Kagera. Watu 11 wamefariki dunia na wengine 16 wamejeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Capco One kufeli breki na kuseleleka kinyumenyume kisha kugonga gari dogo.
Tukio hilo limetokea jana Jumamosi Desemba 21, 2024 katika Kijiji cha Kabango eneo la milima pori la Kasibdaga, Wilaya Biharamulo mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Brasius Chatanda ajali hiyo imetokea saa 8 mchana baada ya basi hilo kufeli breki na kuanza kurudi nyuma wakati kondakta akimshusha mtoto.
“Gari hilo lilokuwa limesimama likimsubiri kondakta aliyekuwa amempeleka mtoto kwenye gari jingine ambalo lilikuwa linarudi wilayani Muleba, baada ya kumpitisha kituo. Hivyo ghafla lilianza kurudi nyuma ambapo dereva alijitahidi kulidhibiti lakini lilimshinda na kuporomoka hadi kwenye korongo,” amesema.
“Gari liligeuka na kusababisha kukatika sehemu ya juu, vikabakia viti na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 16. Tunaendelea na uchunguzi zaidi,” amesema Kamanda Chatanda.
Endelea kufuatilia Mwananchi ili kupata taarifa zaidi..