Profesa Lwoga azikwa, wazungumzia alama alizoziacha

Morogoro. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kumpumzisha aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Anselm Lwoga ambaye amezikwa leo Desemba 21, 2024 huku akitajwa kuacha urithi wa tafiti na machapisho mengi.

Profesa Lwoga aliyezaliwa mwaka 1946, alifariki wiki iliyopita na amezikwa leo katika makaburi ya Kola yaliyopo Manispaa ya Morogoro na enzi za uhai wake,  amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Sua na baadaye Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa  Elimu ya Juu (HESLB).

Akisimulia namna alivyomfahamu na kufanya naye kazi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Raphael Chibunda amesema mwaka 1990, akiwa mwanafunzi wa Sua, ndipo alimfahamu marehemu Lwoga, wakati huo akiwa makamu mkuu wa chuo hicho.

“Nilifika hapa chuoni kama mwanafunzi na nilimkuta marehemu Profesa Lwoga akiwa ni makamu mkuu wa chuo hiki. Hakika nitamkumbuka kwa mengi, lakini kubwa ni namna alivyopenda kufuata utaratibu kwenye shughuli zake za kila siku, pia alikuwa tayari kumsikiliza yeyote aliyefika ofisini kwake na kumsaidia,” amesema Profesa Chibunda.

Amesema mwaka 2000 alirudi chuoni hapo kama mwajiriwa na kumkuta marehemu Lwoga akiwa amestaafu kama makamu mkuu wa chuo, lakini bado aliendelea kufanya kazi chuoni hapo kwenye moja ya vitivo, hata hivyo bado aliendelea kuwa kiungo muhimu kati ya uongozi wa chuo na wanafunzi.

Profesa Chibunda ameeleza historia ya kitaaluma ya marehemu Profesa Lwoga akisema awali akisoma Chuo Kikuu cha Makerere Uganda na baadaye alikwenda kusoma digrii yake nchini Uingereza, hata hivyo kwa namna alivyofanya vizuri katika chuo hicho, alipewa PhD badala ya shahada ya uzamili.

Amesema baada ya kutoka Uingereza, alirudi nchini na kuwa makamu mkuu wa chuo, mwaka 1988, ikiwa ni miaka minne imepita tangu kuanzishwa kwa chuo hicho na hivyo kuwa ni miongoni mwa wasomi wachache waliokiasisi chuo hicho.

“Wasomi wengi wa nchi hii, nikiwemo mimi mwenyewe, tumepita kwenye mikono yake na alijisikia fahari kubwa hasa kuona mafanikio ya mtu aliyepita kwenye mikono yake. Nchi imepoteza mtu makini na msomi,” amesema Profesa Chibunda.

Kwa upande wake, meneja biashara mstaafu wa Sua, Derek Murusuri amesema mchango wa marehemu Profesa Lwoga hautasahaulika kwani ameacha alama zikiwemo tafiti na machapisho mbalimbali ambayo yanasomwa na kutumiwa kwa maendeleo ya nchi.

Murusuri amewataka vijana wasomi kusoma vitabu na machapisho ya wasomi wa zamani kama ya marehemu Profesa Lwoga ili waweze kupata ujuzi na maarifa yatakayoweza kuwafanya nao wawe wasomi wakubwa watakaoweza kulisaidia Taifa.

Awali, mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga amesema sio tu wamempoteza baba, bali kiongozi wa familia, mlezi na mtu aliyependa maendeleo.

Dk Lwoga amesema baba yao amefanya kazi kama makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sua kwa miaka 18 na amefanya tafiti nyingine na kuandika machapisho mengi ambayo yataishi na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

“Baba aliipenda familia yake na hata sisi watoto wake alitufundisha kupenda familia na kupendana sisi wenyewe kama watoto. Aliishi vema na watu wote waliomzunguka kuanzia chuoni hadi nyumbani na kwenye familia na mara zote aliamini kwenye uadilifu na ndiyo maana hata baada ya kustaafu Sua aliteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,” amesema Dk Lwoga.

Related Posts