KIUNGO wa KenGold, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, ameelezea kuwa wakati umefika kwa wachezaji wa timu hiyo kujitathmini na kubadilisha mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara, ambayo wanaburuza mkia.
Hii ni baada ya KenGold kushinda mechi moja tu, kutoa sare tatu, na kupoteza kumi na moja katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.
Masoud ‘Cabaye’, alisema kuwa huu ni wakati muhimu kwa wachezaji na viongozi wa timu kujitathmini kwa kina, ili kurekebisha makosa na kuonyesha uwezo wao ili kupambana na changamoto zilizopo mbele yao.
“Sasa ni wakati wa kutambua makosa yetu na kurekebisha hali hii. Ligi Kuu Bara ni vita, kila timu ina nafasi ya kushinda na kila mechi ni muhimu kwa mustakabali wetu,” alisema Cabaye, akisisitiza kuwa mabadiliko ya haraka ni lazima ili kuepuka kushushwa daraja mwishoni mwa msimu.
Aliendelea kusema kuwa ingawa wanajua changamoto waliyonayo, bado wanaamini kuwa wakiwa na umoja na juhudi, wanaweza kubadili mwelekeo wa msimu huu.
Cabaye aliongeza kuwa, “Tunajua mechi yetu ijayo dhidi ya Singida Black Stars ni ngumu, lakini kila mechi ni fursa kwetu. Lazima tujitahidi na kuwa na umoja uwanjani. Kwa sasa tunahitaji kujiinua na kuonyesha ubora wetu kama wachezaji wa KenGold.”
Katika mchezo huo, KenGold itakuwa ugenini huko Singida, kukabiliana na wenyeji wao, ambao wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 30. Huu utakuwa mtihani mkubwa kwa KenGold, kwani Singida inaonekana kuwa tishio msimu huu.