Mbowe amkazia Tundu Lissu | Mwananchi

Dar es Salaam. Hatimaye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza rasmi kuitetea nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 20, akisema anawania miaka mitano kwa mara ya mwisho na kufunga rasmi mjadala kuwa huenda angeamua kuachana na suala hilo.

Kwa hatua hiyo, Mbowe sasa atachuana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu na kada wa Chadema, Romanus Mapunda ambao tayari wameshachukua na kurejesha fomu zao.

Hatua ya Mbowe kutangaza kuwania nafasi hiyo imefikiwa baada ya kutimia saa 48 alizotoa Desemba 19, alipofuatwa nyumbani kwake Mikocheni kushawishiwa na kundi  la wanachama kugombea nafasi hiyo, akaomba muda huo kutafakari.

Mbowe aliyechukua fomu ya kugombea leo alasiri Desemba 21, 2024 baada ya kutangaza msimamo huo mbele ya wahariri wa vyombo vya habari, amesema atairejesha kesho Desemba 22 makao makuu ya chama hicho, Mikocheni Dar es Malaam.

Anagombea nafasi hiyo katika uchaguzi unaoonekana kuwa na ushindani mkali baada ya Lissu kutangaza nia ya kugombea Desemba 12, jijini Dar es Salaam, kuchukua fomu na kuirejesha siku chache baadaye.

Lissu aliyeanza kuonyesha msigano na Mbowe kabla hata ya kutangaza nia ya kugombea uenyekiti, amekuwa akikosoa baadhi ya mambo ndani ya chama hicho yakiwamo madai ya kuwepo kwa fedha za rushwa, akitaka kuwe na ukomo wa madaraka na kubadili mfumo wa uchaguzi.

Mnyukano kati ya wawili hao umezalisha kambi mbili za Lissu na Mbowe, baadhi ya makada wametangaza hadharani kuunga mkono pande hizo, zinazozua wasiwasi wa mpasuko.

Akizungumza na wahariri nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam, Mbowe amesema baada ya kutafakari ameamua kujitosa kwa mara nyingine.

“Nimetafakari kwa kina, nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka, lakini siwezi kuondoka katikati ya minyukano iliyopo, kwa hiyo Chadema nipo, nitakuwepo, nitagombea.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kulia)  akipokea fomu ya Uwenyekiti kwa Katibu Mkuu wa Chadema,John Mnyika (kushoto) wakati alipoenda kuchukua fomu katika makao makuu ya chama hicho mikocheni jijini Dar es Salaam leo.Picha na Sunday George

“Mimi na viongozi wenzangu wote wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono naamini tutakutana kwenye mazungumzo ya kukiweka chama chetu sawa,” amesema.

Mbowe aliyewahi kuwa mbunge wa Hai kwa vipindi tofauti, amesema baada ya kutafakari na kubaini kuwa chama hicho kinakabiliwa na mapambano makubwa, ameona hana budi kugombea.

“Nimetafakari, kuna mambo mengi mbele yetu, tunahitaji Katiba, kutaka Katiba unacheza miguu yote. Tuna programu tumeianza ya grass root fortification (ukuzaji wa ngazi za msingi).

“Tuna uchaguzi mbele yetu uko karibu, tuko kwenye vita, kubadilisha makamanda katikati ya vita naona haiwezekani. Anayetaka kugombea tukutane kwenye boksi, tufanye kampeni za kistaarabu,” amesema Mbowe, akiwaasa wagombea katika nafasi mbalimbali waepuke kufitiniana.

Akijibu maswali ya wahariri, Mbowe amesema hamwogopi mpinzani wake Lissu katika nafasi hiyo.

“Hivi nisimwogope Magufuli (hayati Rais John Magufuli) aliyekuwa na majeshi na kila kitu, nimwogope Lissu?

“Lissu ni kiongozi mwenzangu tunaheshimiana tunafanya kazi pamoja. Basi ni kwa sababu mafahali wawili katika zizi moja,” amesema na kuongeza:

“Hata Biblia inasema kura humaliza ubishi, acha tukapambane wanachama waamue.”

Kauli ya Mbowe haina tofauti na aliyotoa Lissu Jumatano Desemba 12, 2024 alipotangaza nia ya kugombea uenyekiti, Dar es Salaam akisema hamhofii Mbowe endapo angetangaza kuwania uenyekiti.

“Sina wasiwasi wowote akigombea hata kidogo, sijawahi kuwa mwenyekiti. Nisipochaguliwa nitakuwa sijawahi kuwa mwenyekiti wa chama, nikichaguliwa nitakuwa mwenyekiti wa nne wa chama hiki,” alisema.

Mbowe akionekana kujibu hoja zilizoibuliwa na Lissu kwa nyakati tofauti, amezungumzia ukomo wa madaraka akisema bado hajachoka.

“Sijui wanatumia kigezo gani kusema Mbowe amechoka, aisee mimi sijachoka wewe. Naweza kufanya mikutano minane kwa siku bila kula. Nionyeshe nani anaweza hivyo,” amesema.

Akiendelea kujenga hoja ya kukaa madarakani kwa muda mrefu, Mbowe ametoa mfano wa kiongozi wa zamani wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zamani Zaire, (Etienne) Tshisekedi akisema alianza kuwa kiongozi wa upinzani tangu enzi za Rais wa zamani wa nchi hiyo, Mobutu Seseseko.

“Tshisekedi amepambana na utawala wa Mobutu, Kabila senior (Laurent), Kabila Junior (Joseph Kabila) kwa miaka 38, mpaka amezeeka na mtoto wake (Felix Tshisekedi) ndio ameshika madaraka,” amesema.

Mbowe akijibu swali aliloulizwa iwapo atahama chama endapo atashindwa katika uchaguzi huo, amesema anawania nafasi hiyo kwa miaka mitano ya mwisho.

“Nihame chama nihamie wapi? Mimi lengo langu ni kutumikia chama kwa miaka mitano ya mwisho. Mtei (Edwin Mtei) alistaafu akiwa na miaka 68, Bob Makani alistaafu akiwa na miaka 67, mimi nina miaka 63,” amesema.

Kuhusu kauli ya Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere aliyewaasa viongozi wasikae madarakani muda mrefu amesema:

“Baba wa Taifa alisema usikae kwenye uongozi hadi upopolewe mawe, hapa hakuna kupopolewa mawe, hapa watu wanakaa kwa kura.

“Kila mmoja apewe haki ya kugombea, anayetaka kugombea tukutane kwa boksi (sanduku la kura), tufanye kampeni za kistaharabu, nimewaambia viongozi wa mabaraza, vijana, wanawake na wazee, kila mmoja afanye kampeni zake akijua ana wajibu wa kukilinda chama,” amesema.

Akijibu hoja ya maridhiano ambayo pia Lissu amekuwa akiizungumia na kusema hayakuwa na faida yoyote, Mbowe ametumia muda mrefu akieleza historia ya kusaka fursa ya kuzungumza tangu wakati wa hayati Magufuli ambaye amesema hakuwajibu barua zao.

Hata hivyo, amesema Magufuli aliwaalika kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika jijini Mwanza Desemba 9, 2019.

Baada ya kifo cha Magufuli Machi 2021, Mbowe amesema waliendelea na juhudi za kusaka maridhiano na Rais Samia Suluhu Hassan, lakini haikufaniki baada ya yeye kukamatwa na kufunguliwa kesi ya ugaidi ambayo alikaa gerezani kwa miezi minane tangu Julai 2021 hadi Machi 2022.

Baada ya kesi hiyo kufutwa, Mbowe alikutana na Rais Samia siku hiyohiyo na baadaye ziliundwa timu za maridhiano kati ya CCM na Chadema.

“Kama tusingeingia kwenye maridhiano, tukaendelea kutunishiana misuli, mikutano isifunguliwe kwa sababu ilizuiwa kwa miaka saba japo ni haki yetu ya kisheria.

“Tusingeingia kwenye maridhiano leo tusingekuwa na uwezo wa kufanya uchaguzi wa chama wa Taifa, leo tusingeweza kushiriki hata uchaguzi wa Serikali za Mitaa, japo walituchakachua, lakini uwepo wetu ulionyesha bado CCM inaiogopa Chadema,” amesema.

Ametaja pia kupatikana kwa ruzuku ya chama hicho ya zaidi ya Sh2 bilioni, ambazo amesema walitenga Sh1.6 bilioni kununua ofisi ya makao makuu ya chama iliyoko Mikocheni kuwa ni mafanikio ya maridhiano.

“Miongoni mwa mafanikio ni viongozi wetu waliokuwa uhamishoni akiwemo Tundu Lissu, Ezekia Wenje na Godbless Lema walirejea nchini.

“Kuna kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, kulikuwa na wafungwa zaidi ya 426, zimesalia kesi mbili. Kama wanafamilia wanajua baba yao amefungwa maisha, leo anarudi nyumbani, ukimwambia maridhiano hayana maana watakuelewa?” amehoji.

Hata hivyo, amesema baadhi ya mambo waliyokuwa wakiyadai hayakupatikana yakiwamo madai ya mabadiliko ya Katiba na mfumo mpya wa uchaguzi.

“Sisi maridhiano yetu na CCM yalikwama, lakini bado tuna matatizo makubwa, bado tunahitaji Katiba mpya, tunahitaji mifumo bora ya uchaguzi,” amesema.

Ameendelea kusisitiza umuhimu wa maridhiano akisema siyo jambo jepesi na si lazima tu wazungumze na CCM bali pia wadau wengine, wakiwamo waandishi wa habari na viongozi wa dini.

“Mchakato wa maridhiano ni give and take (kutoa na kupokea),” amesema.

Akisisitiza suala la maridhiano, Mbowe amewataja viongozi na watu maarufu duniani waliosisitiza umuhimu wa maridhiano, wakiwamo hayati Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini, Rais mstaafu wa Marekani, Barrack Obama, Rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Nelson Mandela, Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan, Rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy na Waziri Mkuu wa zamani wa India Mahatma Ghandi.

Amewataja pia Kansela mstaafu wa Ujerumani, Angela Merkel, Rais wa zamani wa Marekani, Theodore Roosevelt, Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza Winston Churchill na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Akizungumzia madai yaliyowahi kutolewa na Lissu kwamba chama chake kimeahidiwa kupewa vyeo alivyoita nusu mkate, Mbowe amekanusha.

Lissu aliyatoa madai hayo Novemba 12 alipozungumza na waandishi wa habari mjini Singida, akikosoa maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kuhusu hilo, Mbowe amesema: “Madai ya kuahidiwa kinachoitwa serikali ya nusu mkate, madai hayo ni ya uongo. Haijawahi kuwa ajenda ya Chadema kwenye vikao vya kamati kuu kwenye vikao vya kamati ya maridhiano, kwenye hoja 11 tulizopeleka kwa Rais na kwenye maridhiano na hatujawahi kulijadili popote.

“Nashangaa mtu amezuka nalo kwenye jukwaa kwamba Mbowe ameahidiwa atapewa uwaziri mkuu. Uwaziri mkuu unatolewa kama keki au mkate… uwaziri mkuu ni suala la kikatiba.”

Akijibu swali kuhusu mfumo wa fedha, Mbowe amesema yeye kukifadhili Chadema hajaanza leo wala jana, kwa muda mrefu amekuwa akikifadhili.

“Mimi ni mfanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, namiliki mali ndani na nje ya nchi, siyo mbangaizaji na siasa kwangu siyo biashara. Nina historia ya kufanya biashara, nina uwezo wa kutengeneza fedha, sihitaji fedha za wizi wala sihitaji fedha za kukusanya za chama eti kwa mtaji wa Mbowe,” amesema.

Hata hivyo, amesema kila mwanachama ana jukumu la kukifadhili chama hicho.

“Ni kweli kuna wakati nalikikopesha fedha chama hiki, lakini nadhani mara ya mwisho ni miaka mitano iliyopita. Ukikopa kwa nini usirudishe?” amehoji.

Kuhusu madai ya fedha za rushwa, Mbowe amesema Lissu kama Makamu Mwenyekiti pia ni mwenyekiti wa kamati ya maadili, alikuwa na uwezo wa kuitisha kikao na kuwahoji anaodai wamepokea fedha hizo.

“Makamu mwenyekiti wa chama ni msaidizi wa mwenyekiti wa Taifa, wa pili baada ya mwenyekiti, vikao vya kamati kuu anashiriki, watu wanaoweza kuagiza kazi ni mwenyekiti. Hahitaji kusubiri mwenyekiti bali anaweza kumwagiza katibu mkuu amwandalie kikao ayaseme hayo,” amesema.

Related Posts