WAKATI Yanga ikiwa na mpango wa kumsajili beki wa kati kutoka Zanzibar, ghafla mabosi wa AS Vita Club ya DR Congo wameibuka na mkakati wa kuhakikisha wanainasa saini ya nyota huyo ili akakiongezee nguvu kikosi hicho.
Yanga ilishaonyesha nia ya kuihitaji saini ya nyota huyo ambaye ni panga pangua ndani ya Fountain baada ya uwezekano wa kumpata beki wa Coastal Union, Lameck Lawi kuonekana kuingia dosari, kufuatia Simba kuingilia kati kuhusu dili hilo.
Wakati hayo yakiendelea, Yanga ikaangalia uwezekano wa kumpata Makame ikiamini ni beki mzuri mzawa anayeweza kuongezea nguvu.Sasa wakati Yanga ikipiga hesabu hizo, ghafla AS Vita Club imepiga tena hodi Fountain kumuhitaji beki huyo ikiwa ni pendekezo la kocha wa zamani wa Azam FC, raia wa Senegali, Youssouph Dabo anayemuhitaji ili kuongeza nguvu kikosi hicho.
“Ni kweli AS Vita wametuulizia juu ya upatikanaji wa beki wetu lakini hatujafikia makubaliano yoyote, Makame ni miongoni mwa mabeki bora hapa nchini hivyo sisi kama uongozi hatushangai akigombaniwa na klabu nyingi,” kilisema chanzo chetu.
Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha ambaye hakutaka kuweka wazi juu ya suala hilo, zaidi ya kusema ni muda wa usajili na kila mmoja wao anazungumza lile analoliona kwa maslahi yake.
Kocha wa AS Vita Club, Youssouph Dabo alisema hawezi kuzungumzia mchezaji wa timu nyingine, kwa sababu ni muumini wa kuheshimu na kufuata taratibu.