Mnyukano Wenje, Lissu washika kasi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje amekanusha tuhuma za kushiriki kuwahonga wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, akijibu hoja iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu, aliyemtaja kuwa ndiye alimpeleka mtu kwake kumhonga fedha.

Lissu aliibua tuhuma hizo Mei, 2024 katika mahojiano yaliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii, akieleza mmoja wa viongozi wa chama hicho ndiye aliyempeleka mtu huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu hajafikiwa na Mwananchi kujibu tuhuma hizo) nyumbani kwake.

Pia amewahi kueleza huyo ndiye anayekula fedha za mtu huyo na anashirikiana naye kuwahonga wajumbe wa kamati kuu ya Chadema.

Lissu alirejea kauli hiyo Desemba 18, aliporejesha fomu ya uenyekiti, aliposema aliyempeleka mtu huyo nyumbani kwake kumhonga anawania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, ambaye imefahamika ni Wenje.

Wakati Wenje akikana tuhuma hizo na kutoa maelezo yake, Lissu amemjibu akisema ndani yake kuna uongo, nusu ukweli na ukweli.

Wenje katika video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana Desemba 20, amekana tuhuma hizo akieleza namna alivyokutana na anayetahwa mhongaji (anamtaja) hadi kumkutanisha na Lissu.

Amesema kwa mara ya kwanza alikutana na mtu huyo Oktoba, 2023.

“Katika utambulisho kuna mtu alivaa kanzu, nikatambulishwa (anamtaja jina na mzazi wake), basi tukasalimiana,” amesema na kwamba, baada ya salamu walibadilishana namba za simu.

Wenje amesema alimuuliza mtu huyo ni kwa nini Serikali haitaki kumlipia Lissu fedha zake za matibabu.

“Kumbuka Lissu alikuwa anaidai Serikali fedha zake za matibabu, alipokutana na Rais Samia Ubelgiji moja ya madai yake ilikuwa ni malipo ya fedha zake za matibabu,” amesema.

Amesema mtu huyo alijibu zimeshalipwa, wakabishana hadi alipoamua kumpigia Lissu kuthibitisha iwapo amelipwa au vinginevyo.

“Nikampigia Makamu hapa nipo na mtu nikamweleza ni nani, nimemuuliza kwa nini hawataki kukulipa fedha zako, akasema umeshalipwa ni kweli?

“Nami nilikuwa nafanya hivyo kwa sababu nilikuwa na masilahi na hizo fedha kwani nilitoa za kwangu kusaidia mambo mengi kwa timu ya Lissu,” amesema.

Kwa mujibu wa Wenje, siku moja walisafiri Peter Msigwa na John Heche kwenda Arusha ambako Lissu alikuwa na kesi, hivyo alipaswa kuripoti.

Amesema baada ya kukutana na Lissu kesho yake wakaanza safari ya kurejea Dar es Salaam tayari kupanga kikao na mtu huyo kuhusu malipo ya fedha za matibabu.

Usiku wake, amesema Lissu aliugua tumbo akashindwa kwenda kwenye kikao walichopanga katika moja ya hoteli walizokubaliana.

Kutokana na mazingira hayo, Wenje amesema Lissu aliomba kwa hali aliyokuwa nayo kikao kisifanyike hotelini kwa kuwa asingeweza kuhudhuria, badala yake kifanyike nyumbani kwake.

Wenje amesema safari yao na mtu huyo kwenda kwa Lissu ilitokana na mwaliko walioupata na ilikuwa Novemba, 2023.

“Tulipofika Lissu akasema bwana napaswa nilipwe hizi fedha kwa sababu ni zangu, maana Serikali ilipaswa kunigharimia matibabu kwa mujibu wa Sheria,” amesema.

Amesema Lissu aliingia ndani akatoka na mfuko uliokuwa na nyaraka za malipo na mgeni wao aliomba pia atumiwe kwa email (barua pepe).

Katika mazingira hayo, amesema anashangaa kumsikia Lissu akidai mara ya kwanza alimfukuza mgani hiyo alipokwenda kwake, ilhali alimpa nyaraka na kumtumia kwa email.

Amesema uamuzi wa kumtumia mtu huyo kwa ajili ya malipo ya Lissu ilhali si mtumishi wa umma ni kwamba, alijua ni mtu mwenye ushawishi katika kulifanikisha hilo.

Wenje amehoji kama amempeleka kuwahonga wajumbe wa kamati kuu Chadema, mbona kati yao hakuna anayeisifia Serikali.

Wenye amesema Lissu amewahi kuwatuhumu wengi kwa madai yasiyo ya kweli, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyedai alihongwa magari mawili na Serikali.

Amesema alipofuatilia na kwenda kumuuliza Mbowe, alimkabidhi uthibitisho wa nyaraka kwamba magari hayo yalinunuliwa kwenye mnada Sinza, Dar es Salaam.

Wenje amemtuhumu Lissu kuwa mwanasiasa anayejaribu kumchafua kila mmoja, akifananisha kitendo hicho na alichosema, fisi akitaka kuwala watoto wake anawasingizia wananuka kama mbuzi.

Amesema hata tuhuma dhidi yake zingekuwa na ukweli, chama hicho kisingemvumilia, kingemfukuza kama kilivyowahi kufanya kwa wengine.

Hata hivyo, amesema haina maana kwamba Lissu ni mtu mbaya isipokuwa amebadilika kwa sasa.

Amesema hata uamuzi wake wa kuwania uenyekiti wa chama hicho, haupaswi kupingwa kwa kuwa ndiyo demokrasia.

Amesema ikitokea uchaguzi ukafanyika na ukamalizika Chadema ikiwa na umoja, itakuwa historia nzuri kwa nchi na chama husika.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 21, Lissu amesema kati ya maelezo ya Wenje, kuna uongo na ukweli ndani yake.

“Kuna ambayo amesema ya uongo kabisa, kuna aliyoyasema ya nusu ukweli, kuna aliyoyasema ya ukweli… Kwa mfano amekubali amemleta (anamtaja) nyumbani kwangu, hivyo hakuna ubishi, alimleta nyumbani,” amesema.

Lissu amesema si kweli alikuwa yeye na changamoto ya tumbo, bali alikataa kikao hicho kufanyika hoteli iliyopangwa maeneo ya Masaki.

Amesema alimweleza Wenje kama (anamtaja) anataka kumuona, basi amfuate nyumbani kwake Tegeta Azania, wilayani Kinondoni.

“Siyo kweli alimleta ili tuzungumzie habari za malipo yangu, ni uongo, ukweli alimleta ili anipe hela, kama alivyopewa yeye… akaniambia nichukue fedha ili ninunue gari niache kuhangaika. Nikamwambia anataka tuonane wapi, akajibu Masaki, nikamwambia huko siendi, kama anataka kuniona aje nyumbani kwangu,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, mchakato wa kukutanishwa na mtu huyo ulianza Agosti, siyo Oktoba kama alivyoeleza Wenje.

Lissu amesema kilichomfanya Wenje kumpleka mtu huyo kwake ni baada ya yeye kumshambulia kupitia mikutano ya hadhara aliyoifanya kwa nyakati tofauti Mabibo na Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

“Nilimsema baada ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ‘kutwiti’ kuwa amepokea ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na mtu huyo kuzungumzia masuala ya nishati, nikamshambulia sana. Toka mwezi huo walinifuatilia sana hadi Novemba 2023 nikaonana nao,” amesema.

Lissu amesema siyo kweli kwamba walisafiri na Wenje kutoka Machame, Moshi hadi Dar es Salaam, bali yeye akiwa na mlinzi wake mmoja walipanda ndege.

“Anasema nilikuwa na shida ya tumbo! ipo hivi, nilikuwa nje ya nchi, nilipokewa Nairobi na walinzi wangu. Tukaja Arusha hadi Machame. Wakati wa kurudi Dar es Salaam, kwa vile nilikuwa mgonjwa nilisafiri kwa ndege usiku, sikusafiri na Wenje kwenye gari lake.

“Anachanganya mambo tu, ni kweli nilikuwa naumwa lakini sikusafiri naye. Baada ya hiyo safari kesho yake akamleta (anamtaja) kwangu. Nilimwambia kama unataka kunisaidia anilipwe fedha zangu maana siyo msaada bali ni haki yangu,” amesema.

Amesema aliambiwa hajapeleka nyaraka, naye akamjibu amempelekea mara mbili ila hazijafanyiwa kazi.

Lissu amekiri kumpa nakala nyaraka moja iliyobaki lakini akamweleza hakuna kiambatanisho, isipokuwa kimoja kipo kwenye barua pepe.

“Nikamuomba barua pepe ili nimtumie kukamilisha nyaraka hizo. Hii habari ya kumpa nyaraka zangu kwani ina ugomvi, mbona nimeshaisema hadharani? Mbona Wenje anaisema as if (kana kwamba) ni kitu kigeni.

“Angalau tutafika kwa sababu kuna vitu amevisema na kukiri kwamba alimleta (anamtaja) nyumbani,” amesema.

Kuhusu kuomba msamaha ndani ya kamati kuu, Lissu amesema alianza kuzungumza masuala ya rushwa katika chaguzi ndani ya vikao hivyo, lakini yalipuuzwa, ndipo akazungumza kwa mara nyingine mkoani Iringa.

“Niliandika ujumbe na barua pepe kwa wajumbe wote wa kamati kuu wiki mbili kabla sijakwenda Iringa. Baada ya kuzungumza Iringa, nilitwa kwenye kikao cha kamati kuu ili nijieleze na kuthibitisha, walileta na kamera kwa ajili ya kurekodi.

“Niliwasihi sana wasirekodi kwa sababu maneno ambayo ningeyasema yalikuwa mabaya, lakini wote walikataa, wakijua kwamba wamenibana sina ushahidi, nilizungumza kwa saa tatu, na kujata watu niliokuwa na taarifa zao za kupokea fedha ambao wengine walikuwamo ndani ya kikao,” amesema.

Amesema suala kubwa lililoibuka ni hatua ya yeye kuzungumzia suala hilo nje, wakimtuhumu anakichafua chama.

Alisema hoja ya kuthibitisha tuhuma ilibadilishwa ikaja ya kukichafua chama na siku hiyo kikao hakikumalizika.

“Kesho yake mwenyekiti (Mbowe) alikuja analalamika nimemtukana na kumdhalilisha, akasusia kikao na kurudi ofisini kwake, wajumbe wakaniambia nikamuombe msamaha. Nikamfuata kumuomba msamaha kwa maneno yangu, lakini sikuomba msamaha kwa sababu nimeongea uongo.

“Ndipo akaja kwenye kikao nikamwambia mwenyekiti kama maneno yangu yamekuudhi, naomba msamaha, haikuwa habari ya kuomba msamaha kwamba nimeongea uongo, niliomba msamaha kwa sababu alisusa kikao, sasa hiki kinaendana na alichokisema Wenje,” amehoji.

Related Posts