Morogoro. Mwenyekiti wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali nchini, Mwamtumu Mahiza amewataka vongozi wa mashirika hayo kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa badala ya maslahi yao binafsi na mashirika yao.
Mahiza ametoa wito huo Desemba 19, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali mkoani Morogoro ambapo amewataka viongozi hao kuwa wawazi katika shughuli zao za kila siku na kujenga tabia ya kuwashirikisha viongozi wa Serikali kuanzia kwenye ngazi ya mtaa hadi mkoa.
“Serikali na ninyi watu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, wote mnafanya kazi moja ya kuwahudumia wananchi, lakini cha kusikitisha, yapo mashirika ambayo hayafuati sheria na utaratibu, yanakwenda kufanya kazi kwenye vijiji bila kuwajulisha viongozi wa vijiji,” amesema Mahiza.
Amesisitiza kwamba kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yana mchango mkubwa katika kutoa elimu ya uraia, hivyo amewahimiza kufanya kazi hiyo kwa uzalendo na kudumisha amani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala amesema mkutano huo wa viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali umeandaliwa kwa lengo la kujadili changamoto zinazoyakabili mashirika hayo na kuona namna ya kuimarisha ushirikiano baina yao.
“Hapa Morogoro yapo mashirika zaidi ya 470, lakini yanayolipa ada hayazidi 50, hii nayo ni changamoto kwa upande wa mashirika, lakini pia yapo baadhi ya mashirika hayawasilishi taarifa za mwaka za utendaji kazi wao na mengine yanafanya kazi kinyume na shughuli walizokusudia,” amesema Makala.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema pamoja na uhuru waliopewa, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanapaswa kujua uhuru unaenda na mipaka.
Amesema Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa yenye mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali na kupitia mkutano huo wameweza kuboresha uhusiano na kuondoa dhana ya kuogopana ambayo imejengeka kwa baadhi ya mashirika.