WANASIMBA walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kumshuhudia nyota mpya, Elie Mpanzu ambaye jioni ya leo alitumia dakika 57 pekee kuonyesha umwamba wakati Simba ikishinda mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Mpanzu aliyetambulishwa Simba, Septemba 30 mwaka huu akitokea AS Vita ya DR Congo, leo akiwa na jezi namba 34 alicheza mchezo wa kwanza wa kimashindano akiwa na kikosi hicho na kuisaidia kupata ushindi huo mnono na kurejea kileleni ikiitoa Azam iliyokuwa hapo muda mrefu.
Simba imefikisha pointi 34, moja zaidi na ilizonazo Azam iliyokamilisha mechi 15 za duru la kwanza, tofauti na Simba iliyocheza mechi ya 13 leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Katika mchezo huo, Mpanzu licha ya kutofunga bao, lakini alionyesha ana kitu cha kuisaidia Simba katika mechi zijazo kutokana na ubora wake.
Winga huyo ameonekana kuwa mtulivu anapomiliki mpira kwani haikuwa rahisi kupoteza pasi kwani asilimia kubwa alizopiga zilifika kwa walengwa.
Usumbufu wake kwa wapinzani, uliwafanya Kagera kumchezea faulo mara nne huku moja akimsababishia Hija Shamte kadi ya njano kipindi cha pili.
Mbali na kuwasumbua Kagera kwa kasi yake, chenga na pasi za uhakika, pia Mpanzu alionyesha umahiri wa kupiga mashuti langoni mwa wapinzani akifanya hivyo mara mbili na yote yalilenga lango. Hakuna shuti alilopiga nje akitumia miguu yote miwili kwa ufasaha.
Hata hivyo, Mpanzu anaonekana si mzuri kwa kupiga krosi kwani alijaribu moja haikuwa na manufaa, akaamua kubadili mtindo wa uchezaji, akawa anaingia ndani anapopata mpira kutokea pembeni.
Wakati mchezo unaanza, Mpanzu alikuwa akitokea pembeni lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda, alikuwa akibadilishana na Awesu Awesu na Jean Charles Ahoua kuingia ndani.
Akiwa ndani akicheza namba 10, alionekana kuisumbua vilivyo safu ya kiungo na ulinzi ya Kagera Sugar iliyokuwa makini kwenda kumkaba kwani walitambua wakienda vibaya wanamchezea faulo au wanapitwa kirahisi.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, dakika zake 57 zilitosha kuvuja jasho ambapo alimpisha Joshua Mutale kumalizia mchezo huo.
Wakati Mpanzu akianza kuonyesha makeke yake, Jean Charles Ahoua ameendelea kudhihirisha kwamba ni mtu muhimu katika kikosi cha Simba baada ya kufunga bao lake la sita kwenye ligi msimu huu akiwa kinara wa ufungaji kikosini hapo.
Ahoua ambaye pia ana asisti nne, alifunga bao hilo dakika ya 44 kwa pigo la faulo ya moja kwa moja nje kidogo ya eneo la hatari la Kagera Sugar. Faulo hiyo ilitokana na yeye mwenyewe kuchezesha vibaya na beki wa Kagera Sugar, Abdallah Mfuko wakati wa kumzuia asimfikie kipa wake, Ramadhan Chalamanda.
Kabla ya Ahoua, Shomari Kapombe alifungua akaunti ya mabao katika mchezo huo dakika ya 13 akimalizia krosi ya Mohamed Hussien ‘Tshabalala’.
Hilo lilikuwa ni bao la pili kwa Kapombe katika ligi msimu huu wakati Tshabalala akifikisha asisti ya tatu.
Fabrice Ngoma aliongeza bao la tatu dakika ya 54 kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Ladack Chasambi ambaye aliingia uwanjani dakika ya 41 kuchukua nafasi ya Awesu. Hilo likiwa la pili kwake msimu huu.
Steven Mukwala aliongeza bao la nne dakika ya 68 akimalizia pasi ya Chasambi ambaye katika mchezo huo alitoa asisti tatu ikiwemo ya bao la tano lililofungwa pia na Mukwala dakika ya 84.
Kagera Sugar walitibua rekodi ya Simba kucheza mechi sita mfululizo bila ya kuruhusu bao baada ya Datius Peter kufunga dakika ya 80 akimchambua vizuri kipa Moussa Camara ambaye anaongoza kwa clean sheet akiwa nazo 10 katika mechi 13 huku pia Cleophace Mkandala akifunga dakika ya 90+3.
Kocha Melis Medo wa Kagera Sugar, alijaribu kuimarisha kikosi chake ili kuepuka na kipigo hicho lakini hakufanikiwa licha ya kwamba kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne akiwatoa Jofrey Manyasi, Erick Mwijage, Saleh Kambenga na Peter Lwasa nafasi zao zikichukuliwa na Joseph Mahundi, Deogratius Mafie, Samweli Onditi na Tariq Kiakala.
Fadlu Davids naye alifanya mabadiliko ya wachezaji kwenye kikosi cha Simba kwani licha ya kumtoa Awesu na kuingia Chasambi, pia aliwatoa Fabrice Ngoma, Elie Mpanzu, Shomari Kapombe na Debora Mavambo wakaingia Yusuph Kagoma, Joshua Mutale, Kelvin Kijiri na Mzamiru Yassin.
Simba itarudi jijini Dar es salaam kujiandaa kuvaana na Tanzania Prisons ambayo kesho jioni itakuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge kupepetana na watetezi wa Ligi Kuu, Yanga katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara iliyokamilisha mechi za duru la kwanza isipokuwa kwa baadhi ya timu vikiwa vigogo hivyo.