Siku 10 zasalia ahadi ya mabasi Dart

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 10 kuhitimisha Desemba iliyoahidiwa kuwasili mabasi ya mwendo wa haraka, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), umesema suala hilo lipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye naye ameeleza litakamilika ndani ya Desemba.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu utekelezaji wa agizo la Serikali kuwa mabasi hayo yawe yamewasili Desemba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Dart, William Gatambi amesema suala hilo lipo mikononi mwa AG.

Agosti 2, 2024 akizindua mageti na kadi janja kwa ajili ya usafiri huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, aliiagiza Dart ifikapo Desemba 2024, mabasi ya mwendokasi yanayotakiwa katika barabara ya Morogoro na ile ya Mbagala yawe yamepatikana.

Mchengerwa alisema wananchi wamechoka na danadana za ujio wa mabasi hayo, akaagiza Desemba iwe mwisho, yawe yamekuja lakini mpaka sasa ukimya umetawala.

“Watanzania wamesubiri kwa muda mrefu kupatikana kwa mabasi hayo na sasa inatosha, hatatuki tena kusikia changamoto hii wizarani.

“Pia lile suala linaloitwa mchakato kila siku wala ubishani kuhusu utekelezaji wa suala hilo kati ya Wakala wa Mabasi (Dart) na Kampuni ya uendeshji Mradi (Udart) nisisikie,” aliagiza Mchengerwa.

Alisema taarifa alizokuwa nazo ni kuwa, Barabara ya Morogoro inahitaji mabasi 170, huku ile ya Mbagala ikihitaji mabasi 500.

Mwananchi ilipozungumza na AG, Johari Hamza jana Desemba 20, 2024 alikiri suala hilo limeshamfikia na linafanyiwa kazi.

Johari alisema wanatarajia kukamilisha mchakato kabla ya Desemba kwisha kama ilivyoagizwa na Serikali.

Akizungumzia mchakato huo kuchukua muda mrefu alisema: “Hii ni kutokana na mradi huo kuhusisha taasisi nyingi, hivyo kila mahali Serikali lazima kujiridhisha kabla ya kuingia mkataba.

“Niwaombe wananchi wawe na subira, Desemba hii kabla haijaisha, mkataba utakuwa umesainiwa kama ambavyo Serikali iliahidi,” amesema.

Gatambi amesema katika utekelezaji wa agizo la Serikali, kazi waliyofanya ni kufuata taratibu za kupata dhamana ya Serikali kuwezesha mkataba kati ya Dart na mwekezaji Emirates National Group (ENG) kutoka Falme za Kiarabu.

“Dhamana ya Serikali imepitia ngazi mbalimbali na sasa ipo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikitoka hapo kitakachofuata ni kufuata taratibu zingine za kuleta mabasi,” amesema.

Amesema mwekezaji ataleta mabasi kwa ajili ya awamu ya kwanza inayohusisha barabara ya Morogoro, kazi ambayo atapaswa kuitekeleza ndani ya miezi mitatu tangu watakaposaini mkataba.

Kwa barabara ya Mbagala, amesema wameshaanza upembuzi yakinifu na kinachosubiriwa ni kupitiwa na kupewa idhini na kamati ya uongozi.

“Katika barabara ya Morogoro, baada ya kamati kumaliza kazi yake na kupata idhini, taratibu zingine za mabasi awamu ya pili ya barabara iendayo Mbagala zitaendelea.

“Kwa hiyo zote hizo zinafanyiwa kazi kwa hatua mbalimbali ambazo nimezitaja, huku zile za awamu ya tatu na ya nne, nazo zipo katika hatua mbalimbali ambazo hatuwezi kuzizungumzia kwa sasa,” amesema.

Amesema ujenzi wa barabara utakapokamilika na ujio wa mabasi utakuwa umekamilika.

Obadia Alphonce, mkazi wa Mbezi anayetumia usafiri huo amesema wamechoka na ahadi zisizotekelezwa, akisema kwa sasa usafiri umekuwa mgumu kutokana na mabasi kuwa machache.

Charity Maimu, mkazi wa Mbagala, amesema barabara imeshakamilika, hivyo Serikali ipeleke mabasi ili waondokane na adha iliyopo ya usafiri.

Katika usanifu wa awamu ya kwanza ya mradi huo, kwa mujibu wa Dart mabasi yaliyotakiwa ni 305 lakini kimkataba yalitakiwa yawe 210 kwa mwekezaji Udart.

Hivyo, mwekezaji anayekuja anapaswa kuongeza mabasi 177 na endapo yataonekana hayatoshi ataruhusiwa kuleta mengine.

Awali, wakati mradi huo unaanza kufanya kazi mwaka 2016, Udart ilileta mabasi 140 baadaye ikaongeza 70.

Hata hivyo, kutokana na mabasi mengine kuchakaa na kuharibika, hivi sasa yanayofanya kazi barabarani hayazidi 100.

Kwa barabara ya Mbagala katika usanifu mabasi 755 ndiyo yanayotakiwa.

Related Posts