Katika ujumbe wake ulioandikwa kwenye sentensi moja fupi, Elon Musk amesema, ”Ni AfD pekee inayoweza kuiokoa Ujerumani”.
Hii si mara ya kwanza kwa tajiri huyo namba moja duniani kuunga mkono vyama vyenye sera za kupinga wahamiaji barani Ulaya.
Mwezi uliopita alipigia kampeni kufukuzwa kwa jaji wa Italia, aliyetilia shaka sera ya serikali ya nchi hiyo dhidi ya uhamiaji wa kiholela.
Soma pia: Scholz akiri matokeo yaliyokipa ushindi chama cha AfD yanatia wasiwasi
Wanasiasa wa Ujerumani wamemkosoa Elon Musk, wakisema alichokifanya ni uingiliaji wa siasa za ndani za nchi yao, ambayo inaandaa uchaguzi wa bunge mapema mwakani.
Maoni ya Wabunge Kuhusu Kauli ya Elon Musk
Clara Bünger wa chama cha mrengo wa kushoto alieleza kuwa kauli hiyo ni uingiliaji wa wazi, lakini haina uzito wowote kwani Musk hana uelewa wa mfumo wa siasa za Ujerumani.
Alexander Throm wa chama cha kihafidhina CDU, alisema ameshangazwa na kauli hiyo, akisisitiza kuwa mabadiliko yanaweza kufanywa tu na chama kilicho madarakani, na kusisitiza kuwa chama cha AfD hakitaingia serikalini kwa sababu hakuna chama kingine tayari kushirikiana nao.
Soma pia: Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD chashinda uchaguzi Thuringia
Anton Hofreiter wa chama cha walinzi wa mazingira alikemea vikali, akiwataja mafashisti kama wasaliti wanaoungwa mkono na mabilionea wa mrengo wa kulia kama Musk, akiashiria pia msaada wao wa awali kutoka kwa Putin.
Kauli hizi zinaonyesha mitazamo tofauti ya wanasiasa juu ya ushawishi wa bilionea huyo katika siasa za Ujerumani.
Scholz: Hata mabilionea wana uhuru wa maoni
Hata Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameelezea mtazamo wake kuhusiana na ujumbe huo wa Musk.
Scholz amesema uhuru wa watu kutoa mawazo unawaruhusu pia mabilionea kusema fikra zao, hata ikiwa fikra hizo sio sahihi na hazina maudhui yoyote yenye tija kisiasa.
Chama cha AfD alichokimwagia sifa Elon Musk kinaendesha siasa zake kwa misingi ya chuki dhidi ya wahamiaji, na pia kinapinga Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Wajerumani weusi wahofia ushindi wa AFD majimbo ya mashariki
Katika kura za maoni kipo katika katika nafasi ya pili, huku Ujerumani ikielekea katika uchaguzi wa Februari 23 mwakani, ulioitishwa mapema baada ya kusambaratika kwa serikali ya muungano wa vyama vitatu iliyoongozwa na Kansela Olaf Scholz.
Bilionea Elon Musk ambaye ni mpambe wa rais mteule wa Marekani Donald Trump, tayari amekwishaviunga mkono vyama vingine vya mrengo mkali wa kulia katika mataifa tofauti barani Ulaya.