Mbozi. Watu wanane wamejeruhiwa katika ajali ya moto uliotokea katika duka la kuhifadhia na kuuzia vinywaji vya jumla na rejareja, baada ya duka hilo kuwaka moto unaodaiwa kusababishwa na mafuta ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa ndani.
Majeruhi hao waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyopo Mkoa wa Songwe, walikuwa wakiangalia mpira katika duka hilo, lakini moto ulipozuka walitoka na kujaribu kuuzima, hata hivyo waliungua wakati wakijaribu kuuzima moto huo.
Ajali hiyo ilitokea Desemba 19, 2024 katika Kijiji cha Ihowa kilichopo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kwenye nyumba iliyokuwa ikitumika pia kama duka la kuuzia vinywaji vya jumla na rejareja (depo).
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shabani limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia Patrick Mwachimbona kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo na pindi upelelezi utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya shughuli za kuuza wa nishati ya mafuta (dizeli na petroli) kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli kwenye vyanzo vya moto kama kwenye maghala au sehemu ambayo yanahifadhiwa mafuta na gesi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imebainisha kwamba upelelezi wa awali ulibaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kitendo cha Rose Charles ambaye ni mke wa mmiliki wa kibanda hicho, ambaye alikuwa akifanya shughuli za kuwahudumia wateja huku akiendelea kupika ndani ya kibanda hicho na ndani ya kibanda kulikuwa kumehifadhiwa mafuta aina ya petroli ndipo moto ulilipuka.
Jeshi hilo limeeleza kwamba waliposikia mlipuko huo, watu waliokuwa wanaangalia mechi, walikuja kwa ajili ya msaada wa kuokoa na katika harakati za uokoaji na wao waliungua na moto huo.
Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa kijiji hicho, Spidi Mbembela amesema majeruhi wengi wa ajali hiyo ni wale waliofika eneo la tukio kwa lengo la kuokoa baada ya moto kulipuka ndani ya duka hilo.
“Majeruhi wengi ni wanaume waliokuwa jirani na eneo la tukio wakiangalia mechi ya mpira wa miguu uliokuwa ukiendelea, ambapo walifika kwa ajili ya kuokoa na kujikuta wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitali,” amesema Mbembela.
Kwa upande wake, mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, Dk John Mwanyingili amekiri kupokea majeruhi hao wanane ambao walifanyiwa uchunguzi wa awali.
Amesema majeruhi hao walifikishwa hospitalini hapo saa 12 jioni, Desemba 19, 2024 na kupokelewa katika kitengo cha dharura, ambapo walifanyiwa uchunguzi wa awali na kuanza kupatiwa matibabu.
Amewataja majeruhi hao kuwa ni Rose ambaye ndiye mama mwenye nyumba iliyoshika moto, wengine ni Isambi Mwene (34), Maneno Julius (49), Fadhiri Festo (32), Lewis Patrick (19), Frank Msyan (40) na Matokeo Islam (51).