Anti, kuna vitu hadi vinatia aibu kuvisema hadharani, unajua mke wangu ananipiga ndole (kuchomoa pesa) kila ninaporudi nyumbani na kuvua suruali.
Kuna wakati natamani nilale na suruali maana nikivua tu ananisachi. Nimesema, nimelalamika mpaka nimechoka, ningekuwa ninakunywa pombe angekuwa anasema nimepoteza nilipokuwa baa au nilipoolewa, kwangu amekosa kisingizio.
Ninarudi na akili zangu timamu na ninajua mfukoni nina kiasi gani, ila si jambo rahisi kuzikuta asubuhi. Anakomba ukifanya masihara zote.
Siyo kwamba simpi pesa ya matumizi, ninampa na kila kitu kipo ndani hata sijui anasumbuliwa na nini?
Kibaya zaidi kila nikimuuliza anataka kufanya shughuli gani ya kujiingizia kipato hana anachonijibu.
Awali nilijua anakuwa na hekaheka za kulea maana watoto wetu watatu tuliwazaa harakaharaka. Hivi sasa mtoto wetu wa mwisho ana miaka minane, lakini hataki kujishughulisha na chochote na wazo la kitu cha kufanya pia hana.
Nilimtuma hadi dada yake amuulize lakini hakuna cha maana alichomjibu zaidi ya kusema siwezi kumpa pesa ya mtaji namtania. Basi hata simuelewi.
Nipe mbinu ili angalau vichenji ninavyorudi navyo nyumbani vipone.
….Pole sana. Ila huu ugonjwa umeufuga tangu alipoanza hukuukemea kwa nguvu zaidi ya kusema tu. Ili kukomesha hii tabia ungeweka mtego ili umnase kwa ushahidi kisha umshirikishe kwenye hiyo kesi shangazi yake au bibi yake, kwani wao ndio wana jukumu la kumfundisha binti yao tabia njema.
Wizi ni kitu kibaya kwa wote, lakini unapofanywa na mwanamke unakuwa mbaya zaidi, kwani kiasili mwanamke hana haiba ya mambo hayo.
Ila hata sasa dawa unayo. Kuanzia leo ukirudi kazini pesa ulizorudi nazo ziweke mezani mahali peupe na uwe mkali asichukue hata senti tano kwa sababu pesa zake za matumizi unampa.
Pia unaweza kumpa akushikie utazichukua asubuhi, ukifanya hivi mara mbili tatu atajua umechoka tabia yake ya wizi na akichukua hata senti tano kesi yake iwe kubwa sana hadi akuombe msamaha.
Wewe ni baba wa familia, usikubali mkeo awe na tabia mbaya tena ya wizi. Ikitokea amechukua katika hizo ulizompa washirikishe watu muhimu kwenye familia, wakiwamo niliowataja hapo awali, ukishindwa washirikishe wasimamizi wenu wa ndoa.
Muhimu hakikisha watoto hawasikii mabishano yenu kuhusu mkeo kukuibia pesa mifukoni kwa sababu atawaharibu, itawaathiri wanaweza kuona hilo ni jambo jema wakaliiga huko waendako au jambo baya wakamchukia mama yao. Kwa namna yoyote ile linaweza kuwaathiri kwenye maisha yao.
Pia mkeo kama ni mama wa nyumbani mtafutie shughuli ya kufanya kwa sababu akijua uchungu wa kutafuta pesa hatathubutu kumuibia mwingine, ataelewa namna inavyouma kuibiwa pesa uliyoitafuta kwa jasho.
Hili suala la kusema hataki kujishughulisha halina maana, lazima ajishughulishe kama binadamu, kukaa bila shughuli ndiyo maana anakuwa na tabia mbaya.
Kumshirikisha kuhusu shughuli ya kufanya ni jambo jema, wakati huu unakomesha tabia ya wizi kwa msimamo mkali, hapo hapo akueleze anataka kufanya shughuli gani ya kujiingizia kipato. Uipime na uone kama ina masilahi, asije akachagua jambo lisilowezekana akaleta hasara mkashindwa kuelewana. Unaweza kumsaidia mawazo kama una unachokifikiria mkakijadili kwa pamoja na kufikia muafaka.