Moshi. Wakati wanafunzi 30,901 wakitarajiwa kujiunga kidato cha kwanza Januari 2025, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro imesema maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao yamekamilika, huku zaidi ya Sh17 bilioni zikitumika kuboresha miundombinu ya madarasa, mabweni na ujenzi wa shule mpya 14.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Yusuf Nzowa amesema hakuna changamoto yoyote ya upungufu wa madarasa na miundombinu mingine, hivyo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni kwa wakati.
“Katika mkoa wetu, wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba 30,901, wakiwemo wavulana 14,721 na wasichana 16,180, mwaka huu wote wamepangiwa shule na Januari 2025 wanapaswa kuripoti kwenye shule walizopangiwa,” amesema Nzowa.
Ameongeza: “Wanafunzi wote ambao wamefaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, watakwenda kidato cha kwanza, hakuna mwanafunzi yeyote atashindwa kwenda shule katika halmashauri zote za mkoa huu kwa sababu yoyote ile, maandalizi yote muhimu yamekamilika.’’
Pia, amewataka wazazi na walezi mkoani humo, kuhakikisha muda utakapofika wanafunzi wote waripoti shuleni kwa wakati kwa kuwa Serikali tayari imeshatekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha madarasa yapo ya kutosha.
“Maagizo ya Serikali ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye atakosa kwenda shule kwa sababu yoyote ile, hivyo niwatake wazazi wafanye maandalizi madogo madogo ya wanafunzi mapema,” amesema Nzowa.
Ameishukuru Serikali kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya sekondari (SEQUIP) ambapo imetoa zaidi ya Sh17 bilioni kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu, ili kuhakikisha wanafunzi mkoani humo wanasoma katika mazingira bora.
“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule mpya 14 ambayo imegharimu Sh10.7 bilioni, madarasa 24 ambayo yamegharimu Sh600 milioni, mabweni 29 ambayo yamegharimu Sh3.8 bilioni pamoja na matundu ya vyoo 121 ambayo yamegharimu Sh243.6 milioni,” amesema Nzowa.
Wananchi wachangamkia mahitaji
Wakati huohuo, Mwananchi imepita katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kushuhudia baadhi ya wazazi wakinunua mahitaji ya wanafunzi ikiwemo sare za shule, soksi pamoja na mahitaji mengine.
Adolfina Joseph, mmoja wa wazazi mkoani humo, amesema ameamua kufanya maandalizi mapema ya mtoto wake mapema ili kupunguza mzigo wa Januari.
“Leo nipo sokoni na mtoto wangu, tunapitia hapa na pale kununua mahitaji mbalimbali ya shule, kama unavyojua Januari mambo yanakuwa ni mengi, kidogo kidogo tunafanya maandalizi,” amesema Adolfina.
Mzazi mwingine mkoani humo ambaye alikuwa soko la Mbuyuni kutafuta vitatu vya shule, amesema kwa kuwa Januari vitu hupanda bei, ameamua kufanya maandalizi hayo mapema kuondoa usumbufu wa Januari ambapo vitu huwa vinapanda bei.