Moshi. Baada ya mvutano wa siku 28 wa familia ya Mosha kuhusu eneo atakalozikwa kijana wao, Gilbard Mosha (41) aliyefariki dunia Tunduma mkoani Mbeya, hatimaye familia bila kuelewana wamelazimika kuuzika mwili huo.
Gilbard aliyefariki dunia Novemba 27, mwaka huu, mwili wake umezikwa jana Desemba 21, katika kitongoji cha Koniko B, kijiji cha Rauya, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo, haikuwa rahisi maziko hayo kufanyika, kwani upande mmoja wa familia yake ulitaka azikwe Koniko B, huku mwingine ukitaka azikwe Maji ya chai, Arusha.
Kutokana na mazingira hayo, upande wa waliotaka azikwe Maji ya Chai, walifunga geti na hivyo kuzua taharuki na vurugu mazikoni hapo, zilizosababisha maziko hayo kufanyika chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Akizungumza na Mwananchi Digital, baba mdogo wa marehemu, Josephat Mosha amedai eneo la Koniko B siko alikopaswa kuzikwa, badala yake alipaswa azikwe Arusha alikopewa enzi za uhai wake.
Bibi wa marehemu, Justar Mosha alikosoa hatua ya baba mdogo kupinga maziko kufanyika katika eneo hilo, akisema hakuna mgogoro wowote katika eneo alikozikwa.
“Wazazi wa huyu kijana wamezikwa wote hapa Rauya iweje huyu baba mdogo wake akatae, hii sio sawa hata kama alipewa eneo jingine haimaanishi asizikwe sehemu moja pamoja na wazazi wake,” amesema.
Joseph Mosha ni msimamizi wa mirathi wa familia ya mzee Mosha, amesema alikuwa akipinga marehemu kuzikwa eneo hilo kutokana na wosia aliouacha marehemu baba yake.
Amesema eneo hilo aliachiwa mdogo wa marehemu kwa mujibu wa wosia na hivyo marehemu alipaswa kuzikwa kwenye eneo lake alilopewa mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Koniko B, Godfrey Shirima amesema mgogoro huo ulipaswa kusuluhishwa mapema ili kuepusha vurugu zinazotokea sasa.
“Suala hili lingeweza kumalizwa kwa mazungumzo ya familia, eneo ambalo baba wa marehemu alimpa linapaswa kuheshimiwa, lakini vurugu kama hizi hazina tija,” amesema Shirima.