Utata mtoto aliyefia kwenye shimo la choo

Dodoma. Utata umeibuka kuhusu mtoto Emmanuel Elias, mwenye mwaka mmoja na nusu kutumbukia kwenye shimo la choo, baada ya mama yake kukuta karatasi mlangoni kwake ikimuarifu kuhusu tukio hilo.

Mwili wa mtoto huo uliopolewa jana usiku Desemba 20, 2024 na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika shimo la choo ambacho kinatumiwa na familia zaidi ya tatu, zilizopanga nyumba mmoja iliyopo Mtaa wa Nzuguni B, jijini Dodoma.

Akizungumza leo Desemba 21, 2024 jirani wa familia hiyo, Ester Lusinde amesema mama wa mtoto huyo alimwamsha mwanawe jana saa 11:00 jioni akambadilisha nguo, kisha akaenda kucheza na wenzake maeneo ya jirani.

Amesema saa 12:00 jioni mama huyo alikwenda kumtafuta kwa kuwa hakuwa amerejea nyumbani lakini hakumpata, hivyo aliwaeleza wenzake.

Amesema wenzake walimweleza waende kwa balozi kutoa taarifa lakini wakati wanarudi nyumbani saa 2:30 usiku walikuta karatasi imewekwa mlangoni imeandikwa: “Mtoto wako ametumbukia kwenye shimo, sitaki ushahidi.”

Lusinde amesema mwili wa mtoto huyo uliopolewa saa 5:00 usiku na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Kitendo hiki kinaonyesha kuna mtu alishuhudia tukio hilo lakini hakusema hadi saa nne zilipopita,” amesema mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake kutajwa.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo jana usiku, Ofisa Oparesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Inspekta Deogratius Inano, amesema kifo cha mtoto huyo kinazua maswali mengi katika jamii hiyo.

Hata hivyo, amesema jambo la msingi ni wazazi kuwa waangalifu kwa watoto hasa kipindi hiki ambacho shule zimefungwa.

Amesema Mkoa wa Dodoma, hasa kata ya Nzuguni imekuwa na matukio ya watoto kutumbukia kwenye mashimo nyakati za mvua sababu zikitajwa ni watu kutokufunika mashimo ya vyoo na uangalizi mdogo kwa watoto.

“Kwa mwaka huu hili ni tukio la kwanza hapa Nzuguni, lakini ni tukio la pili kwani juzi tumeopoa mwili wa mtoto wa miaka 10 katika Kata ya Mkonze aliyekufa kwa kutumbukia kwenye dimbwi, wazazi na walezi tuwe makini na watoto wetu nyakati hizi,” amesema.

Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega ameagiza viongozi katika mtaa huo kufanya ukaguzi kubaini mashimo yaliyo wazi na itolewe amri ya kuyafukia haraka iwezekanvyo.

Amewaomba wakazi wa mtaa huo kutochochea maneno ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani, badala yake watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kama kuna mtu anayejua ukweli kuhusu kutumbukia shimoni kwa mtoto huyo na hasa mazingira yalivyokuwa.

Luhega amesema mtindo wa kutofunika mashimo ya vyoo umekuwa kama mazoea kwa baadhi ya wananchi,  bila kujali mazingira halisi wanayoishi kwamba yanahatarisha usalama wao.

Related Posts