Straika Azam anukia Kagera Sugar

Kagera Sugar ipo katika hatua za mwisho kumchukua mshambuliaji wa Azam FC, Adam Adam kwa mkopo.

Kagera kwa sasa ipo katika mikakati ya kuongezea nguvu kikosi chake kutokana na ripoti ya Kocha Melis Medo iliyotoka hivi karibu.

Awali Mwanaspoti iliripoti benchi la ufundi la timu hiyo linataka kusajili mashine nne mpya dirisha dogo lililofunguliwa Jumapili iliyopita.

Katika ripoti hiyo ambayo Mwanaspoti imepenyezewa na mabosi wa juu wa Kagera, Meddo anahitaji kipa wa maana atakayekuja kusaidiana na makipa wawili Ramadhan Chalamanda na Said Kipao.

Mbali na kipa huyo, pia ripoti hiyo ya Medo inahitaji beki mmoja wa kushoto na washambuliaji wawili wenye ubora mkubwa na wote wawe wazawa.

Taarifa za ndani zinasema: “Ripoti hiyo imeanza kufanyiwa kazi na miongoni mwa washambuliaji wawili wanaohitajika na kocha mmoja wapo ni Adam. Sababu za kumchukua mshambuliaji huyo ni kuongeza nguvu katika eneo hilo na uzoefu aliokuwa nao katika michuano ya ligi kwani sio mchezaji mgeni.”

“Tunataka kuwapata wazawa ambao wana uzoefu tunaoamini uwezo wao utakuja kuongeza kitu wakichanganyika na hawa tutakaowabakiza,” kilisema chanzo hicho.

Rekodi za mshambuliaji huyo zinaonyesha amewahi kuichezea Polisi Tanzania msimu mmoja, huku timu zilizofuatia zote akicheza miezi sita ambazo ni Mtibwa Sigar, Singida Black Star, Mashujaa na Azam FC aliposajiliwa dirisha kubwa msimu huu.

Kagera Sugar ipo eneo la hatari kwenye msimamo wa ligi wakishikilia nafasi ya 14 wakiwa na pointi 11 na hesabu zao ni kujiondoa hapo ili isizidishe hesabu za kuweza kushuka daraja.

Related Posts