Mbeya. Mwanaharakati na kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali ameeleza siku 15 za mateso akiwa Polisi, huku akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuteua Tume ya kijaji ya kuchunguza vitendo vya utekeji na kupata mwarobaini wake.
Pia amesema kutokana na demokrasia ya nchi ilivyo kwa sasa anaona mwenye kuwafikisha Chadema katika nchi ya ahadi ni Tundu Lissu, akieleza kuwa Freeman Mbowe alichofanya kinatosha na kitabaki kwenye kumbukumbu.
Nyagali alishikiliwa na Jeshi la Polisi Novemba 22 akiwa na makada wengine wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake Taifa, Mbowe, Mwenyekiti wa Kanda, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wakiwa mkoani Songwe kwa madai ya kufanya kampeni eneo ambalo halikuwa sahihi.
Hata hivyo, viongozi wote na wafuasi wengine waliachiwa, ambapo Nyagali alibaki mikononi mwa Jeshi hilo kwa madai ya mahojiano juu ya tuhuma zinazomkabili ikiwamo matamko na baadaye kusafirishwa mkoani Mbeya na Desemba 7 aliachiwa kwa dhamana.
Akizungumza leo Desemba 21, 2024 jijini hapa, Kada huyo amesema kwa kipindi cha siku 15 alikuwa akiteswa kwa vipigo, huku akipewa maneno na baadhi ya maafisa wa Jeshi kuwa walitaka wampoteze na kilichomsaidia ni kukamatwa mbele ya ushahidi.
Amesema pamoja na mateso hayo, lakini ameumizwa na matukio ya vitendo vya utekeji na kupoteza watu akieleza kuwa Rais Samia ambaye ndiye Amiri wa Jeshi kuteua Tume ya kijaji kuchunguza matukio hayo yanaichafua nchi ndani na nje.
“Sisi wanaharakati tunalaani na kukemea vitendo hivi, Rais akae na vyombo vya ulinzi kupata mwarobaini, tunataka uwajibikaji na bila ubaguzi wa kisiasa kwakuwa mishahara ya Polisi ni kodi zetu wananchi”
“Siku 15 nikiwa Polisi nilifanyiwa vitendo viovu, nia ilikuwa ni kuuawa, nilikaa siku tano sijaonana na ndugu, wala mawakili wangu, kisheria nilipaswa kuchukuliwa onyo ndani ya masaa manne lakini ilikuwa saa 36, hakuna aliyechukuliwa hatua” amesema na kuongeza
“Nawapa pole kijana mwenzangu Abdul Nondo na ACT-Wazalendo kwa ujumla kwa utekwaji na kuumizwa na namuombea arejee tuendeleze gurudumu, lakini Alfonce Lusako kwa kukwepa jaribio la kutekwa, huyu ni rafiki yangu na nina mashaka kutekwa kwake ni kwa ajili yangu” amesema Nyagali.
Kada huyo mkereketwa amesema kuwa katika watu waliochukua fomu za kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, anaona Tundu Lisu anaweza kuongoza kwa sasa.
Amesema hata biblia inaeleza namna nabii Mussa kuwa mkubwa, lakini ilifika hatua Mungu kumpumzisha badala yake kumkabidhi majukumu Joshua hivyo kwa hali ya demokrasia ya sasa nchini, Lisu ndiye mwenye kuwafikisha nchi ya ahadi.
“Freeman Mbowe amefanya makubwa sana kama Mussa na tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wake ila kwa sasa Lisu ndiye mwenye kutupeleka nchi ya ahadi” amesema mwanaharakati huyo.
Ameeleza kuwa kwa sasa Chadema haishindani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali wanapambana na dora, hivyo Lisu ndiye mwenye kuweza kuleta mabadiliko chanya akiwatakia uchaguzi mwema wapiga kura katika uchaguzi huo.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, Nyagali amesema haukuendeshwa kidemokrasia akieleza kuwa katiba ilikiukwa kwa maslahi ya baadhi ya watu na kwamba lazima vitendo hivyo vikomeshwe.
“Mimi ni muumini wa serikali tatu, Muungano, Tanganyika na Zanzibar kwa katiba Jaji Warioba, watu wanajipa madaraka kwa maslahi yao, hatuwezi kuvumilia hali hii”
“Tunaenda kwenye uchaguzi mkuu 2025, tunataka Mageuzi kiutawala na kikatiba, hatutavumilia watu kujipa madaraka na kukiuka Demokrasia iliyowekwa na baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na babu zetu waliopigania nchi” amesema.