Mastraika Pamba ni suala la muda tu

CHANGAMOTO ya ufungaji Pamba Jiji huenda sasa ikapata mwarobaini baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’ kuahidi ujio wa baadhi ya nyota wazoefu na mipango anayoendelea kusuka itatoa suluhu ya tatizo hilo wakati duru la pili la Ligi Kuu kilianza keshokutwa.

Pamba inayokamata nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu, imefunga mabao saba kupitia michezo 15 na kuruhusu 15, huku washambuliaji George Mpole akitupia mawili na Erick Okutu akifunga moja.

Dirisha dogo lililofunguliwa Disemba 15, mwaka huu, timu hiyo imewasajili mshambuliaji, Habib Kyombo kutoka Singida Black Stars, mawinga, Deus Kaseke, Hamad Majimengi na Zabona Mayombya ili kuongeza makali katika eneo la ushambuliaji na nyota wengine wanne wa kigeni.

Minziro alisema eneo la umaliziaji bado linampasua kichwa kwa sababu wanatengeneza nafasi nyingi za mabao lakini hazitumiki ipasavyo, huku akidai usajili waliofanya utaongeza ushindani na kutibu baadhi ya changamoto walizonazo.

“Ni kweli eneo la umaliziaji bado linatusumbua na tumekuwa tukijaribu kulifanyia kazi kwenye mazoezi kila wakati na kurudia kila mara nafikiri pengine tunakosa pia utulivu, kwa hiyo ni vitu tunavyoendelea kuvifanyia kazi, naamini wakipata utulivu tutafunga mabao mengi,” alisema.

Akizungumzia matokeo chanya aliyopata kwenye michezo sita ya mwisho akishinda tatu, sare moja na kufungwa mbili, alisema yanawatia moyo, kuwafanya wajiamini na kuwapa chachu ya kupambana.

Related Posts