Dar es Salaam. Licha ya mabasi kuwapo, upatikanaji wa tiketi umekuwa na changamoto katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, jijini Dar es Salaam, mawakala wakizihodhi na kuuza kwa bei ya juu.
Kutokana na changamoto hiyo inayosababisha baadhi ya abiria kukata tamaa, wamejikuta wakilazimika kukubaliana na mawakala wa mabasi wanaolangua tiketi.
Amina Juma, mfanyabiashara aliyekuwa akielekea Mwanza akizungumza akiwa kituoni hapo leo Desemba 21, 2024 amesema: “Wanagoma kuuza tiketi mapema kwa sababu mawakala wanataka kutengeneza pesa kutokana na hali hii. Nimelazimika kulipa karibu mara mbili ya nauli ili kupata tiketi,” amesema.
Kwa mujibu wa viwango rasmi vya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), nauli ya kawaida ya basi kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ni Sh55,000, huku mabasi ya daraja la kati yakitoza Sh78,000.
Hata hivyo, Mwananchi imebaini kituoni hapo leo kwamba abiria wanalipa kati ya Sh90,000 na Sh170,000, kulingana na daraja la basi.
Mawakala wanaozunguka kituoni hapo huwalenga abiria ambao wamekosa nauli kupitia mfumo wa elektroniki ambao huonyesha basi limejaa. Imeelezwa baadhi ya mawakala hununua tiketi na kuziuza baadaye ili kujipatia fedha za ziada.
“Nimekuwa hapa tangu asubuhi nikijaribu kupata tiketi ya kwenda Arusha,” anasema Michael Komba, ambaye ni mwanafunzi wa chuo na kuongeza:
“Niliposhindwa kuipata, wakala mmoja alinifuata akaniambia anaweza kunipatia kiti ikiwa nitalipa Sh25,000 zaidi. Sikuwa na chaguo lingine.”
Nauli rasmi kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ni Sh30,000 kwa mabasi ya kawaida na Sh42,000 kwa mabasi ya daraja la kati.
Hata hivyo hivi sasa abiria wanalipa kati ya Sh55,000 na Sh70,000 kwa safari hizo.
Wakati wengine wakiona kwamba mawakala wanawasaidia kupata nafasi kwenye mabasi, kwa wengine wanawaona kwamba wao ndiyo chanzo cha matatizo.
Zainabu Hamis, mama aliyekuwa akisafiri kwenda Tarime mkoani Mara akiwa na watoto wake wawili, amesema mawakala wamemsaidia lakini kwa gharama kubwa.
“Nilikuwa nimekata tamaa. Wakala alipata tiketi kwa ajili yangu, lakini nililazimika kulipa Sh120,000 kwa kila kiti badala ya Sh64,000 ya nauli rasmi. Angalau sasa naweza kusafiri,” amesema.
Kwa safari kama za Tarime, abiria hivi sasa wanalipa hadi Sh190,000 kwa mabasi ya daraja la kati, kiwango ambacho ni cha juu ya viwango rasmi vya nauli.
Joseph Matiko, mkulima anayesafiri kwenda Morogoro anasema ameacha kusafiri.
“Mabasi yanawapa kipaumbele wasafiri wa safari za mbali. Nimesubiri kwa saa kadhaa, mawakala waliniambia nilipe mara mbili ya nauli. Siwezi kumudu gharama hiyo,” amesema.
Latra imekiri kuwapo kwa changamoto ikiwataka abiria kusaidia kulitatua.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesema mamlaka inafanya ukaguzi kila siku ili kudhibiti hali hiyo.
“Abiria wana sehemu ya lawama kwa sababu wanakubali kulipa nauli zilizopandishwa na kufanya makubaliano yasiyo rasmi na wamiliki wa mabasi.
“Kwa mfano, tiketi inaweza kugharimu Sh42,000 rasmi, lakini abiria anakubali kulipa Sh45,000, huku kiasi cha ziada hakiorodheshwi. Tunahitaji ushirikiano wao kukomesha hali hii,” amesema.
Amesema Latra pia inatoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu wa kulipa nauli rasmi na kuripoti ukiukwaji wowote unaojitokeza. Hata hivyo, kutekeleza hili wakati wa msimu wa sikukuu ni kazi ngumu.
“Hakuna uhaba wa usafiri. Huduma za reli zimepunguza presha ya mabasi. Tunawasihi abiria kuthibitisha viwango vya nauli kupitia majukwaa yetu na kuhakikisha wanasafiri kwa mabasi yanayozingatia sheria,” amemsema.
Kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya abiria wamekuwa wakizozana na mawakala.
“Ni tatizo la kila mwaka,” amesema George Mkwawa, mfanyabiashara anayeelekea Dodoma.
Anasema: “Safari hii hali inaonekana kuwa mbaya zaidi. Nimetumia saa nyingi nikijadiliana na mawakala. Wana nguvu zote hapa.”
Changamoto ya usafiri imebainisha pengo katika udhibiti wa nauli na uuzaji wa tiketi.
Wakati juhudi za mamlaka za kudhibiti usafiri zikiendelea na kazi, hali halisi katika Kituo cha Magufuli inaonyesha changamoto za usimamizi wa sheria.