo ya moyo ya mwanadamu yanapaswa kuwa kati ya 60 na 100, ikitokea yapo chini na pia hayapo kwenye mwelekeo unaohitajika, basi mtu anawekewa kifaa hicho ili kunyanyua mapigo,” anasema Dk Khanbhai.

Akifafanua kitaalamu, anasema kwenye moyo kuna jenereta tatu ambazo zina kazi ya kufanya mapigo ya moyo yaende sambamba, kuanzia kwenye jenereta ya juu ambayo ndiyo ya kwanza kwenda kupeleka umeme.

Anasema ufanyaji kazi wa jenereta hizo ndipo moyo unapumua. Changamoto inayoweza kutokea kwenye mfumo wa umeme wa moyo, kinachotokea jenereta ya juu au katikati ikipata ugonjwa husababisha mapigo ya moyo yapungue.

Ikitokea changamoto kwenye mfumo wa umeme wa moyo ndipo mgonjwa anawekewa betri inayorejesha mapigo kuwa sawa. Anasema kwa namna ilivyosetiwa, betri inapandisha hadi mapigo kufikia 60.

“Betri ya moyo ni kama jenereta ya nyumbani ya kuzalisha umeme ambapo umeme ukiwa hakuna inafanya kazi, umeme ukirudi basi inazimwa.”

Dk Khanbhai anasema kuna sababu za nje ya mfumo wa moyo zinazosababisha moyo uende taratibu, ikiwemo mgonjwa wa goita, mishipa ya moyo kupata ugonjwa, wanawekewa betri za muda kwa ajili ya kuzibua mapigo.

Anasema mtu anayewekewa betri ni yule ambaye mapigo yake ya moyo yapo chini na hayapo katika mpangilio unaotakiwa.

“Lakini si wote ambao mapigo yao ya moyo yapo chini wanahitaji pacemaker, kuna watu ambao mapigo yao yapo chini, mfano wachezaji wana hali hiyo kuwa na 45 hadi 50, wakimbiaji wa muda mrefu ni kawaida kwa kuwa moyo umeshazoea mazoezi,” anasema Dk Khanbhai na kuongeza:

“Tunaongelea mwelekeo wa mfumo wa umeme kutoka chemba moja kwenda ya pili kupoteza mwelekeo au mwelekeo upo lakini mapigo yako chini,” anafafanua.

Sababu za mapigo kuwa chini

Dk Khanbhai anasema kijana akipata ugonjwa unaoweza kusababisha uvimbe katikati ya moyo au moyo kuvimba, shinikizo la damu kwa wazee, mtoto kuzaliwa na changamoto, basi inaweza kusababisha mapigo ya moyo kwenda chini.

Anasema watu waliohatarini kupata shida inayosababisha kuwekewa pacemaker ni wagonjwa wenye umri kwanzia miaka 60 ambapo asilimia tano wanaweza kupata shida hiyo na wenye magonjwa yasiyoambukiza

Wagonjwa wengi ni wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea, lakini kwa wengine waliochini ya umri huo pengine waliwahi kupata ugonjwa wa moyo wakiwa na umri mdogo.

Dk Khanbhai anasema dalili za mtu mwenye shida inayotaka kuwekewa betri ni kizunguzungu kwa sababu hewa ya oksijeni hupungua kutoka kwenye moyo, kudondoka, kuchoka na pumzi kubana.

Aidha, akitaja hatari ya mapigo ya moyo kuwa chini, anasema ni kufeli kwa moyo, pumzi kubana, kifua kuuma, kizunguzungu na mwili kuwa dhaifu.

Hata hivyo, anasema maisha ya mtu anayewekewa betri hayabadiliki, bali hataruhusiwa kupita maeneo yenye sumaku ambayo inaingilia programu ya betri hiyo.

“Wenye betri huwa tunawapa kadi maalumu ya kupita kwenye maeneo yenye sumaku, kama viwanja vya ndege atakayokuwa anatembea nayo kama utambulisho,” anasema.

Anasema betri hiyo huwekwa mwilini kupitia upasuaji mdogo bila ya dawa za usingizi. Inaweza kuwekwa mkononi kwenye misuli iliyokaribu na eneo la titi. Ambapo moja kwa moja nyaya zake zinaenda kwenye chemba za moyo kwaajili ya ufanyaji kazi.

Anasema mgonjwa akiwekewa betri kisha mapigo ya moyo yakarudi, basi betri hiyo itasimama kufanya kazi na hukaa nayo mwilini kwa muda wa miaka tisa hadi 10.

Hata hivyo, anasema takwimu hizo za wagonjwa zinakuja baada ya uelewa wa watu juu ya magonjwa ya moyo kuongezeka.

“Kuhusu mwitikio wa watu juu ya magonjwa ya moyo, kwa sasa tunawapata wagonjwa wengi kutoka mikoa mbalimbali wanaokuja JKCI, nafikiri kutokana na kufahamika tofauti na zamani. Matibabu ya betri ya moyo yanawezekana kwa gharama nafuu,” anaeleza Dk Khanbhai.

Related Posts