Dodoma. Watu watatu wamejeruhiwa kwa kukatwa kwa mapanga katika Mtaa wa Msangalalee Magharibi, Kata ya Dodoma Makulu na kikundi cha uhalifu cha watoto wenye umri chini ya miaka 18, baada ya kuwanyima fedha walizoomba.
Matukio hayo yametokea kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 12 hadi 14, 2024 kati ya saa 2:00 usiku hadi saa 3:30 usiku waathiriwa walipokuwa wakirejea nyumbani.
Zakayo Mussa, aliyejeruhiwa katika moja ya tukio amesema alivamiwa na vijana wanne mwenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 ambao kati yao alimfahamu mmoja aliyewaeleza wenzake kuwa yeye ni mjomba wake Agape.
“Wakati huo nilikuwa nimeazima pikipiki ya rafiki yangu, nilikuwa nimesimama namsubiri ili nimkabidhi. Ghafla wakatokea vijana wanne wakiwa wameshika mapanga, mmoja akawaambia wenzake huyu si mjomba wake na Agape, kabla sijajua lengo lao walianza kunishambulia na mapanga. Walinikata mara mbili kichwani, nilipiga kelele kuomba msaada wakakimbia,” amesema Mussa.
Amesema vijana hao ambao hawafahamu, hawakuchukua chochote wala hawakuomba kitu. Tukio hilo anasema lilitokea Desemba 14, saa 3:30 usiku eneo la Mkalama MPesa.
Amesema walimjeruhi kichwani na usoni, akalazimika kushindwa.
Salim Aboubakar, mkazi wa Mtaa wa Mkalama amesema alijeruhiwa kwa kukatwa kwa panga Desemba 12, saa 2:00 usiku alipokuwa anarudi nyumbani.
Amesema baada ya kushuka kwenye daladala alikutana na vijana watatu wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 waliomuomba Sh500.
“Waliniuliza una jero (Sh500) nikawaambia sina ndipo mmoja akanikata kwa panga mkononi, nilipopiga kelele kuomba msaada walikimbia.
“Baadhi ya watu walikuja kunisaidia akiwemo ndugu yangu. Tulipowatafuta tuliwakuta wamejificha nyuma ya mgahawa, waliponiona mmoja alichomoa tena panga na kutaka kunikata,” amesema.
Amesema alikimbia kujiokoa lakini kutokana na utelezi alianguka, huku aliyekuwa akimkimbiza naye alianguka na katika kunyang’anyana panga alijikata kidole mkononi.
Amesema alipata msaada wa kwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa aliyeshauri apelekwe hospitalini kwa kuwa alikuwa kivuja damu nyingi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Msangalalee Magharibi, Leonard Ndama amekiri kuyafahamu matukio hayo.
Amesema baadhi ya wahalifu wamekamatwa na kufikishwa polisi kwa hatua za kisheria, akisema mmoja wa watuhumiwa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye miaka 15.
Amesema alisimamishwa shule baada ya kubainika anatumia dawa za kulevya aina ya bangi. Ameeleza mtaani hapo kuna korongo ambalo hulitumia kuvuta bangi.
Amesema mtaa una wakazi 20,365 lakini mgambo waliopo ni wanne hivyo hawawezi kudhibiti matukio yote ya uhalifu yanapotokea.
“Tunaliomba Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye mtaa wetu kwa sababu hali ni mbaya, watu wanajifungia majumbani kuanzia saa moja usiku, wanaogopa kukutana na hawa vijana kwa sababu wakikuomba hela kama huna wanakujeruhi, hatua zisipochukuliwa mapema watasababisha vifo,” amesema Ndama.
Mkazi wa Mtaa wa Mkalama Mpesa, Emmy Mchiwa anafanya shughuli za mama lishe ameomba serikali ya mtaa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwakamata wahalifu hao.
“Tunajua dhamana ni haki ya kila mwananchi lakini hawa vijana wakishawekewa dhamana na wazazi wao wanakuja kwa kasi mpya tena kwa kujitangaza kuwa wameshazoea kukaa gerezani kwa hiyo hakuna wa kuwatisha,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara kwenye mitaa yote ya Jiji la Dodoma ili kudhibiti vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikifanywa na makundi ya wahalifu ambayo kwa kiasi kikubwa wameyadhibiti makundi hayo.
Amesema Mkoa wa Dodoma kwa sasa umetulia kutokana na matukio ya uhalifu yakiwamo uporaji, uvunjaji na wizi wa kutumia silaha ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Tunafanya doria za mara kwa mara na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya kwa pamoja tumekamata wauzaji wakubwa wakiwamo wa bangi na tumewafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi,” amesema.
Amesema Jeshi hilo hufanya mikutano na wananchi kupitia kwa viongozi wao wa mitaa na wa dini katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
“Niwaombe wenyeviti wa serikali za mitaa wanapokutana na watu wanaofanya vitendo vya uhalifu wawasiliane na Jeshi la Polisi badala ya kukaa kimya, kwani wasipotoa taarifa halitajua kama kuna vikundi vya wahalifu,” amesema.