Mpango huo, ulioungwa mkono na na mshauri wake Elon Musk, ulishindwa kwa kura 235 dhidi ya 174, ambapo Warepublican 38 waliungana na karibu Wademocrat wote kuupinga.
Hali hii imeiacha Congress bila mpango wa wazi wa kuepusha kufungwa kwa shughuli za serikali.
Spika wa Bunge, Mike Johnson, ambaye ni Mrepublican, amewekwa katika nafasi ngumu, hali inayokumbusha mizozo ya hivi karibuni ya Warepublican kuhusu uongozi wa Bunge na ukosefu wa mshikamano ndani ya chama chao.
Soma pia: Shughuli za serikali ya Marekani zaanza kufungwa
Johnson aliungana na Musk kuupigia chapuo mpango mpya, baada ya tajiri huyo wa teknolojia, kuwahimiza Warepublican kuukata mpango wa awali kupitia jumbe za mfululizo kwenye jukwaa lake la mtandao wa kijamii wa X.
Sheria hiyo ingeendeleza shughuli za serikali hadi katikati mwa mwezi Machi, na kusimamisha ukomo wa deni la taifa kwa miaka miwili ya kwanza ya utawala wa Donald Trump.
Hata hivyo, mpango huo uliwakera baadhi ya Warepublican wenye msimamo wa kubana matumizi, ambao waliwaonya wenzao kuhusu hatari za kuondoa kikomo cha deni.
Walihoji kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha utulivu wa kifedha wa taifa, na hivyo kuzua upinzani mkali ndani ya chama.
Wakati huo huo, Wademocrat hawakuwa tayari kuwasaidia Warepublican. Walilalamika kuwa ufadhili wa programu muhimu za kijamii ulikuwa umeondolewa kwenye mswada huo.
Kiongozi wa Wachache bungeni, Hakeem Jeffries, aliwakosoa Warepublican, akisema walikuwa wanasukumwa na ufuasi wa kipofu kwa sera za Trump za “Make America Great Again” (MAGA).
“Pendekezo la Musk-Johnson haliko makini. Ni la kuchekesha. Warepublican wenye msimamo mkali wa MAGA wanatusukuma kwenye kufungwa kwa serikali,” alisema Jefferies ambaye ni kiongozi wa Wabunge wa Democrat.
Ni mwanzo wa upinzani dhidi ya Trump?
Akizungumza baada ya kushindwa kwa mpango wake, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mike Johnson ameelezea kuvunjwa moyo na upinzani wa wademocrat dhidi ya muswada huo, na kuahidi kuja na suluhisho jengine.
“Tofauti pekee kwenye sheria hii ilikuwa kusukuma kikomo cha deni hadi Januari 2027”, alijitetea spika huyo mbele ya waandishi wa habari.
Hali iliyotokea bungeni Alhamisi ilikumbusha changamoto nyingi ambazo Trump alikabiliana nazo wakati wa muhula wake wa kwanza wa uongozi.
Trump alikuwa rais mara ya mwisho serikali ilipofungwa mwaka 2018, ambapo wafanyakazi wa serikali takriban 800,000 walikaa nyumbani kwa siku 34.
Kinachosubiriwa kuonekana sasa ni mara ngapi au jinsi gani Warepublican, hasa kwenye Baraza la Wawakilishi, watakwenda kinyume na Trump.
Bunge linaonekana kuwa na wanachama wengi wa mrengo mkali wa kulia na wafuasi waaminifu wa Trump kuliko Seneti, lakini wachambuzi wanasubiri kuona kama upinzani wa Alhamisi ulikuwa tukio la pekee au mwanzo wa matukio zaidi.