Polisi aliyeua kwa AK-47 afungwa kifungo cha nje

Tarime. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Musoma imemhukumu kifungo cha nje cha miezi 12 aliyekuwa Konstebo wa Polisi, Kululutela Nyakai kwa kumuua kwa risasi Ng’ondi Masiaga, aliyetuhumiwa kufanya biashara ya magendo.

Masiaga aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita AK-47 Machi 31, 2023 katika kijiji cha Kubiterere wilayani Tarime wakati Nyakai na mwenzake wakifanya doria mpaka mwa Tanzania na Kenya.

Awali alishitakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia lakini baada ya mahakama chini ya Jaji Kamazima Kafanabo kusikiliza ushahidi wa Jamhuri na utetezi, ilimtia hatiani kwa kosa la kuua pasipo kukusudia.

Jaji amesema adhabu ya juu ya kuua bila kukusudia ni kifungo cha maisha jela, lakini kwa mazingira ya kosa lilivyotendeka, umri wake, utegemezi na muda aliokaa gerezani, anamhukumu kifungo cha nje cha miezi 12.

Ilidaiwa na Jamhuri kuwa siku ya tukio, mshitakiwa na mwenzake, J.3525 Kostebo Charles wakishirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walikuwa doria mpakani Sirari kudhibiti uingizaji bidhaa za magendo kutoka Kenya kuja Tanzania.

Katika doria hiyo, askari polisi hao kutoka kituo cha Sirari walikabidhiwa bunduki AK-47 kila mmoja.

Ilidaiwa polisi hao walikwenda mpakani kuanza doria kabla ya maofisa wa TRA kinyume cha maelekezo na walikamata watu waliokuwa wakivusha saruji kwa pikipiki.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Masiaga aliyekuwa akitumia pikipiki aina ya Honlg namba MC577 CZF.

Wakati wa ukamataji kulitokea mtafaruku, hivyo Koplo Nyakai alizuia pikipiki wakati huohuo Masiaga akilazimisha aondoke nayo.

Katika hali hiyo, Koplo Nyakai alifyatua risasi mbili zilizompata Masiaga kwenye paja na kinena, hivyo kumsababishia majeraha yaliyovuja damu nyingi kabla ya kupelekwa hospitali.

Muda ulipita kabla ya mashuhuda wa tukio hilo kumchukua Masiaga kumpeleka hospitali ya Tarime ambako alifariki dunia akipatiwa matibabu. Nyakai alikamatwa siku hiyohiyo.

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Muheche Masiaga ndugu wa marehemu ameeleza siku ya tukio saa 2:00 asubuhi, yeye na kaka yake walikwenda upande wa Kenya kununua saruji ili kuuingiza Tanzania kwa magendo kupitia Kijiji cha Komwamu.

Amedai walipokuwa wakitaka kurudi, watu waliokuwa upande wa Kenya waliwatonya kuhusu kuwapo polisi njiani.

Amedai ulikuwa utamaduni wa kuwapa polisi angalau Sh2,000 wanapokutana nao, njiani alikutana na askari aliwapa Sh2,000 wakamruhusu kupita pamoja na pikipiki ikiwa na mifuko ya saruji.

Hata hivyo, akiwa mbele alibaini polisi hawakumruhusu ndugu yake kupita, hivyo alisimama kufuatilia ndipo alipomsikia mshitakiwa akimwambia ndugu yake alikiuka utamaduni waliojiwekea, hivyo akamwambia bila kuwapatia Sh300,000 wasingemwachia.

Amedai alipoyasikia hayo aliegesha pikipiki yake jirani na nyumba akarudi eneo alipokuwa ndugu yake akawasikia polisi wakisisitiza wapewe Sh300,000 vinginevyo watamkabidhi kwa maofisa wa TRA.

Konstebo Nyakai anadaiwa na shahidi kusukuma mzigo wa saruji ukaanguka na kwa kuwa ulikuwa mzito, Masiaga naye alianguka.

Amedai Masiaga aliacha pikipiki na kumfuata Nyakai akamweleza amekuwa akitoa fedha, ndipo mshitakiwa alinyanyua bunduki akiwa na hasira na kuweka risasi kwenye chemba.

Kwa mujibu wa ushahidi, askari mwingine aliyekuwa na Nyakai alionyesha kushangazwa na kitendo hicho na kumhoji kwa nini anafanya hivyo, lakini majibizano kati ya mshitakiwa na Masiaga yaliendelea.

Amedai mshitakiwa alirudi nyuma, akamlenga Masiaga na kufyatua risasi iliyompiga sehemu za siri akaanguka. Ameeleza alikwenda kumsaidia mdogo wake aliyekuwa akihangaika.

Shahidi amedai mshitakiwa alimuonya asijaribu kusogea alipo ndugu yake, hivyo kutokana na hofu aliyopata kwa kuona mdogo wake amepigwa risasi, alimsihi Nyakai awaruhusu wambebe kumwahisha hospitali.

Amedai mshtakiwa alikataa akiwaeleza wasubiri gari la polisi lije, wakati huo ndugu yake alikuwa akivuja damu nyingi.

Shahidi alidai Nyakai alipoona gari halifiki aliwaruhusu kumpeleka hospitali ambako alifariki dunia.

Shahidi wa pili, aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Festo Ukulule ameeleza namna mshitakiwa alivyorudisha bunduki ikiwa na risasi 18 badala ya 20 alizopewa.

Pia alikwenda eneo la tukio alikoelezwa mgambo mmoja alipigwa na wananchi na alipelekwa kituo cha polisi upande wa Kenya lakini kulikuwa na taarifa hata polisi hao walishambuliwa.

Mashahidi wengine walikuwa daktari aliyechunguza mwili wa marehemu na maofisa wengine wa polisi ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine kukamata, kupeleleza na kuandika maelezo.

Kostebo Nyakai akijitetea amedai siku ya tukio yeye na ofisa mwenzake walichukua silaha na kupanda gari la TRA likiwa na maofisa wanne waliowaeleza watashirikiana katika doria.

Amedai wakiwa doria walikamata pikipiki kadhaa na baada ya ukaguzi waliziachia kwa kuwa utaratibu ulifuatwa wa kuingia nchini.

Ameeleza baadaye lilifika kundi la pikipiki maarufu bodaboda akamwagiza askari mwenzake kuzisimamisha.

Ameeleza walisimama baadhi wakaegesha katikati ya barabara na wengine walishuka, akashangaa kuwa walimzingira ofisa huyo.

Amedai madereva wa pikipiki walimkaba akapiga kelele kuomba msaada akieleza silaha yake iko hatarini, hivyo alimwelekeza kuondoa magazini kutoka kwenye bunduki yake, naye akajongea kuelekea alipo.

Mshtakiwa amedai aliweka risasi kwenye chemba kama njia ya kwanza ya kuwatisha wavamizi hao na kwamba, hiyo ndiyo njia ya kwanza katika kazi yoyote ya uokoaji pale polisi anapokuwa katika hatari.

Amedai alimshuhudia ofisa mwenzake akipigwa na kitu kizito kichwani na bega la kushoto akaanguka chini na bunduki yake ikiwa kifuani, kisha akashambuliwa akiwa ameanguka sakafuni.

Amedai alishuhudia bunduki ya askari mwenzake ikichukuliwa na wananchi, huku wakiendelea kuwashambulia kwa mawe.

Amedai wakati anajaribu kuweka mtutu uangalie chini huku akijitahidi asinyang’anywe silaha,  alipigwa kwa jiwe kubwa mgongoni na kuanguka chini huku aking’ang’ana kuzuia asiporwe silaha.

Ni katika hali hiyo, ghafla alisikia mlipuko mara mbili kutoka kwenye bunduki yake ambao ulimwangusha chini lakini walipomuona ameumia, wakaamua kumwachia kwa kuwa tayari kuna mtu amejeruhiwa.

Amedai maofisa wa TRA walikuwepo na hawakuweza kuwasaidia kwa kuwa hawakuwa na silaha.

Amejitetea kwamba baadaye aligundua risasi zilizotoka kwenye bunduki yake zilimpata marehemu mguuni.

Jaji Kafanabo katika hukumu aliyotoa Desemba 18, 2024 amesema ili kuthibitisha mtu ana hatia ya mauaji ya kukusudia ni lazima ithibitishwe kuwa kifo chake kimesababishwa na kitendo kisicho halali au dhamira ovu.

Amesema kulingana na ushahidi, hakuna ubishi kuwa kifo cha Masiaga kilikuwa si cha asili, hivyo hatua ya pili ni mahakama kujibu swali la ni nani alisababisha kifo hicho na adhabu yake.

Jaji amesema kwa kuchambua ushahidi uliotolewa, mahakama inathibitisha Koplo Nyakai ndiye aliyefyatua risasi mara mbili na kusababisha kifo, hivyo wajibu wa mahakama ni kupima kama kulikuwa na dhamira ovu.

“Kutokana na utetezi wa mshitakiwa, risasi ilifyatuka bila yeye kujua wakati akipambana asiporwe silaha na alikuwa anapambana silaha hiyo isiingie mikononi mwa wahalifu na wakati huo, tayari alishaikoki.

“Katika hatua hii ni lazima tuangalie ni mazingira gani polisi anaruhusiwa na sheria kutumia silaha,” amesema na kunukuu sheria kuwa anaweza kuitumia wakati akifanya ukamataji au inapolazimika kwa ajili ya kujilinda.

Hata hivyo, Jaji amesema chini ya sheria hiyo, ofisa wa polisi haruhusiwi kufyatua risasi kwa nia ya moja kwa moja ili kusababisha kifo, majeraha mabaya na badala yake anatakiwa kuielekeza kulenga miguu.

Jaji amesema kifungu hicho kinahalalisha mshitakiwa kupakia risasi au kuweka silaha yake katika hali ya kusubiri kwa madhumuni ya kumtetea polisi mwenzake Konstebo Charles ambaye alikuwa chini ya ulinzi wa wavamizi.

“Hoja ya msingi hapa ni kupima kama mshitakiwa alifyatua risasi kwenda kwa marehemu kwa makusudi na kama alidhamiria kusababisha majeraha mabaya kwa marehemu,” amesema na kueleza ilifyatuka bahati mbaya.

Jaji amesema katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulishindwa kuleta mashahidi muhimu ambao wangeweza kuisadia mahakama kuthibitisha shitaka la mauaji na kubakia na simulizi za shahidi pekee.

“Ni kutokana na uchambuzi wa ushahidi, mahakama inahitimisha kuwa mshitakiwa alimuua Masiaga bila kudhamiria. Kifo chake hakikusababishwa na mshitakiwa kwa makusudi,” amesema.

Jaji amesema kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kama mshitakiwa alikuwa na dhamira ovu kulingana na ushahidi uliopo, sheria inaelekeza kesi ya mashtaka iwe kuua bila kukusudia.

Amesema sheria inatoa adhabu ya juu ya kosa la kuua bila kukusudia kuwa kifungo cha maisha jela lakini kwa kuzingatia mazingira ya kosa, muda aliokaa gerezani na maombolezo anamfunga kifungo cha nje.

Jaji Kafanabo amemhukumu mshitakiwa kifungo cha nje cha miezi 12 na katika muda huo, hatakiwi kutenda kosa lolote la jinai na endapo atafanya hivyo, basi atawajibika kuhukumiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia.

Related Posts