Dar es Salaam. Mlinzi, Abdallah Mtema (52) ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, namna alivyolinda shamba lenye ukubwa wa ekari 20, mali ya aliyekuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania, John Sepeku kwa muda wa miaka 36.
Mtema ambaye ni mkazi wa Buza, Wilaya ya Temeke ametoa ushaidi wake leo, mahakamani hapo katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Bernado, ni mtoto wa marehemu John Sepeku, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.
Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke, kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, kama Askofu wa Mkuu wa kwanza kanisa hilo.
Bernardo katika kesi hiyo, amedai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia, anaomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Haya hivyo, mdaiwa wa tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.
Mtema amedai mbele ya Jaji Arafa Msafiri kuwa baba yake alikuwa baba yake mzazi alikuwa mwajiriwa wa kanisa hilo kama mtunza bustani.
“Mimi niliajiriwa kama mlinzi wa eneo hili na mtoto wa Sepeku aitwaye Titus, ambaye kwa sasa ni marehemu, kazi hii ya ulinzi nimeifanya kwa muda wa miaka 36 mpaka sasa,” amedai Mtema.
Wakili Deogratias Butawantemi, alimuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake ambapo amedai kuwa Agosti 7, 2024 aliwasilisha mahakamani hapo ushahidi wa maandishi kuhusiana na kesi hiyo.
Amedai kwa muda wote huo, hakukuwahi kuwa na mgogoro wa aina yoyote, lakini miaka ya hivi karibuni kulitokea simtofahamu kuhusiana na shamba hilo kumegwa na kujengwa kiwanda.
Amedai kuwa mwaka 1988, aliajiriwa na Titus ambaye ni mtoto wa Sepeku kulinda shamba hilo.
Hata hivyo, alipoulizwa na wakili wa mjibu maombi, Dennis Malamba iwapo ametoa uthibitisho wowote mahakamani hapo kuonyesha kuwa aliajiriwa na mtoto huyo, Mtema alidai kuwa hajatoa uthibitisho wowote kwa kuwa aliambiwa kwa mdomo.
Pia, alipoulizwa na Wakili Malamba iwapo ametoa karatasi au nyaraka yoyote mahakamani hapo kuonyesha kuwa eneo hilo alilokuwa analinda ni mali ya Sepeku, shahidi huyo alidai kuwa hajatoa uthibitisho wowote kwa sababu aliambiwa kwa mdomo alinde eneo hilo.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, aliomba mahakama iupokee na uwe sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupingwa na Mahakama.
Wakati huohuo, shahidi wa saba wa upande wa Sepeku, Edward Lwambano (62) amedai namna alivyoteuliwa kuwa msimamizi wa kugawa shamba kati ya familia ya Sepeku na Dayosisi ya Dar es Salalam.
Amedai kuwa yeye alikuwa msimamizi wa shamba hilo tangu alipopewa na Askofu Sepeku.
Lwambano amedai kuwa aliteuliwa na bosi wake, ambaye ni askofu mstaafu wa kanisa hilo, Valentino Mokiwa kwenda kusimamia upimaji wa shamba hilo na kuweka alama za mipaka zoezi ambalo lilikuwa linafanywa na maofisa ardhi wa Manispaa ya Temeke.
“Baada ya kuteuliwa na bosi wangu (Askofu Mokiwa), niliambatana na maofisa wa Manispaa ya Temeke na kwenda kupima lile eneo na kuweka alama za mipaka,” amedai Lwambano.
Amebainisha kuwa amekuwa msimamizi wa shamba hilo kwa zaidi ya miaka 24 na ni mwajiriwa wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
“Awali, nilikuwa msimamizi wa bustani tu ya shamba Buza, lakini baadaye nikawa msimamizi wa shamba zima la marehemu Sepeku,” amedai na kuongeza:
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba alimuuliza maswali ya dodoso Lwambano na haya ni baadhi ya maswali aliyohojiwa.
Wakili: Wewe katika ushahidi wako hujatoa kitambulisho kinachoonyesha wewe ni mtunza bustani, ni sahihi?
Wakili: Mtunza bustani na msimamizi wa shamba ni kazi moja? Au ni kazi mbili tofauti?
Shahidi: Kazi mbili tofauti.
Wakili: Barua ya mwajiri aliyekuajiri, umeitoa hapa mahakamani?
Wakili: Aya ya 5 ya ushahidi wao uliyoutoa mahakamani hapa, ulisema ulichaguliwa kama msimamizi wa kugawa shamba kati ya familia ya Sepeku na Dayosisi ya Dar es Salaam, ni sahihi?
Wakili: Na kwa sababu umesema huna barua wala kitambulisho cha kuonyesha kuwa ulipewa kazi hiyo, mahakama itakuaminije?
Shahidi: Mwaka 2009 ndio nilipewa kitambulisho.
Wakili: Kuna nyaraka yoyote uliyopewa kuonyesha kuwa hilo shamba ni la Askofu Sepeku?
Shahidi: Hapana, bali niliambiwa kwa mdomo na maneno.
Wakili: Sasa huoni kama ulilofanya lilikuwa ni kosa?
Shahidi: Sio kosa kwa sababu mwajiri wangu alinituma niende.
Wakili: Shahidi umesema baada ya kugawa eneo hilo, ulienda Manispaa ya Temeke?
Shahidi: Haikuwa hivyo, bosi wangu alinituma niende kusimamia upimaji wa eneo hilo lililokuwa linapimwa na maofisa wa ardhi wa Manispaa ya Temeke.
Wakili: Hayo melezo ya bosi wako kukutuma kusimamia upimaji wa eneo hilo, umeyatoa mahakamani kama kielelezo?
Shahidi: Mimi aliniambia kwa mdomo na sio kwa maandishi.
Wakili: Je ,umeleta uthibitisho wowote mahakamani hapa kuonyesha kuwa bosi wako alikutuma kuweka alama za mipaka ya shamba hilo?
Shahidi: Mimi nilisimamia upimaji na kupeleka taarifa kwa bosi wangu.
Wakili: Vielelezo vya upimaji na kuweka alama za mipaka, umevileta hapa mahakamani?
Wakili: Wakati unafanya hayo yote, uliambatana na ofisa yoyote wa kanisa?
Shahidi: Bosi wangu( Mokiwa) ndio aliniteua mimi na wala sikuambatana na mtu yeyote yule.
Wakili: Umesema ulienda pekee yako, pamoja na maofisa wa ardhi wa Manispaa ya Temeke?
Wakili: Wewe una utaalamu wowote wa masuala ya ardhi?
Shahidi: Mimi sina utaalamu wowote wa masuala ya ardhi.
Wakili: Shahidi, unaona ulikuwa na uhalali wa kupima ardhi?
Shahidi: Bosi wangu ndio aliyeniteua kwenda kusimamia upimaji wa ardhi kule Buza Mtoni pamoja na wataalamu wa ardhi kutoka Manispaa ya Temeke.
Baada ya kumaliza kuhojiwa, Jaji Msafiri ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 25 na Februari 26, 2025, saa 5:00 itakapoendelea.
Tayari mashahidi saba wameshatoa ushahidi wao katika kesi hiyo.