Aliyekuwa CEO Simba ageuka lulu Rwanda

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Francois Regis, ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara ya michezo Rwanda.

Regis ambaye alidumu Simba katika muda usiozidi miezi miwili, uteuzi wake wa nafasi hiyo ya ukatibu mkuu wa wizara ya michezo umetangazwa jana na waziri wa michezo wa nchi hiyo Edouard Ngirente na umefanywa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Kabla ya kuibukia katika nafasi hiyo, Regis alikuwa mtendaji mkuu wa Simba, nafasi ambayo aliitumikia kwa miezi minne tu kabla ya kufikia makubaliano na klabu hiyo ya kuachana kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.

Novemba 23, Simba ilitangaza uamuzi wa Regis kutoendelea kuitumikia huku nafasi yake ikichukuliwa na Zubeda Sakuru ambaye anaikaimu hadi hivi sasa wakati ikisaka mtendaji mkuu wa kudumu.

“Tunapenda kuutarifu umma kuwa Klabu ya Simba imefikia makubalino ya kusitisha mkataba na ndugu Francois Regis ambaye alikuwa ni Mtendaji Mkuu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu. Tunamshukuru Mr. Regis kwa kipindi alichohudumu katika klabu yetu.

“Bodi imefanya uteuzi wa Bi. Zubeda Hassan Sakuru kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu,” ilifafanua taarifa ya Simba kuachana na Regis na kumkaribisha Zubeda Sakuru.

Regis, alikuwa CEO wa pili raia wa kigeni kuhudumu ndani ya Simba baada ya Senzo Mbatha kutoka Afrika Kusini ambaye alikaa kwa msimu mmoja wa 2019/20 kabla ya kuhamia Yanga.

Wasifu wa Regis unaonyesha kuwa ana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika uongozi wa michezo na hasa soka.

Amewahi kuwa mtendaji mkuu wa Chama cha Soka Rwanda kwa zaidi ya miaka mitatu, amekuwa makamu mwenyekiti wa klabu ya APR na pia amewahi kuwa mratibu mkuu wa mechi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Ni miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha makocha wa soka Rwanda ambacho amewahi kuwa makamu wake wa rais.

Regis pia ana taaluma ya ukocha wa soka akiwa na leseni ngazi B ya umoja wa vyama vya mpira wa miguu Ulaya (Uefa) aliyoipata Ujerumani.

Ni mtaalam wa masuala ya utawala wa biashara akiwa na elimu ngazi ya shahada ya uzamili (Masters) na pia ana cheti cha kimataifa cha utunzaji fedha za umma (IPSAS).

Amewahi kufanya kazi kama mkaguzi mkuu wa ndani wa Rwanda, mkurugenzi wa utawala na fedha na pia mkurugenzi wa uendeshaji wa taasisi tofauti ndani ya Rwanda.

Related Posts