Mgambo aliyepoteza mguu tukio la kumkamata mtuhumiwa, aomba msaada

Dodoma. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilingo, Kijiji cha Msagali kilichopo Wilaya ya Mpwapwa, Alex Chikumbi ameomba Serikali na wadau kusaidia matibabu ya mgambo, Masimo Nyau, aliyejeruhiwa katika tukio la mauaji ya polisi wawili na mtuhumiwa wa unyang’anyi, Atanasio Malenda.

Katika tukio hilo lilitokea Desemba 18, 2024, askari D/Koplo Jairo Boniface Kalanda na PC Alfred John walifariki dunia huku D/Koplo Msuka na Nyau wakijeruhiwa na mtuhumiwa huyo wakati wakirushiana risasi.

Majeruhi walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa huku Nyau akihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akizungumza Desemba 20, 2024, Chikumbi amesema katika tukio hilo, mgambo huyo aliumia mikono yote miwili na mguu mmoja wa kushoto.

“Hospitali ya Mpwapwa waliamua kumfunga kwenye mguu hadi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo iliwabidi kumpeleka katika X-Ray wakajua bora kuukata kwa kuwa utamsababishia mguu kuoza,” amesema.

Amesema walimfanyia upasuaji usiku wa juzi kuamkia jana na kumkata mguu huku wakimshona mikono iliyokuwa imekatwa na mapanga.

“Namshukuru Mungu anaendelea vizuri, tofauti na tulivyomleta hapa,” amesema.

Chikumbi anasema hadi kufikia jana alikuwa ametumia Sh305,000 kwa ajili ya matibabu ya mgambo huyo kutoka mfukoni mwake.

“Hadi hivi sasa sina fedha za kumsaidia kwenye matibabu. Naiomba Serikali na watu wenye mapenzi mema wamsaidie huyu askari jamii aweze kutibiwa,” amesema.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema askari hao waliuawa kwenye mapambano ya risasi na mtuhumiwa aliyedaiwa kumjeruhi na kumpora mtu Sh2 milioni.

Katabazi amesema mtuhumiwa Malenda alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo.

D/Koplo Jairo Boniface Kalanda alisafirishwa kwenda Rukwa huku PC Alfred John akisafirishwa kwenda Sirari, Tarime mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.

Kabla ya kusafirishwa, miili hiyo iliagwa jana wilayani Mpwapwa ambapo Kamishna wa Utawala na Raslimali Watu, Tatu Jumbe alilaani tukio hilo na kuhimiza jamii kutoacha kufichua tabia zisizo za kawaida miongoni mwao.

“Nawasisitiza askari wetu kuendelea kuwa waangalifu na kutumia weledi wenu mnapokuwa kazini. IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) amenituma niwaambie msikate tamaa na endeleeni kutimiza wajibu wenu wenu kwa haki,” amesema.

Related Posts