Simba, Yanga zambakisha Karia madarakani, TFF yafafanua

Klabu za Simba na Yanga kwa pamoja zimeshawishi wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF, kuamua Wallace Karia aendelee kuwa rais wa shirikisho hilo kwa awamu ijayo kabla hata ya uchaguzi wake mwakani kutokana na kile zilichosema ni kuridhishwa na kazi nzuri ambayo ameifanya kwa miaka saba iliyopita.

Hata hivyo, shirikisho hilo kupitia kwa makamu wa kwanza wa rais wa TFF, Athuman Nyamlani limejibu kuwa njia bora ya kufanya hivyo ni wanachama wote wa shirikisho hilo kumuwekea dhamana (endorsement) mara akishachukua fomu ya kuwania urais na sio kutofanya uchaguzi wa nafasi yake kama uongozi wa Yanga na Simba ulivyoshauri.

Hoja ya kutaka kusifanyike uchaguzi wa nafasi ya urais wa TFF mwakani ilianzishwa na mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu katika mkutano wa mwaka wa shirikisho hilo uliofanyika Kilimanjaro leo na kisha baadaye ikaungwa mkono na Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said.

“Dhumuni na dhamira rasmi ya kuwa na shirikisho kwamba ndio kilele cha uongozi wa soka katika nchi yetu. Umezungumzia mafanikio ya timu ya taifa ya vijana, timu ya taifa ya wakubwa, timu za taifa za wanawake, soka la ufukweni, hayo ndio mambo ambayo sisi wajumbe wako tunayatamani yawe yanatokea.

Hoja yangu, katiba ya TFF Ibara ya 25(1) na Ibara ya 27(C) imetoa wigo mpana na mamlaka ya kimaamuzi ya mkutano mkuu huu. Maamuzi yanayofanywa na mkutano mkuu huu hayawezi kupingwa na chombo kingine chochote. Tanzania ni sifa yetu kutokuwa na ‘consistency’ (muendelezo). Tunaweza tukaanzisha jambo zuri lakini tukafika kati tukakwama.

Wewe umefanya kazi nzuri sana tukupongeze. Kazi hiyo nzuri inastahili upewe tuzo. Chanda chema huvikwa pete na tuzo yenyewe uchaguzi wa Rais wa TFF mwakani unaoutaka wa nini? Mkutano ukuthibitishe leo. Hawa wajumbe wa kamati ya utendaji ndio tutakwenda kwenye uchaguzi lakini hili la rais kwanza tuwe tumemaliza, simamia hili jambo vizuri ili twende mbele. Ambaye atachukua fomu hiyo mwakani atakuja kutueleza jambo gani kubwa ambalo wewe umeshindwa kulifanya?,” alisema Mangungu.

Hersi aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa hakuna sababu ya kufanya uchaguzi wa nafasi ya urais ili kutoa heshima kwa kile kilichofanywa na Karia.

“Mafanikio makubwa ambayo Rais pamoja na kamati ya utendaji ya TFF yamekuwa ni sababu kubwa ya maendeleo ya mpira wa miguu katika taifa letu. Sisi kama wadau wa soka katika taifa hili tunajivunia utendaji wako mheshimiwa Rais.

Kwa nafasi hii ndogo niliyopewa mheshimiwa Rais nikuhakikishie ya kwamba sisi wadau wa michezo tutaendelea kukuunga mkono wewe na kamati yako ya utendaji na nipongeze wazo zuri ambalo kaka yangu, Murtaza Mangungu amelitoa kwa asilimia mia moja. Kwa
Muktadha huo tutakuwa na uchaguzi wa idara nyingine kama za wajumbe wa kamati ya utendaji na sio eneo la rais,” alisema Hersi.

Akijibu maoni hayo, Nyamlani alisema kwa dhana ya utawala bora, kufanyika kwa uchaguzi ni njia nzuri ingawa kinachoweza kufanywa na wanachama wa TFF ni wote kumdhamini Karia ili kusiwepo na mshindani mwingine katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.

“Kwanza ni hoja nzuri lakini tunaweza tukaiboresha ili tusivuruge katiba yetu. Takwa la uchaguzi ni takwa la kikatiba. Tunaweza tukahemewa tukatengeneza mazingira huko mikoani na wilayani huko kukawa na balaa zaidi.

“Kwa hiyo tunachoweza kufanya kwa vile rais wetu amefanya kazi kubwa na sisi ni mashuhuda wa kazi ambayo rais ameifanya. Na sisi ni masikini, hatuna mali ya kumuenzi rais wetu. Kumuenzi kwetu rais wetu ni kumuunga mkono sasa tunamuungaje mkono? Ndio hoja iliyopo mezani.

“Mtoa hoja alikuwa anazungumzia tumpitishe rais kwa azimio. Wanasheria wenzetu katika mambo ya utawala bora watasema haijakaa vizuri. Basi mimi nishauri, Katika kugombea urais wa TFF kuna takwa la kikatiba la kupata endorsement kutoka kwa wanachama wa TFF. Tukubaliane na kaazimio kidogo kwamba mkutano huu umeazimia kwamba wote tumpe endorsement rais atakapogombea,” alisema Nyamlani.

Nyamlani alisema kuwa suala hilo sio geni na linafanyika sana kwenye mpira wa miguu.

Related Posts