Dar es Salaam. Mtoto anapaswa kulala katika mazingira mazuri na salama ili kusaidia ukuaji wake wa kimwili, kiakili na kihisia.
Kutokana na umuhimu wa usingizi kwa mtoto, anapaswa kulala eneo lenye joto la wastani mahali pasipo na mwanga mkali au kelele.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imeweka msingi wa kisheria kwa ajili ya ulinzi, malezi, na maendeleo ya watoto nchini. Sheria hii inatambua haki na wajibu wa mtoto, wazazi na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha masilahi ya mtoto yanapewa kipaumbele.
Licha ya uwepo wa sheria, baadhi ya wazazi na walezi wanapokwenda kwenye mikesha iwe ya kidini au hata ya sherehe huambatana na watoto kuanzia umri wa chini ya miaka mitano hivyo kuwaweka katika hatari za usalama wao.
Wakili Neema Sanga akizungumza na Mwananchi hivi karibuni amesema kwa kutokujali sheria, watoto wamejikuta kwenye hatari, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwajibika kuhakikisha wanakuwa katika mazingira salama wakati wote.
“Unakutana na mtu ana watoto barabarani saa 6:00 usiku, ukimuuliza anasema wametoka kwenye sherehe au mkesha wa kidini kweli tunahitaji watoto wajifunze jambo lakini tuangalie na usalama wao,” amesema Neema.
Mwanasaikolojia, Anna Mshana amesema kuwapeleka watoto kwenye mikesha kunaweza kuwa na madhara kwa afya yao ya akili na mwili.
“Watoto wanahitaji muda wa kutosha wa kulala ili kukuza akili na miili yao, kukosa usingizi wa kutosha kunaweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia kama vile msongo wa mawazo na kupungua kwa uwezo wa kufikiri,” amesema.
Amesema tabia ya kukesha mara kwa mara inaweza kuathiri uhusiano wa mtoto na wazazi, walimu na wenzake kwani mtoto wenye uchovu mwingi hawezi kushirikiana vyema na watu au akawa na tabia za kujitenga.
Mbali ya mikesha ya aina hiyo, anasema mazoea kama vile kuangalia runinga na kutumia simu usiku yanaweza kuongeza hali ya kukesha na huathiri uwezo wa mtoto kufuata ratiba za kawaida za maisha.
Anna anasema ikiwa mtoto anaonyesha dalili za wasiwasi, huzuni au matatizo ya tabia kutokana na kukosa usingizi ni vyema kushauriana na mtaalamu wa saikolojia.
“Usingizi wa kutosha ni muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili za mtoto, kukesha kunapaswa kuepukwa kadri inavyowezekana,” amesema.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwaacha watoto waendelee kuwa macho usiku kucha kunaweza kudhoofisha kinga yao ya mwili na kuwafanya wawe rahisi kushambuliwa na magonjwa.
Dk James Mwangaza wa Hospitali ya Tabata, jijini Dar es Salaam anasema ukosefu wa usingizi wa kutosha huathiri mfumo wa kinga na kufanya watoto kuwa hatarini zaidi kupata maambukizi na magonjwa.
“Usingizi wa kutosha ni muhimu kwa ukuaji wa mwili, kwani homoni za ukuaji hutolewa kwa wingi wakati wa usingizi wa kina, watoto wanaokosa usingizi wanaweza kupata matatizo ya ukuaji,” amesema.
Anasema kukosa usingizi kunapunguza uwezo wa kuzingatia, kukumbuka na kujifunza, hivyo kunaweza kuwa chanzo cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtoto shuleni, pia kuwa na hasira, mabadilio ya hisia na ukaidi unaosababishwa na uchovu.
“Kukesha mara kwa mara kutasababisha matatizo ya muda mrefu ya akili, kama vile wasiwasi na mfadhaiko, kupoteza mwelekeo pia kupata shinikizo la damu ambalo ni hatari kwa watoto,” amesema.
Mwenyekiti wa Juimya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum amesema hakuna ubaya kwa watoto kukesha katika shughuli za kidini ikiwa kuna ulinzi na uangalizi wa kutosha na haitakuwa siku ya kuamkia shuleni.
“Inapendeza na haina shida kipindi ambacho hakuna shule lakini unapomfanya mtoto akeshe halafu siku inayofuata anakwenda shule hiyo haifai kwa sababu utakuwa unamuathiri kwa namna moja au nyingine anapokwenda shuleni,” amesema.
Amesema mtoto hawezi kukesha moja kwa moja lazima atalala na kwamba wanaposhirikishwa ni katika kuwajenga kiimani.
Sheikh Alhad amesema watoto wanapojisikia kulala walazwe sehemu salama ili wapumzike kwani kwenda nao ni kuwapa malezi ya wazee wao kwenye masuala ya kidini.
Mchungaji wa Kanisa la Upendo lililopo Ukonga, Emmanuel Kambi anasema mikesha isiwe adhabu kwa watoto kwani hata wakiwepo wanavyojifunza ni vichache.
“Mikesha ya kidini inalenga kuwajenga watoto kiimani, lakini wazazi wanapaswa kuhakikisha wanakuwa salama na wanapumzika vya kutosha baada ya mikesha hiyo,” amesema.
Jane Mbwana, mkazi wa Kinondoni amesema wanawapeleka watoto kwenye mikesha kwa sababu ya kukosa mtu wa kuwaachia.
“Hakuna mtu wa kubaki na watoto nyumbani, hivyo ni rahisi kuwachukua kwenda nao kwenye mkesha,” anasema Jane.
“Siwezi kumpeleka mwanangu kwenye mkesha. Watoto wanahitaji usingizi wa usiku ili wakue vizuri,” anasema Bakari Hamisi, mazazi na mkazi wa Temeke.
Mkazi wa Mbagala, Hasnat Salum anasema mazingira ya mikesha mara nyingine si salama kwa watoto, kwani wapo wanaopotea au hata kufanyiwa vitendo vya ukatili.
“Nilijuta kumpeleka mwanangu kwenye shughuli ambayo ilifanyika usiku, wakati wa kutoa zawadi kwenye sherehe nikamwambia mtoto kaa nakuja kumbe katoka nilihangaika nimekuja kumpata saa 8:00 usiku alikuwa anarudi nyumbani mwenyewe akiwa amechoka,” anasema.
Mwanasaikolojia Anna anasema kuwapeleka watoto kwenye mikesha ni suala linalohitaji umakini mkubwa kutoka kwa wazazi na walezi. Ingawa kuna faida ya kuwajenga watoto kiimani na kijamii, madhara yake yanaweza kuwa makubwa ikiwa hakutakuwa na mipaka na usimamizi wa karibu.
Wazazi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye kuzingatia afya yao ya akili, mwili na haki zao za msingi.
“Mkesha wa watoto unaweza kufanyika mapema kabla ya usiku wa manani na wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanalala mapema,” anasema.