Rombo. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitowo kilichopo katika Kijiji cha Mengwe Juu, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Agustina Lyakurwa amejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo kwa takribani siku 25 baada ya kuchaguliwa Novemba 27, 2024.
Hicho ndicho kitongoji pekee kilichochukuliwa na upinzani katika kijiji hicho kati ya vitongoji sita vilivyopo kwenye kijiji hicho, huku vitongoji vingine vitano vikichukuliwa na CCM kwenye uchaguzi uliopita.
Akizungumzia uamuzi wake huo leo Desemba 21, 2024, Lyakurwa ametaja sababu za kutimkia CCM akisema amejiona mpweke kuwa peke yake, hivyo ameamua kuungana na chama hicho ili wafanye kazi kwa pamoja.
“Niligombea Chadema, wananchi waliniamini wakanipigia kura na kunichagua, nikapata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa kitongoji hiki. Sasa nimeona kukaa mwenyewe haitawezekana, bora nijiunge na wenzangu wa CCM tufanye kazi pamoja,” ameeleza Lyakurwa.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Katibu wa Chadema Wilaya ya Rombo, Emmanuel Tarimo amesema amezisikia taarifa hizo na kwamba wanaheshimu uamuzi wake.
“Taarifa nimezisikia lakini zipo juu kwa juu, nilimpigia simu sijampata hewani, hili jambo limetusikitisha sana kwa sababu ni mtu ambaye tulimsimamisha, tukampambania, akashinda, kama ameamua kwenda upande mwingine, ni haki yake ya kidemokrasia, pia, katiba inamruhusu mtu kuhama kwenda upande wa pili,” amesema Tarimo.
Ameongeza: “Kwetu sisi ni pigo na tunaheshimu uamuzi wake kama yeye. Kama ameamua yeye mwenyewe basi, tutaendelea na mapambano kama kawaida,” amesema Tarimo.
Akizungumza wakati akimpokea kwenye chama, Katibu wa CCM, Wilaya ya Rombo, Mary Sule amempongeza mwenyekiti huyo na kwamba wao kama chama wako tayari kufanya naye kazi na hata akitaka kugombea katika nafasi hiyo, watampa nafasi.
“Katika vitongoji saba vya Kijiji cha Mengwe Juu, tulichukua vitongoji sita, kimoja kilichukuliwa na upande wa upinzani, hivyo tulishinda asilimia 99 ya vitongoji vyote, hivyo tunampongeza kwa uamuzi mzuri aliouchukua kuhakikisha anaungana na CCM kuleta maendeleo katika kijiji hiki,” amesema.
Sule amesema kwa sasa wanasubiri maelekezo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi atakapotangaza nafasi iliyoachwa wazi.